33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ulinzi waimarishwa Dodoma

Mjini Dodoma
Mjini Dodoma

DEBORA SANJA, DODOMA NA ESTHER MBUSSI, DAR

VIKOSI vya ulinzi na usalama, vimeimarisha ulinzi mkoani Dodoma ikiwa ni maandalizi ya sherehe za kukabidhi Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Kukabidhiwa kwa Katiba hiyo kunahitimisha uhai wa siku 90 za Bunge la Katiba ambalo lilianza vikao vyake Februari 18 hadi Aprili 25, mwaka huu kwa kupisha vikao vya Bunge la Bajeti.

Awamu ya pili ya uhai wa Bunge hilo ilianza tena kuanzia Agosti 5, hadi Septemba 4, mwaka huu, kwa kupiga kura za Ndiyo na Hapana ili kukubali kuunga mkono kwa Katiba iliyopendekezwa na Bunge hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, itahakikisha sherehe hizo za kihistoria zinamalizika kwa salama na amani.

Alisema sherehe hizo za makabidhiano zitafanyika kesho katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

“Taifa lote litahamia Dodoma, nasi kama viongozi tumejipanga kuhakikisha ulinzi na usalama unakuwapo wakati wote wa tukio hilo la kitaifa.

“Viongozi wa juu wa Serikali, na taasisi mbalimbali na mabalozi kutoka nchi mbalimbali watakuwapo kushuhudia makabidhiano hayo,” alisema.

Alisema bado hawajawa na uhakika wa viongozi kutoka nchi nyingine ikiwamo nchi za jirani kama wataweza kuhudhuria sherehe hizo.

“Kama wasipoweza kuhudhuria, wanaweza wakawapo katika tukio kama hili ambalo litafanyika pia Zanzibar,” alisema.

Alisema mbali na viongozi hao, pia wawakilishi wa makundi mbalimbali watahudhuria sherehe hizo na kwamba mikoa husika itahusika katika kuratibu kufika kwa makundi hayo Dodoma.

“Sherehe zinatarajiwa kuanza majira ya saa tano asubuhi, lakini milango ya uwanja wa Jamhuri itakuwa wazi kuanzia saa 12 asubuhi,” alisema Dk. Nchimbi.

Alisema tukio hilo litatanguliwa na dua maalumu ambayo inafanyika leo katika viwanja vya Nyerere Square na itahudhuriwa na viongozi wa Serikali, taasisi za umma na binafsi pamoja na viongozi wa dini.

“Dua hiyo itaongozwa na viongozi wakuu wa dini wa Mkoa wa Dodoma kutoka TEC (Baraza la Maaskofu) CCT (Jumuiya ya Makanisa ya Kikristo), Bakwata (Baraza la Waislamu), FTC na Singasinga,” alisema.

Wakati maandalizi ya kukabidhiwa kwa Katiba inayopendekezwa kesho yakiendelea, baadhi ya viongozi wa kitaifa wa vyama za upinzani nchini pamoja na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wamekanusha kupokea mwaliko huo.

JAJI WARIOBA

Akizungumza na MTANZANIA, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisema hajapata mwaliko wa kuhudhuria hafla hiyo.

“Sijapata mwaliko, nikipata nita-decide (nitaamua) kama nitakwenda au la, ila kwa sasa sijajua kwa sababu sina mwaliko huo,” alisema Jaji Warioba kwa kifupi.

CHADEMA

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema hajapata mwaliko, lakini hata akipata hawezi kwenda kwani kufanya hivyo ni kuwasaliti Watanzania.

“Hadi sasa ninapozungumza na wewe, Ofisi ya Katibu Mkuu haijapokea mwaliko wala barua yoyote inayohusu mwaliko huo.

“Lakini la pili, hata kama ningepata mwaliko huo nisingekwenda kwa sababu kuhudhuria hafla hiyo ni kuhalalisha uovu na usaliti waliofanyiwa Watanzania ambao mawazo yao yameuliwa katika rasimu hiyo.

“Kwanza Katiba hiyo ni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa hiyo wakabidhiane wenyewe,” alisema.

KAULI YA CUF

Chama cha Wananchi (CUF), kimesema hakijapata mwaliko huo ambapo kimeungana na Chadema kukataa kuhudhuria hata kama wakialikwa.

Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Abdul Kambaya, alisema kuhudhuria sherehe hizo ni sawa na kusaliti msimamo wao na wenzao wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba na wananchi ambao maoni yao yamechakachuliwa.

“Sisi hatumo, si tulishatoka tangu bungeni, hatuwezi kwenda kwa sababu na sisi tutakuwa ni sehemu ya watekelezaji wa usaliti waliofanyiwa Watanzania,” alisema Kambaya.

Katiba hiyo inayopendekezwa ilipitishwa bungeni Oktoba 2, mwaka huu na Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa tofauti ya kura mbili baada ya kuwasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge hilo, Andrew Chenge.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Nataka nione ni Masskofu gani hawa wa TEC na CCT, Pentekoste na SDA wataokwenda kuhudhuria sherehe ya kukabidhi katiba haramu iliyowasaliti watanzania. kama watahudhuria nitasema kumbe wakristo nao ni wanafiki, viongozi hao wa dini watakuwa wanaunga mkono usaliti wa CCM kwa wananchi. Miminasubiri sana kuona hilo. lakini tujue kwamba ” kusherekea uovu ni dhambi kubwa ana, Mungu anaona sana hilo, na katiba kwa utabiri wangu haitafika mbali, hadi sasa imeshakataliwa hata na Mungu. Matumizi makubwa ya nguvu, mbavu, vitisho, polisi na FFu ni alama kwamba jambo hili halikubaliki na jamii. Hata CCM na serikali yao wanajua, lakini wafanye nini? Kwa hivi ni juu ya sisi Wananchi kuikataa kwa njia yeyote ile, na itakua hivyo. Ni heri kupotexa mabilioni kuliko kuikubali katiba chafu kwa kisingizio cha matumizi makubwa ya pesa. Pesa hainunui haki, uhuru, umoja, utu na upendo wa Watanzania. Sherehe hiyo ni feki, na itaendelea kuwa feki hata kwenye upigaji kura, unajua ukianza na uwongo lazima uushikilie hadi mwishowe utakapoumbuliwa. Shetani lazima ashindwe. Waliomwua Yesu na ukweli walifikiri wameshinda, kumbe wakawa wameshindwa hadi leo, Yesu na Ukweli ni Mshindi. na ndivyo itakavyokuwa haa hii katiba haramau’ wanafikiri wameshinda, lakini kiukweli bunge la katiba ya CCm limepigwa mueleka mkubwa sana, ni bahati mbaya hakuna anayeweza kuliona hili katika ya viongozi wakuu wa CCM, ndiyo upofu na kiburi walichopewana Mungu na ugumu wa moyo’ ili Mungu awakomboe watanzania. Kutegemea nguvu za Polisi, FFU, wanajeshi na uslama wa taifa, kuipitisha na kuilinda katiba nihatario kubwa sana, hata hao viongozi wa dini watakaohudhuria sherehe hiyo lazima wajiulize wapo upande wa shetani au wa Yesu? Mungu wabariki watanganyika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles