24.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 8, 2022

Ronaldo: Hii ndiyo sababu Juve kunisajili

TURIN, ITALIA

BAADA ya mshambuliaji wa Juventus, Cristiano Ronaldo, kupachika mabao matatu na kuipeleka timu hiyo kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mchezaji huyo amedai hiyo ni sababu ambayo imewafanya Juve wamsajili.

Juventus wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani juzi, walikuwa na kibarua kizito cha kuhakikisha wanaingia hatua hiyo ya robo fainali baada ya mchezo wa kwanza kukubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Atletico Madrid, hivyo Juventus walikuwa wanahitaji ushindi wa mabao 3-0 ili waweze kusonga mbele na Ronaldo akaweza kuifungia timu hiyo mabao yote.

Ronaldo alijiunga na Juventus mara baada ya kumalizika kwa msimu uliopita akitokea Real Madrid kwa uhamisho wa kitita cha pauni milioni 100.

Baada ya kuonesha kiwango hicho cha hali ya juu, Ronaldo alishindwa kuzuia hisia zake na kudai kwamba ulikuwa usiku muhimu kwake.

“Ulikuwa usiku maalumu kwangu, kama tutaendelea kufanya hivi tutakuwa na kila sababu ya kujivunia kwamba tupo kwenye mwelekeo sahihi, si kwamba tutakuwa mabingwa.

“Naweza kusema hii ni sababu ambayo iliwafanya Juventus wanisajili na nimekuwa nikijaribu kufanya kazi yangu kwa ubora.

“Ulikuwa usiku wa maajabu. Tulikutana na timu ngumu sana, lakini tuliwaonesha kuwa na sisi ni timu bora. Tunaendelea kufanya vizuri hatua kwa hatua na mwisho wa siku tutaona,” alisema Ronaldo.

Kwa matokeo hayo, Juventus imefanikiwa kutangulia hatua ya robo fainali ikiungana na Manchester City ambayo imeingia hatua hiyo baada ya kuwachana wapinzani wao Schalke 04 mabao 7-0, huku mchezo wa awali Schalke 04 wakifungwa mabao 3-2 nyumbani, hivyo kuwa jumla ya mabao 10-2 baada ya kucheza michezo yote miwili.

Droo ya hatua ya robo fainali inatarajiwa kuchezeshwa kesho baada ya michezo mingine miwili kumalizika leo kati ya Bayern Munich dhidi ya Liverpool na Barcelona dhidi ya Lyon.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,235FollowersFollow
549,000SubscribersSubscribe

Latest Articles