CHAMA cha Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel kimeshindwa katika uchaguzi wa wabunge katika majimbo mawili kati ya matatu, matokeo ya utafiti wa baada ya uchaguzi yanaonyesha.
Matokeo hayo yanaonyesha chama hicho cha Christian Democrats (CDU) kimeshindwa katika majimbo ya Baden-Wuerttemberg na Rhineland Palatinate, lakini kimepeta Saxony-Anhalt.
Chama cha AfD kinachowapinga wahamiaji, kimeimarika kwa kiasi kikubwa katika majimbo yote matatu.
Uchaguzi huo ulitazamwa na wengi kama hukumu kwa Kansela Merkel kwa sera yake ya kuwapokea wakimbizi.
Zaidi ya wakimbizi na wahamiaji milioni moja waliingia Ujerumani mwaka 2015.
Naibu Kansela wa Ujerumani, Sigmar Gabriel alisema Jumamosi iliyopita kwamba kuimarika kwa AfD hakutabadili sera za Serikali yake kuhusu uhamiaji
“Huu ni msimamo wazi ambao tutaendelea kuutetea, wa kutetea utu na ubinadamu. Hatutabadili msimamo wetu sasa,” alisema Gabriel, ambaye ni Rais wa Chama cha Social Democratic Party of Germany (SPD) na pia Waziri wa Shirikisho wa Uchumi na Nishati katika Serikali ya mseto inayoongozwa na Merkel.