30.1 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Magereza wadaiwa ‘kuiba’ teknolojia ya madawati

Edward MaduhuPatricia Kimelemeta na Jonas Mushi, Dar es Salaam

MKURUGENZI Mkuu wa Kampuni ya Edosama Hardware Limited iliyopo Kinyerezi jijini Dar es Salaam, Edward Maduhu, amelalamikia Jeshi la Magereza akidai wamemrubuni na kumwibia teknolojia yake ya kutengeneza madawati ya gharama nafuu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Maduhu alisema teknolojia hizo zimewagharimu fedha nyingi na kumwomba Rais Dk. John Magufuli kuangalia chombo hicho cha usalama kwa makini, kwani kimemwonea na kumdhulumu  huku akiwa ni raia maskini.

“Teknolojia hizi zimetugharimu pesa nyingi, akili, nguvu na muda wa miaka mitano tukifanya tafiti kwa kutembelea viwanda zaidi ya 17 katika nchi mbalimbali kwa nia ya kujifunza teknolojia na ujuzi zaidi,” alisema Maduhu.

Akielezea namna walivyoanza mawasiliano na baadhi ya askari (majina tunayo) alisema  waliwasiliana naye na baadaye walikwenda ofisini kwake kwa ajili ya kuangalia utengenezaji wa samani hizo na baadaye walianza vikao wakimweleza namna wanavyoweza kushirikiana pamoja kutengeneza madawati 120, 000.

Alisema  baada ya kujadiliana kwa kufanya vikao zaidi ya vinne walikubaliana kuwa yeye wangempa kazi ya kutengeneza miguu ya madawati hayo kwa kutumia vyuma na wao wangemalizia kuweka bodi (mbao) huku wakikubaliana kila chuma atawauzia kwa Sh 25,000 kila kimoja.

Kwa mujibu wa maduhu teknolojia aliyonayo anaweza kutengeneza dawati kwa bei ya Sh 50,000 tofauti na wengine ambao hutengeneza hadi Sh 120,000.

“Walifika ofisini kwangu kwa ajili ya kuangalia ubunifu wangu ili tuweze kuingia ubia wa kutengeneza madawati ambapo waliniambia nitengeneze vyuma vya miguu na wao kutengeneza mbao za kukalia.

“Lakini cha kushangaza wamenikimbia na hata nikipiga simu hawapokei na madawati yangu mawili ya mfano wanayo wao, nimepata taarifa wameanza kutengeneza hayo madawati, namwomba Rais Magufuli niko tayari kumweleza kila kitu jinsi nilivyodhulumiwa.

“Nimejaribu kufuatilia mpaka sasa hawajanambia kitu chochote jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa, wamekuja kuiba teknolojia yangu,”alisema Maduhu.

Alisema lakini mpaka sasa wameanza kutengeneza madawati hayo kwa kutumia teknolojia yake jambo ambalo ni kinyume na makubaliano.

Kutokana na sintofamu hiyo, anaiomba Serikali kuingilia kati mgogoro huo kwa sababu unaonyesha wazi kuwa wana usalama hao hawakuwa nia njema ya kuingia naye ubia, bali kumwibia teknolojia yake.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mkuu wa Kiwanda cha Magereza, ACP Ismail Mlawa, alisema baada ya Serikali kuwapa tenda ya kutengeneza madawati, taasisi hiyo iliunda timu maalumu ya kutengeneza madawati hayo.

Alisema walikubaliana kuzunguka kwenye viwanda mbalimbali nchini kwa ajili ya kuangalia vifaa na sampuli ya utengenezaji wa madawati hayo ili yaweze kuwa katika ubora unaokubalika.

Alisema timu hiyo ilikwenda kwenye viwanda mbalimbali kikiwamo hicho cha Edosama kwa lengo la kuangalia upatikanaji wa vifaa na si vinginevyo.

“Tulienda kwenye viwanda zaidi ya vinne kikiwamo cha Edosama, lengo ni kuangalia namna ya upatikanaji wa material (malighafi) ya kutengeneza madawati pamoja na kufanya ‘window shoping’.

“Lakini katika viwanda vyote hivyo, hakuna hata kimoja tulichoingia nacho mkataba wa kutengeneza madawati kwa sababu hatukuwa na mamlaka ya kufanya hivyo hadi tutakapowasilisha taarifa kwa viongozi wetu,” alisema Mlawa.

Aliongeza kuwa baada ya kuona wanavyotengeneza madawati hayo, walilazimika kuwasilisha taarifa hiyo kwa viongozi wao ili waweze kujadiliana kuhusiana na suala la utengenezaji wa madawati hayo.

Alisema serikali iliwataka kutengeneza sampuli ya madawati na kuyawasilisha Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, lakini imekuwa vigumu kutengeneza sampuli ya madawati waliyochukua katika Kampuni ya Edosama.

“Tuliporudi ofisini, ilikuja ‘order’ ya kutengeneza sampuli ya madawati kama inavyoelekezwa na Wizara ya Elimu na baada ya kumwambia huyo bwana (Maduhu) kuwa hatuwezi kutengeneza sampuli zake ndio akaanza malalamiko kuwa haiwezekani na kwamba tumeshajua mambo mengi ambayo awali hatukuyajua hivyo hatuwezi kumwacha,” alisema Malawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles