RAMADHAN LIBENANGA-KILOMBERO
NI mzimu wa ajali. Ndivyo unavyoweza kusema, baada ya kutokea kwa ajali iliyopoteza uhai wa wafanyakazi tisa wa Wizara Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.
Ajali hiyo imetokea siku chache baada ya ajali iliyotokea Februari 22, mwaka huu na kupoteza uhai wa watu 19 wilayani Momba, mkoani Songwe, huku Rais Dk. John Magufuli akizitaka mamlaka zinazohusika na usalama wa barabarani mkoani humo kuchunguza na kisha kuchukua hatua katika ajali hiyo.
CHANZO CHA AJALI
Akieleza chanzo cha ajali jana alipokuwa akizungumza na MTANZANIA, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa gari hilo aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili STK 9444.
Alisema kutokana na mwendokasi wa dereva huyo ambaye alikuwa amebeba abiria zaidi ya 10, gari hilo lilimshinda na kutumbukia katika Mto Kikwawila, wakiwa wamebakisha kilomita saba ili waingie katika mji wa Ifakara.
DC Ihunyo alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 11 jioni, wakati watumishi hao wa Wizara ya Ardhi wanaofanya kazi katika Idara ya Urasimishaji Ardhi wilayani humo walipokuwa wakitokea katika shughuli za urasimishaji vijijini.
“Wakiwa bado kilomita saba kufika Ifakara wilayani Kilombero, dereva wa gari Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili STK 9444 akiwa kwenye mwendo mkali, gari lilimshinda na kuingia Mto Kikwawila na kusababisha vifo vya watumishi tisa kati ya kumi na tatu waliokuwa kwenye gari hilo,” alisema DC.
Alisema baada ya kutokea ajali hiyo, wananchi waliwahi kufika katika eneo la tukio na kuanza kutoa msaada, ikiwamo kuliinua gari hilo lililokuwa mtoni kwenye maji na kufanikiwa, ambapo waliweza kuokoa watu wanne wakiwa hai.
“Majeruhi katika ajali hiyo ni Faraja Gowele, Sauda Shaban, Stanslaus Budodi na dereva wa gari hilo, ambao wote wamelazwa katika Hospitali ya St. Francis kwa matibabu,” alisema DC Ihunyo.
Aliwataja watumishi waliofariki dunia kwenye ajali hiyo kuwa ni Salome Lukusi, Glory Mziray, Rudaya Mwakalebela, Maria Buyenja, Msafiri Gelard, Silvester Mwakalebela, Hassan Kayunga na Sheila Shaban.
Alisema baada ya ajali hiyo jana asubuhi Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Morogoro, ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Stephen Kebwe, ilifika katika eneo hilo na kupanga taratibu za mazishi ya watumishi hao kwa kushirikiana na familia.
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mtafungwa, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva huyo ambaye gari hilo lilimshinda.
Kutokana na hali hiyo, amewataka madereva, hasa wa serikali kuwa makini barabarani, kwani madereva wengi wa serikali wamekuwa wakikaidi sheria na kusababisha kupoteza maisha ya watumishi wengi wa umma kwa uzembe.
DK. KEBWE
Akizungumza jana baada ya kufika wilayani Kilombero, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe, alisema amesikitishwa na vifo vya watumishi hao.
Alisema serikali inatoa rambirambi kwa familia za marehemu hao na uongozi wa mkoa uko nao bega kwa bega katika kufanikisha miili ya marehemu inahifadhiwa na kuzikwa kwa mujibu wa imani zao.
“Tupo pamoja na hizo familia, mara tu baada ya kutokea kwa ajili hiyo Kamati ya Ulinzi na Usalama ilikutana kama ilivyo kawaida, kwa kweli ni tukio la kusikitisha na serikali imepoteza vijana wachapaka kazi,” alisema.
LUGOLA ATOA POLE
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu, ilieleza kwamba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ametoa pole kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na ndugu wa familia zote zilizopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.
“Natoa pole nyingi kwa Mheshimiwa Waziri Lukuvi, ndugu, jamaa na marafiki waliowapoteza wapendwa wao katika ajali hii, Mwenyezi Mungu aziweke roho za Marehemu mahali pema peponi, Amina,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, licha ya watumishi hao, pia mwingine aliyefariki ni mfanyakazi mmoja wa Chama cha Kijamii.
“Gari la Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili STK 994, walilopanda watumishi hao ambao walikuwa wanatekeleza Mradi wa Wizara hiyo, kwenye halmashauri hiyo, lilikuwa linakwenda Ifakara, lilipofika daraja la Mto Kikwawila liliingia kwenye daraja na kutumbukia Mtoni upande wa kushoto na kusababisha vifo vya watumishi tisa,” ilieza taarifa hiyo
AJALI YA SONGWE
Katika ajali iliyotokea mkoani Songwe Februari 22, mwaka huu, ilielezwa kuwa watu 17 kati ya watu hao 19 waliofariki hapo hapo walikuwa ni abiria wa basi hilo lenye namba za usajili T 269 CJC.
Inaelezwa kuwa basi hilo liligongwa kwa nyuma na lori la mizigo lililokuwa limebeba shehena ya mahindi na kusababisha vifo hivyo.
Ajali hiyo ilitokea saa 3:30 usiku katika Kijiji cha Senjele, wilayani Mbozi, mkoani hapa, ambapo abiria wote wa basi hilo walifariki dunia papo hapo, na abiria wawili waliokuwa kwenye lori walifariki muda mfupi baada ya kukimbizwa katika Hospitali teule ya Ifisi, Mbeya Vijijini.
Juma Amily, ambaye alishuhudia tukio hilo, alisema akiwa pembezoni mwa barabara hiyo ghafla alisikia kishindo na aliposogea aliona watu wakiwa wamevunjika vibaya.
Alisema muda mfupi baadaye majirani na viongozi wa serikali walifika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa ilitokana na lori lenye namba za usajili T 825 CNJ likiwa na tela lake namba T 388 CAA, lililokuwa likitoka nchini Kongo likiwa limebeba kichwa cha lori lingine kuelekea Jijini Dar es Saalam, kupata hitilafu kwenye mfumo wa breki.