NA BAKARI KIMWANGA, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI mpya wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, amewataka Watanzania wamwamini katika kazi na watarajie makubwa.
Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu muda mfupi baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na mtangulizi wake, Jaji Dk. Elizer Feleshi.
Alisema pamoja na kuteuliwa kuongoza ofisi hiyo, lakini hakuna aliyezaliwa na kujua kila kitu kwa siku moja huku akitaka Watanzania kuvuta subira.
MTANZANIA ilipotaka kujua mikakati na matarajio yake katika ofisi hiyo, alijibu kwa kifupi: “Huwezi kuwa na mtoto wako aliyezaliwa leo ukamuuliza uhusiano wa baba na mama, hapana kwanza tusubiri tusiwe na haraka.
“Ni mapema kusema nitafanya nini, kwanza acha tufanye kazi kwani hata wewe unapotoka nyumbani kwako kwenda kazini huwa una mipango, nami ninapenda kukwambia vuta subira,” alisema DPP Mganga.
Uteuzi wa DPP Mganga umekuja huku akiwa Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Urejeshaji Mali zilizopatikana kwa njia zisizo halali.
Akiwa katika ofisi hiyo, DPP Mganga, alianza kujitokeza mwaka 2008 kwa kuendesha kesi za EPA pamoja na ya Samaki wa Magufuli ambazo aliweza kuzisimamia kwa uadilifu na Serikali kuweza kushinda.
Mbali na kushika nafasi hiyo, akiwa katika Ofisi ya DPP, alianza kazi kama Principle kabla ya kuwa Mkurugenzi Msaidizi.
DPP Mganga anatajwa kuwa mmoja wa wanasheria vijana ambao wamekuwa hawayumbishwi kwa nguvu ya fedha na muda wote amekuwa akisimamia maadili ya kazi yake.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Peter Ilomo jana, ilieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete, amemteua Biswalo Mganga kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) uteuzi ambao ulianza Ijumaa iliyopita.
Kabla ya uteuzi huo, Mganga alikuwa Mkurugenzi Msaidizi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Wakili wa Serikali Mfawidhi.
Awali nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Dk. Feleshi, ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa jaji wa Mahakama Kuu.
Uteuzi wa Dk. Feleshi kushika wadhifa huo mpya ulianza rasmi Agosti 13 mwaka huu na aliapishwa Agosti 15 mwaka huu.
watanzania tuangalie hii katiba iliyopendekezwa na bunge maalumu la katiba itatusaidia vipi kutatua changamoto za maendeleo zinazotukabili ili tupate kusonga mbele kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia badala ya kusikia wanasiasa wanataka nini ili watutawale.kumbukeni kuwa lengo la chama chochote cha siasa ni kushika dola na si vinginevyo.