21.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Mganga anaswa na maiti mbili za watoto

Gurian Adolf-Sumbawanga

JESHI la Polisi mkoani Rukwa, linamshikilia mganga wa jadi, James Kapyela (52)  na mtoto wake, Michael Kapyela (14), wakazi wa Mtaa wa Vuta Kitongoji cha Kizwite mjini Sumbawanga kwa tuhuma za kukutwa na maiti mbili za watoto  ndani ya chumba wanachotumia kutolea tiba.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Mathias Nyangi alisema tukio hilo lilitokea juzi  saa 7 mchana, baada ya mtoto mmoja aliyekuwa amefungiwa ndani pamoja na marehemu wawili kutoka na kwenda kutoa taarifa kwa wananchi.

Alisema kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, watoto hao, Nicolous Mwambage (7) na Emanuel Juma (4), walifariki dunia baada ya kufungiwa ndani ya chumba ambacho Kapyela alikuwa akitumia kutolea tiba za jadi.

Inaelezwa  wakati mganga huyo akiendelea kuwatibu watoto hao, aliwaacha ndani ya chumba hicho na watoto  waliingia ndani ya gari bovu na kujifungia, kisha kushindwa kufungua milango na vioo kitendo kilichosababisha wakose hewa.

Baada ya muda mrefu, watoto wawili walifariki dunia na mmoja ambaye alikuwa ni watatu alifanikiwa kutoka na kwenda kutoa taarifa kwa majirani wanaoishi karibu na mganga huyo.

Majirani baada ya kupata taarifa hizo, huku wakiwa na hasira kali walivamia nyumba ya mganga huyo na kuichoma moto pamoja na kuharibu mali zilizokuwamo

Wakati tukio hilo likiendelea, polisi walifika eneo la tukio na kumkamata mganga huyo wa jadi na mtoto wake na kuwaomba wananchi kutulia.

Baada ya hali kuwa shwari, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo alifika eneo la tukio ili kuhutubia wananchi waliokuwa na hasira ambapo aliliagiza polisi kufanya msako wa waganga wa jadi wanaofanya shughuli zao mkoani humo bila kufuata taratibu.

”Ninawaagiza polisi fanyeni msako ili kuwabaini watu wanaofanya shughuli za uganga wa jadi bila kusajiliwa.

“Kunasheria ambazo ni lazima zifuatwe ili mtu aweze kufanya kazi hiyo,si kuamua tu kujifanyia, hivyo wakamateni wote ambao hawajasajiliwa ili sheria ifuate mkondo wake” alisema Wangabo.

Alisema iwapo mganga wa jadi atakuwa amesajiliwa itakuwa rahisi kufahamika anapofanyia shughuli zake.

Mmoja wa majirani wa mganga huyo, Debora Maenge alisema mtuhumiwa huyo ni jirani yao na siku zote wamekuwa wakitambua ni mtu mwema, lakini wameshangazwa na unyama huo.

Hivi karibuni kulitokea mauaji mfululizo ya watoto mkoani Njombe, hali iliyosababisha Serikali iingilie kati kwa nguvu kubwa.

Mpaka sasa watuhumiwa watatu wa mauji hayo yamefikishwa mahakamani na kesi yao inaendelea kusikilizwa.

Pia mauaji hayo, yalihamia Kata ya Lamadi, Wilaya ya Busega mkoani Simiyu ambako watu kadhaa waliuawa kwa imani za kishirikina.

Tukio la kwanza lililotokea Oktoba 10, mwaka jana wakati mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Mwabasabi, Susana Shija (9)   katika Kijij cha Lamadi, alipokutwa amekufa na mwili wake kutupwa kwenye jumba chakavu, huku baadhi ya viungo vyake vikiwa vimeondolewa.

Mwili wa mwanafunzi huyo ulikutwa ukiwa hauna baadhi ya viungo vyake, zikiwemo sehemu zake za siri, mikono yake yote miwili, miguu yote miwili na kuondolewa kwa nywele zake zote za kichwani.

Katika tukio la pili, mtoto wa kike, Milembe    Maduhu (12), mwanafunzi wa darasa la saba,  naye alikutwa akiwa ameuawa ndani ya jengo linaloendelea na ujenzi maeneo ya Lamadi   Desemba 13, 2018.

Baada ya matukio hayo, wananchi walimuomba Mkuu Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka  awaruhusu wapige kura ya kuwataja wahusika wakuu wa matukio hayo kwa kuwa wanawafahamu vizuri.

Mauaji hayo kwa asilimia kubwa katika mikoa yote, yalikuwa yakihusishwa na imani za kishirikiana kutokana na maiti nyingi kukutwa hazina baadhi ya viongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,580FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles