*Asema Magufuli anaendesha nchi kama mali yake binafsi
*Amtuhumu kulirudisha Bunge miaka ya chama kushika hatamu
* Awatuhumu Dk. Mwakyembe, AG kuwa ni majipu
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE WA Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amewalipua bungeni Waziri wa Katiba na Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju kuwa ni majipu yanayohitaji kutumbuliwa kwa kile alichodai wameshindwa kumshauri vizuri Rais Dk. John Magufuli kuhusu masuala ya sheria.
Amesema hatua ya Rais Magufuli kushindwa kufuata sheria hasa katika masuala ya kiungozi, ikiwamo kuunda Baraza la Mawaziri bila kuwa na ‘instrument’, imetokana na wasaidizi wake hao kushindwa kazi ya kumshauri kwa mujibu wa sheria za nchi.
Kauli hiyo aliitoa jana bungeni mjini hapa, alipokuwa akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu Wizara ya Katiba na Sheria.
Alisema kwa muda sasa nchi imekuwa ikiongozwa na matamko, huku mawaziri wakifanya kazi bila kuwa na mwongozo jambo ambalo linakwenda kinyume na sheria.
Lissu ambaye ni msemaji wa kambi ya upinzani kwa wizara hiyo, alisema Rais Magufuli anatakiwa kufuata sheria za nchi na hayuko juu ya sheria.
“Kiapo chake kinamtaka kuilinda, kuitetea na kuihifadhi Katiba ya nchi yetu na sheria zake. “Mamlaka ya nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika, kama inavyotamka ibara ya 9(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 ili kuhakikisha kwamba sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa.
“Kwa sababu Rais Magufuli si mwanasheria, ameteua Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye kwa maneno ya ibara ya 59(3) ya Katiba, ndiye mshauri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo ya sheria, na atawajibika kutoa ushauri kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo yote ya kisheria.
“Aidha, kwa sababu hiyo hiyo, Rais Magufuli ameteua Waziri wa Katiba na Sheria ili kama inavyotakiwa na ibara ya 54(3), awe mshauri wake mkuu katika utekelezaji wa madaraka yake katika masuala ya kikatiba na kisheria.
“Kwa bahati nzuri, Rais Magufuli amemteua pia Dk. Harrison George Mwakyembe, mmoja wa wasomi wa juu kabisa wa sheria katika nchi yetu, kuwa Waziri wake wa Katiba na Sheria. Vile vile, amemteua Dk. Sifuni Ernest Mchome – msomi mwingine wa juu kabisa wa sheria, kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria; na Amon Mpanju, mwanasheria mwingine tena, kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hii, lakini wameshindwa kuonyesha uwezo wa kumshauri,” alisema Lissu.
Alisema kwa kuangalia mifano ya matangazo mbalimbali ambayo yametolewa na watangulizi wa Rais Magufuli tangu sheria ya utekelezaji wa majukumu ya kiuwaziri ilipotungwa mwaka 1980, hata mwanafunzi wa sheria wa mwaka wa kwanza angeweza kumtengenezea Rais Magufuli ‘draft’ ya tangazo la aina hiyo.
“Iweje watu wenye shahada za uzamivu na uzamili katika sheria washindwe kufanya hivyo kwa karibu nusu mwaka tangu wateuliwe? Kama ni majipu ya kutumbuliwa na Rais Magufuli, basi wasomi hawa wa sheria ni majipu na wanastahili kutumbuliwa. Itatushangaza sana endapo Rais Magufuli atayafumbia macho majipu haya,” alisema Lissu.
Alisema Kambi Rasmi ya Upinzani inaliomba Bunge ili kupatiwa majibu sahihi ni kwanini wanasheria wabobezi wote wameshindwa kumshauri Rais Magufuli kutoa tangazo la kukasimisha majukumu ya kiuwaziri kwa mawaziri mbalimbali aliowateua karibu miezi sita iliyopita.
Lissu alisema hivi sasa Serikali inaendeshwa kama mali binafsi ya Rais Magufuli, bila kufuata wala kuheshimu sheria, sio tu kwa sababu Rais Magufuli ana viashiria vyote vya utawala wa kiimla, bali pia kwa sababu anaelekea kutokuwa na washauri katika masuala ya Katiba na sheria za nchi.
Alisema kwa maana hiyo, athari ya kisheria ya kutokuwepo kwa tangazo la ukasimishaji wa majukumu ya kiuwaziri ni kubwa mno. Wengi wa mawaziri wa Serikali hii waliteuliwa na Rais Magufuli Desemba 10, 2015.
KUTOFUATA SHERIA
Lissu alisema kwa mujibu wa matangazo kadhaa, marais waliomtangulia Dk. Magufuli, katika vipindi tofauti tofauti, wamekuwa wakitumia mamlaka yao chini ya kifungu cha 5(1) cha sheria, kufanya marekebisho katika majukumu ya kiuwaziri ambayo yalikuwa chini ya rais mwenyewe, au aliyakasimisha kwa mawaziri.
“Hivyo, kwa mfano mwaka 1982, Mwalimu Julius Nyerere alitoa Tangazo la Serikali Na. 133 la 1982 kwa ajili hiyo,” alisema.
Lissu alisema rais hatakiwi kugawa wizara, idara za Serikali na majukumu ya kiuwaziri kiholela kwani hayo ni majukumu ya umma ambayo ni lazima yafanywe kwa kufuata taratibu za kisheria zilizopo.
Alisema kwa upande wao, mawaziri wanatakiwa kutekeleza majukumu waliyokasimiwa na rais kwa mujibu wa sheria ya utekelezaji wa majukumu ya kiuwaziri.
UCHAGUZI WA Z’BAR
Lissu alisema kwa watu wasiofahamu Katiba, wanaweza kuhoji kwanini kambi hiyo inazungumzia masuala ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar katika hoja iliyoko mezani.
Alisema sura ya nne yote ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inahusu ‘Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (na Rais wa Zanzibar), Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.’
Lissu alisema ibara ya 104 ya Katiba imewekwa mahsusi kwa ajili ya ‘Uchaguzi wa Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.’
Alisema kwa sababu hizi, ni halali kuzungumzia yaliyotokea Zanzibar katika hoja iliyoko mezani.
“Kilele cha matumizi haya ya mabavu ya kijeshi ni Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, ambapo vibaraka wa Tanganyika katika Zanzibar walikataliwa kabisa na wananchi katika Uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani. Ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tu ndilo ambalo limehakikisha vibaraka hawa waliokataliwa na wananchi wao, wanaendelea kubakia madarakani.
“Kwa maoni yetu mheshimiwa Spika, katika mazingira haya, tatizo la msingi la Zanzibar siyo Jecha Salim Jecha wala ZEC wala Ali Mohamed Shein. Hawa ni vibaraka tu wasiokuwa na nguvu wala uhalali wowote. Bila nguvu ya Tanganyika vibaraka hawa hawawezi kudumu madarakani kwa muda mrefu.
“Tatizo la msingi ni ukoloni wa Tanganyika kwa Zanzibar ambao umevikwa joho la Muungano. Bila kulivua joho hili na kushona lingine badala yake, Zanzibar haitakuwa huru na itaendelea kutawaliwa na Tanganyika kisiasa, kiuchumi na kijeshi,” alisema.
KUNYAMAZISHWA UPINZANI
Lissu alisema hatua ya kunyamazisha upinzani, ni sawa na kubaka demokrasia kwa kutumia nguvu za kijeshi Zanzibar ili kukipokonya Chama cha Wananchi (CUF) ushindi wake halali.
“Serikali hii ya ‘hapa kazi tu’ imeingia katika njia ya kuongezeka kwa vitendo vya kikandamizaji kila mahali katika nchi yetu,” alisema.
Alisema katika Jiji la Tanga ambako CCM ilikataliwa na wananchi, Serikali ilitumia ghilba na mabavu ya kila aina kuhakikisha CCM inanyakua kiti cha Meya wa Jiji hilo.
“Kwa vile Serikali hii ya Rais Magufuli imekumbatia dhana ya kunyamazisha upinzani dhidi yake, uhuru wa vyombo vya habari umewekwa rehani.
“Kwa kuwa Bunge hili lilijitokeza miaka 10 ya utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kama chombo chenye nguvu ya kuiwajibisha Serikali na watendaji wake, Serikali ya hapa kazi tu, imeamua kulinyamazisha na kulifanya kama lilivyokuwa wakati wa miaka ya ‘chama kushika hatamu’,” alisema.
MWAKYEMBE NA BAJETI
Awali akiwasilisha bajeti ya wizara yake, Waziri Mwakyembe alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 wizara yake itataka maelezo ya kisheria yawepo ya muda mahsusi, ikiwemo kutomalizika kwa kesi zisizomalizika kwa kisingizio cha upelelezi.
“Upotevu wa mafaili ya kesi pamoja na mahakama kuchukua hatua stahili za kiutendaji na kinidhamu kila upotevu wa mafaili ukitokea kwani tatizo hili hujirudia mara kwa mara na hata kusababisha mrundikano wa kesi.
“Ucheleweshaji wa nakala za hukumu na mwenendo wa mashauri, pamoja na jitihada bayana zinazofanywa na mahakama kuongeza kasi katika utoaji wa nyaraka hizo,” alisema Dk. Mwakyembe
KATIBA MPYA
Kuhusu kura ya maoni kwa ajili ya Katiba Mpya, Waziri Dk. Mwakyembe alisema hivi sasa suala hilo lipo chini ya uratibu wa Tume ya Taifa ya Uchuguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Alisema suala hilo, ni moja ya vipaumbele vya kufanyiwa kazi na Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli.