24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Bashiru awaonya wenye uchu wa madaraka

MWANDISHI WETU-KAGERA

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema makada wanaohitaji nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho tawala wajipange kwa sera nzuri zitakaowauza na si kuwarubuni wala kuwahonga wananchi.

Hayo aliyasema juzi, baada ya kuwasili nyumbani kwao Kanazi mkoani Kagera wakati akizungumza na viongozi wa chama, serikali na wananchi waliojitokeza kumpokea.

Alisistiza kuhusu wagombea kufanya siasa za maendeleo na si za kuchafuana, kuwagawa watu, kujikomba, kurubuni wala kutoa hongo.

Aliwataka wanachama wa CCM kuanza kubaini wanachama wenye sifa, wenye uchu na maendeleo  na wasioweka mbele masilahi yao binafsi ili uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na Vijiji mwaka 2019  na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 uwe wa mfano kama chaguzi zilizofanyika enzi za TANU.

Alisema kiongozi atakayechaguliwa kwa kutumia njia za ulaghai hata kama atakuwa amepitishwa, akibainika ataenguliwa mara moja.

Katika hatua nyingine, Dk. Bashiru aliwataka viongozi waliopo madarakani waachwe wafanye kazi, kwani muda wa kunadi sera bado huku wale walioanza kupita kwa wananchi waache mara moja.

“Orodha yao tunayo kwa wale walioanza kupitapita nchi nzima,” alisema Dk. Bashiru

Akizungumzia wawekezaji, Dk. Bashiru, alisema Tanzania bado ni maskini na nyenzo pekee ya kujikwamua kutoka katika umasikini huo ni kupitia sekta ya kilimo, hivyo hapendezwi na hali iliyopo kwa sasa ya kuwaruhusu wawekezaji kutoka nje ya nchi kufanya shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi hapa nchini.

MBUNGE LWAKATARE

Aliwataka wanachama wa chama hicho kumuunga mkono Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare huku akiweka wazi mipango yake ya kumng’oa mwaka 2020.

Alisema sababu za kuunga mkono kuwa ni mbunge halali, muungwana na hapotoshi wananchi.

Hata hivyo, pamoja na sifa hizo alisema mbunge huyo ajiandae kung’oka mwaka 2020.

Mapokezi ya Dk Bashiru mjini hapa yalianzia uwanja wa ndege wa Bukoba ambapo yaliongozwa na waendesha pikipiki.

Alisema amekwenda nyumbani kwa ajili ya mapumziko ya mwishoni mwa mwaka yatakayokwenda sambamba na ziara hadi Januari 2, 2019 kwa kutembelea wilaya za mkoa huu.

Aliagiza kabla ya kuondoka mkoani hapa apatiwe maelezo ya sababu ya kufa kwa kilimo cha zao la chai alilodai lilikuwa mkombozi kwa wananchi ambao walifanikiwa kujiongezea kipato na kusomesha watoto.

Alisistiza  Taifa lina uwezo wa kujitegemea, huku akitaja baadhi ya chanyamoto zilizopo kama ukosefu wa ajira na kuagiza wakuu wa mikoa kutatua kero za wananchi pamoja na kuondoa uonevu kwa wafanyabiashara wadogo.

Hata hivyo, alirejea kauli yake kuwa CCM siyo chama cha matajiri, bali wakulima na wafanyakazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles