25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Polisi: Watakaoingia barabarani watachakaa

  • RPC Muroto asema mambo ya Bunge huhojiwa bungeni na si nje, Mnyika ahoji taarifa ya CAG kutowasilishwa

MWANDISHI WETU-DODOMA                

SIKU moja baada ya Vijana wa Chama cha ACT-Wazalendo, kutangaza maandamano yanayotarajiwa kufanyika leo mjini Dodoma kushinikiza Bunge kufuta azimio lake la kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, Jeshi la Polisi limesema wataoingia barabarani watapigwa mpaka  watachakaa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto aliwatahadharisha waliopanga kufanya maandamano hayo.

Alisema zipo taarifa zina sambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa baadhi ya vyama vya upinzani ikiwepo ACT Wazalendo wamepanga kufanya maandamano kesho (leo) kushinikiza Bunge kubadili uamuzi wake wa kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad.

Kamanda Muroto alisema wapo wengine wamepanga kusafiri kuja Dodoma kwa ajili kufanya maandamano hayo, huku akiwataka kuacha mara moja kwani wataambulia kipigo kikali.

“Niwatake wale wote waliopanga kufanya maandamano kesho  (leo) Aprili 9, 2019 kusitisha maandamano yao haramu, wasije kuingia barabarani maana watapigwa vibaya,” alisema Muroto.

Kamanda huyo wa Polisi alisema kazi za Bunge zinahojiwa ndani ya Bunge na si nje ya Bunge, hivyo amewataka wananchi wa Dodoma kuendelea na kazi zao kama kawaida kwani hakuna maandamano yoyote yatakayofanyika.

Hata hivyo alisema Jeshi la Polisi limejipanga kukabiliana na wale wote waliopanga kufanya matukio ya uhalifu katika kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu ya Pasaka.

MNYIKA NA HOJA YA CAG

Naye Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema),  jana aliomba mwongozo bungeni akihoji sababu ya orodha ya shughuli za za Bunge kutoonyesha kuwasilishwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad, akidai ni kinyume na Katiba.

Mnyika alitumia kifungu cha 143 (4) cha Katiba ya Tanzania kuomba mwongozo huo, ambapo Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama wamemtaka mbunge huyo kusoma vyema sheria na tafsiri ya sheria ili kuelewa kwa kina muda wa uwasilishwaji wa taarifa hiyo bungeni.

Ibara ya 143 (4) inasema; Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atawasilisha kwa Rais kila taarifa atakayotoa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hii.  Baada ya kupokea taarifa hiyo Rais atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha kwanza cha Bunge kitakachofanyika baada ya Rais kupokea taarifa hiyo na itabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile kilipoanza kikao hicho. 

Iwapo Rais hatachukua hatua za kuwasilisha taarifa hiyo kwa Spika wa Bunge (au Naibu wa Spika ikiwa kiti cha Spika ki wazi wakati huo au ikiwa kwa sababu yoyote Spika hawezi kutekeleza shughuli za kazi yake) ambaye atawasilisha taarifa hiyo kwenye Bunge.

 “Mapema leo (jana) asubuhi tumekabidhiwa orodha ya shughuli za leo (jana)  ambayo pamoja na mambo mengine kulikuwa na hati za kuwasilishwa mezani, lakini mwenyekiti Katiba 143 (4) inasema CAG atawasilisha kwa Rais (na kusoma ibara hiyo).”

“Naomba mwongozo wako kwa sababu taarifa iliyotolewa na CAG inaonyesha kwamba Machi 28, 2019 Rais alipokea ripoti za ukaguzi kutoka kwa CAG kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2018, na kikao cha kwanza cha Bunge kilianza Aprili 2, 2019 na taarifa (za CAG) zilizowasilishwa kwa Rais hazikuwasilishwa hadi sasa (bungeni).

“Katiba haikusema kama ni siku saba za kazi ama zisizokuwa za kazi. Kwanini orodha ya shughuli za Bunge leo (jana) hakuna ripoti ya CAG katika hati zilizowasilishwa mezani?,” alihoji Mnyika.

Baada ya Mnyika kuomba mwongozo huo, Waziri Mhagama alisimama na kuomba mwongozo, akitoa ufafanuzi kuhusu hoja ya Mnyika, “Kwa kuwa katika mijadala iliyoendelea bungeni leo, Mnyika wakati akiomba mwongozo ameonyesha kujua kuitafsiri Katiba na kunukuu vifungu vya sheria ya CAG lakini hakwenda mbali zaidi na kusoma sheria.

“Sheria nyingine ambazo zinaambatana na maagizo hayo ya kikatiba na kisheria katika kufanya tafsiri ya siku ambazo zimeandikwa katika katiba na sheria zinazohusika na uwasilishwaji wa ripoti ya CAG na hasa sheria ya tafsiri za sheria na hivyo kuonyesha wazi kuwa Serikali haitaki kuwajibika ama haijawajibika,” alisema.

Alisema Mnyika anatakiwa kusoma na kutafsiri na sheria hizo zote ili asiendelee kulipotosha Bunge na kuiacha Serikali iendelee kujipanga katika utekelezaji wa jambo hilo.

Akijibu mwongozi huo Chenge alisema. “Mnyika tunaongozwa na orodha ya shughuli za Bunge. Katiba kama ulivyoisoma lazima pia usome na sheria ya tafsiri, kwa sababu halikutokea bungeni, hakuna kitu kama hicho, hati zilizowasilishwa ni hizo. Nakusihi kasome sheria ya tafsiri inayoeleza siku na naamini Serikali haijaenda nje ya tafsiri,” alisema.

MAANDAMANO YA ACT

Akitangaza maandamano hayo mbele ya waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa vijana wa chama hicho, Karama Kaila alisema lengo la maandamano hayo ni kulitaka Bunge kufuta azimio hilo na kuendelea kufanya kazi na CAG.

“Sababu nyingine ni kulitaka Bunge kuweka kwenye shughuli za Bunge (Order Paper) upokeaji wa taarifa ya CAG ikiwa na saini ya Profesa Assad ifikapo Aprili 10 mwaka huu saa tatu asubuhi.

“Maandamano yataanzia eneo la Nyerere Square jijini Dodoma kupitia barabara ya Jamatini na kuingia barabara ya Bunge hadi Jengo la Bunge jijini Dodoma. Tumemwomba Spika wa Bunge au Naibu Spika wapokee maandamano yetu haya ya amani,”alisema Kaila.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,695FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles