24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

Tanesco yaeleza sababu kukatika umeme Dar, yaomba radhi

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limeeleza sababu za kukatika kwa umeme mara kwa mara jijini Dar es Salaam zinatokana na maboresho makubwa yanayohusisha matengenezo kinga ya mashine tatu za Kituo cha Ubungo II.

Kutokana na hali hiyo, shirika hilo limewaomba radhi wateja wake jijini humo kwa kukosa huduma ya umeme kwa siku za hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Uhusiano ya shirika hilo, maboresho hayo pia yanahusisha uwekaji wa transfoma kubwa la MVA 300 kwenye Kituo cha kupoza umeme cha Ubungo ili kukiongezea uwezo na kwenda sambamba na ukuaji wa mahitaji ya jiji la Dar es Salaam.

Imesema kabla ya matengenezo kuanza Januari mwaka huu, Kituo hiki cha kupoza umeme cha Ubungo kimekuwa kinapokea umeme kutoka katika vituo vya uzalishaji umeme vilivyopo upande wa msongo wa kilovolti 220 kupitia transfoma mbili zenye uwezo wa MVA 150 kila moja, zenye kupokea umeme wa msongo wa Kilovolti  220 na kuushusha hadi kuwa msongo wa Kilovolti 132  katika transforma namba sita na namba  saba za kituo cha Ubungo na  vituo vya uzalishaji umeme vilivyoungwa kwenye msongo wa kilovolti 132 ambavyo vimeungwa moja kwa moja kwenye mfumo mkuu wa usambazaji umeme  kwa Dar es Salaam na Zanzibar.

“Kutokana na matengenezo yanayoendelea vituo vya uzalishaji umeme vilivyoungwa kwenye msongo wa kilovoti 132 na 33 vimekuwa nguzo kubwa ya upatikanaji wa umeme. Vituo hivyo ni Ubungo II na Tegeta.

“Shirika kupitia wataalamu wake tayari limefanya jitihada kubwa za kupunguza athari za upungufu wa upatikanaji wa umeme kwa wakazi wa Dar es salaam na Zanzibar kwa kufungua laini ya msongo wa kilovoti 132 kati ya Kilimanjaro na Hale, Hili hufanyika ili kutoruhusu umeme wa kutoka Dar es Salaam na Morogoro kwenda Kilimanjaro hivyo Mkoa huu kuchukulia kwenye upande wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Arusha.

Pia kuwezesha upatikanaji wa umeme katika baadhi ya  maeneo ya Mkoa wa Dar es salaam, kwa kuunga baadhi ya njia za Usafirishaji  umeme kutoka Kituo cha Kinyerezi, Gongolamboto hadi Mbagala ili kuwezesha maeneo hayo kupata umeme bila kupitia kituo cha Ubungo  ambacho kipo katika matengenezo.

“Tatu, Kufungua njia ya umeme ya kilovolti 132 itokayo Kituo cha Kunduchi   hadi Mlandizi na kuunga maeneo hayo katika njia ya umeme ya kilovolti 132 itokayo Morogoro ili kuwezesha jiji la Dar es salaam kuwa na umeme wa uhakika.

“Tunatarajia matengenezo haya yanayokwenda kwa awamu yatakamilika Juni mwaka huu,” imesema taarifa hiyo.

Pamoja na mambo mengine, shirika hilo limesema litaendelea kutoa taarifa ya maendeleo ya kazi ya matengenezo ya kituo cha Ubungo yenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika Dar es salaam na Zanzibar kwa siku zijazo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles