24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

WASIRA: KUIKOSOA SERIKALI SI JINAI

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA waziri katika Serikali za awamu nne za kwanza, Stephen Wasira, amesema si jinai kuikosoa Serikali bali kuitukana ndiyo kosa kisheria.

Mwanasiasa huyo mkongwe nchini aliyewahi kuwa Mbunge wa Bunda kabla ya kushindwa na Esther Bulaya (Chadema) katika uchaguzi mkuu uliopita, ni miongoni mwa wanachama wa CCM waliojitokeza kuwania urais ndani ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana akiwa nchini Marekani, Wasira ambaye  alikuwa waziri katika kipindi chote cha miaka 10 ya uongozi wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, alisema watu waikosoe Serikali kwa hoja na si kutukana.

“Ipo tofauti kati ya kutukana na kukosoa. Mimi naweza nikasema na bado nisitukane, mfano Zitto Kabwe (Mbunge wa Kigoma Mjini), huwa nasoma maandiko yake anaonekana ana hoja kabisa ambayo inahitaji kujibiwa na sijawahi kusikia akikamatwa.

“Lakini wapo wanasiasa; akisimama asipotukana hajisikii vizuri hao naona ndiyo wanaoshughulikiwa. Unaweza ukaikosoa Serikali bila kutukana, kukosoa Serikali si jinai lakini kutukana ndiyo jinai,”alisema Wasira.

Kuhusu viongozi wa vyama vya siasa wanaokamatwa na vyombo vya dola pale wanapoikosoa Serikali, alisema hata kama wakikamatwa watakwenda mahakamani na baadaye Mahakama itasema kama kuna kesi au laa.

“Akikamatwa si anakwenda mahakamani na kama hana kesi anaachiwa, hivyo pale mahakama inapotoa uamuzi kuwa hakuna kesi watapunguza ukamataji wa aina hiyo watawakamata wale wenye makosa tu,”alisema.

Katika kushughulikia suala hilo, Wasira alilitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa uangalifu na kusisitiza kuwa watu wasiokuwa na hatia wasikamatwe.

“Jeshi la Polisi liwe na uangalifu, waendelee kufanyakazi lakini wasikamate watu wasio na hatia,”alisema Wasira.

Aidha mwanasiasa huyo mkongwe ambaye ameshiriki na kuongoza kamati maalum iliyoandaa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020, alizungumzia pia uongozi wa awamu ya tano kulinganisha na awamu zilizopita, akisema haiwezekani watu wote wawe na mtazamo sawa.

“Kuna siku niliulizwa swali kama hilo kuwa nimefanya kazi karibu na viongozi wote, nikaulizwa nani kafanana na nani na mimi nikasema hakuna anayefanana na mwingine.

“Nikimaanisha kwamba kila kiongozi ana style yake ya kuongoza. JK (Jakaya Kikwete) alikuwa anapenda kushirikisha watu wote anaopingana nao, alikuwa akiwakaribisha wapinzani wake lakini pamoja na yote hayo alitukanwa, aliitwa dhaifu.

“Amekuja JPM (Rais John Magufuli) wanasema ni mkali mara dikteta, lakini aliyekuwa mpole, msikilizaji wa maoni yao ni dhaifu. JPM anayesimamia misingi anayoiamini yeye wanasema ni dikteta…Kikwete aliwapa uhuru mwingi sana,”alisema.

Akifafanua hoja hiyo, Wasira alisema Rais anayo haki ya kuongoza watu wake na pale wananchi wanapolalamika anao wajibu wa kuwasikiliza.

“Rais kama kiongozi wetu ana wajibu wa kuwasikiliza wananchi wake na pale malalamiko yanapozidi lazima awasikilize na si lazima akakubaliana na kila kinachosemwa lakini ni wajibu wake kusikiliza.

“Kwa kusikiliza wanachokisema anaweza kupata ukweli na uongo…atatofautisha pumba na mchele na katika kuwasikiliza anaweza akaujua ukweli ambao alikuwa haufahamu,”alisema Wasira.

TUKIO LA LISSU

Katika mazungumzo hayo, Wasira alizungumzia kwa masikitiko tukio la kushambuliwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ambapo alisema tukio hilo ni la kulaaniwa na wapenda amani wote.

Wasira ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, (Mahusiano na Uratibu) katika Serikali ya awamu ya nne, alisema siasa za chuki na visasi hazifai na kwamba hoja zijibiwe kwa hoja na si kutoa roho za watu.

Alisema matukio ya aina hiyo alikuwa akiyasikia nchi nyingine lakini ameshtushwa kutokea kwa nchi kama Tanzania ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikisifiwa kwa kuwa na amani.

“Tukio la Lissu ni baya sana…watu wote wapenda amani tunasikitishwa, tunalipinga na kulilaani. Tunataka siasa ziendeshwe kwa hoja na hoja zijibiwe kwa hoja…tupingane kwa hoja.

“Kutoa roho za watu na kukatisha maisha ya mtu hiyo si siasa, siasa za chuki na visasi hazipendezi, mauaji ni hatua ya juu kabisa ya visasi…haifai.

“…Mambo haya tulikuwa tunayasikia nchi zingine na tusiige mambo hayo, hatuyakubali kabisa,’alisema Wasira.

Alisema Jeshi la Polisi, lina wajibu wa kujua watu hao waliofanya kitendo hicho kibaya ili kuwaondolea wananchi hofu.

Aidha mwanasiasa huyo alisema katika mazingira kama hayo, watu wabaya wanaweza wakaingia katikati kwa lengo la kuichonganisha Serikali na wananchi.

“Polisi wana wajibu wa kujua haya yanayoendelea…watu wabaya wanaweza wakaingia katikati yetu, wakaichonganisha Serikali na wananchi.

“Watu wabaya wapo hapa duniani; yaani kama Polisi haiwachukulii hatua wahalifu watu hao wabaya wanaweza wakampiga Lissu na baadaye wakasema Serikali imefanya hivyo,”alisema Wasira.

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka huu mjini Dodoma, yupo Nairobi nchini Kenya akiendelea na matibabu zaidi.

MIILI ILIYOOPOLEWA BAHARINI

Akizungumzia kuhusu miili ya watu walioopolewa baharini, Wasira alisema Jeshi la Polisi linapaswa kufanya uchunguzi na kutoa taarifa ili kuwaondolea wananchi hofu.

“Jeshi la Polisi lina wajibu wa kulinda amani na utulivu pamoja na mali za watu, hivyo lina wajibu wa kutoa taarifa na kuwahakikishia amani Watanzania,”alisema Lissu.

KATIBA MPYA  

Akizungumzia kuhusu Katiba mpya ambapo alikuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Wasira alisema yapo mambo yanaenda kwa mahitaji ya wakati na kipaumbele cha Serikali.

“Rais Magufuli wakati analihutubia Bunge alisema amerithi kiporo cha Katiba mpya, hivyo atashughulikia kwa wakati.

“Hivyo ni suala la wakati ambao Serikali imeona itafaa, lakini huwezi kusema haina mpango nao wakati tulikaa siku 120 kuandika Katiba inayopendekezwa hivyo ghafla tu huwezi ukaibuka ukasema haihitajiki isipokuwa ni siku ya kuliendeleza.

“Tunahitaji Katiba mpya, maji, chakula, zote zinatokana na rasilimali, hivyo kupanga ni kuchagua,”alisema.

AMVAA NKAMIA

Wasira alieleza kushangazwa na hatua ya Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia kutaka kupeleka hoja binafsi bungeni ya kuongezwa miaka saba ya uchaguzi.

Wasira ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alihoji mbunge huyo alipotoa hoja ambayo haina manufaa kwa wananchi.

“Hivi ameitoa wapi, anaitaka miaka saba ya nini? Tuzungumze katiba kwa ujumla…sijui miaka saba…mimi hata simwelewi huyu Nkamia, sijui anataka ya nini na nimeshaongea naye tayari.

“Katiba huwa inaamsha hisia za watu, atueleze miaka saba ya nini na hiyo mitano amefanya nini? Watanzania waulizwe…hamuwezi kubadili katikati ya mchezo haiwezekani kabisa,”alisema.

HANA MPANGO WA KUGOMBEA

Kuhusu matarajio yake ya kisiasa baada ya kushindwa ubunge katika uchaguzi uliopita, Wasira alisema hana mpango wa kugombea na kwamba ameacha hiyo kazi, bali kwa sasa anagombea vyeo ndani ya chama chake.

“Mwaka 2020 sigombei, nimeacha hiyo kazi. Kwa sasa nagombea vyeo vya CCM nagombea mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), wakinipitisha sawa,”alisema.

Akitoa maoni yake kuhusiana na kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kwamba hivi sasa chama hicho kitawapitisha wagombea ubunge ambao ni wakaazi wa eneo husika, Wasira alisema: “Hilo ni jambo la kikatiba, kisheria.

“Kama Polepole amelisema litakuja katika vikao vya chama tutalizungumza kwa sasa nimeliona kwenye mitandao tu, hivyo kwa sasa sina maoni kuhusiana na hilo kwa sababu lazima lije kwenye vikao,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles