30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Kauli ya Rais Samia ni mwanzo mzuri kwa vyombo vya habari- TEF

Na Faraja Masinde, Dar es Salaam

Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) limesema kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kufunguliwa kwa vyombo vya habari ni mwanzo mzuri wa kutambua umuhimu wa tasnia hiyo.

Hayo yalibainishwa juzi jijini Dar es Salaam na Katibu wa Jukwaa hilo, Neville Meena wakati akichangia mjadala ulionadaliwa na Jukwaa hilo kwa kushirikiana na Internews Tanzania ukilenga kuangalia matokeo ya hotuba ya Rais Samia kufunguliwa kwa Vyombo vya Habari vilivyokuwa vimefungwa na kuangaliwa kwa Sheria za Vyombo vya Habari nchini.

Itakumbukwa Aprili 6, mwaka huu Rais Samia aliiagiza Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa huku akisisitiza vyombo vya habari viachwe vifanye kazi yake, aidha Aprili 22, mwaka huu wakati akilihutubia Bunge kwenye sehemu ya hotuba yake alibainisha kuwa; “Maeneo mengine ni pamoja na kuendelea kulinda misingi ya demokrasia na uhuru wa watu pamoja na vyombo vya habari,” alisema Rais Samia.

Akizungumzia hatua hiyo, Meena amesema kauli hiyo ya rais ni kiashiria mtazamo mpya wa serikali kwa vyombo vya habari katika kuhakikisha kuwa vinatekeleza majukumu yake.

“Kauli hii iliyotoewa na Rais Samia kuhusu kufunguliwa kwa vyombo vya habari ni mwanzo mzuri kwa serikali kutambua muhimili huu, hivyo huu ni mwanzo kwa taasisi mbalimbali za tasnia ya habari kuungana pamoja na kuweka mawazo sawa kwa ajili ya kuiendea serikali tukiwa na sauti moja.

“Kwani hii itakuwa rahisi kufanyiwa kazi kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia kuliko kila upande kusimama peke yake,” amesema Meena.

Upande wake Mwenyekiti wa MISA-TAN Tanzania, Salome Kitomari akichangia mjadala huo amesema kuwa ni wakati wa vyombo vya habari kuimarisha maslahi mazuri ya waandishi wa habari ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanakuwa na bima za afya ili zilewe kuwasaidia pale wanapopata changamoto.

“Hakuna asiyetambua mchango au kazi nzuri inayofanywa na vyombo vya habari, hata hivyo changamoto inakuja kwamba bado waandishi wengi maisha yao ni magumu ikiwamo kutokuwa na bima za afya.

“Kwani wengi wamekuwa wakikosa msaada wa kimatibabu pale linapokuja suala la fedha, hivyo wamiliki wa vyombo vya habari wanapaswa kuangalia maslahi ya waandishi wa habari ikiwamo kuwapatia bima za afya,” amesema Kitomari.

Akijibu hoja hiyo kwa upande wa Wamiliki wa Vyombo vya habari, Deodatus Balile ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, amesema bado kumekuwa na changamoto kutoka kwa waandishi wenyewe kutokana na kile alichosema kwamba wamekuwa siyo wabunifu.

“Nikianza na hili la rais, pamoja na kwamba kumekuwa na ahueni lakini bado, kwani licha ya maagizo ya Rais Samia Hassan kuhusu vyombo vya habari vilivyofungiwa nchini kuruhusiwa, mkanganyiko wa tafsiri juu ya maagizo hayo bado unaendelea kutamalaki.

“Pamoja na mkaanganyiko huo, bado rais hakurudi kueleza iwapo aliagiza vyombo vyote vufunguliwe, hivyo bado kuna changamoto,” amesema Balile.

Kuhusu masilahi ya Wanahabari Balile alisema: “Ni kweli kwamba hili la masilahi limekuwa na ukakasi, kwani wamiliki wanalalamika kuwa waandishi hawawajibiki ipasavyo, huku Waandishi nao wakisema kuwa mazingira ya kazi yamekuwa ni magumu, hivyo imekuwa ni kurushiana mpira.

“Lakini hiyo yote imechangiwa zaidi na vyombo vingi vya habari kutokuwa na matangazo ya kutosha hivyo kuwa kazi kujiendesha,” amesema Balile.

Aidha, baadhi ya washiriki waliochangia mjadala huo walikiri kuwa kwasasa kumeanza kuwa na mazingira mazuri ya upatikanaji wa habari ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Sasahivi imekuwa ni rahisi hata ukimtafuta msomi au mchambuzi kukupa maoni juu ya jambo lolole wamekuwa wakitoa ushirikiano ikilinganishwa na siku za nyuma ambapo ilikuwa siyo jambo rahisi,” wamesema wachangiaji hao.

Mjandala huo ulishirikisha wadau lkutoka taasisi mbalimbali ikiwamo Chama Cha wamiliki wa vyombo vya habari nchini (MOAT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na taasisi nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles