Waliohukumiwa kunyongwa nchini wafika 470

0
482

Na PATRICIA KIMELEMETA – dar es salaam

TAKWIMU zilizotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) zinaonesha kuwa hadi mwaka 2017, watu 472 wameshahukumiwa adhabu ya kifo, kati yao wanaume ni 452 na wanawake 20.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kupinga Adhabu ya Kifo, Kaimu Mkurugenzi wa kituo hicho, Felista Mauya, alisema katika takwimu hizo watu 228 wanasubiri utekelezaji wa adhabu hiyo, huku 244 wakiwa wamekata rufaa kuipinga katika Mahakama ya Rufaa.

Felista alisema licha ya Rais Dk. John Magufuli kutangaza kutotekeleza adhabu ya kifo katika kipindi chake cha uongozi, Serikali inapaswa kufanya marekebisho ya sheria ya adhabu hiyo na kuruhusu kuwapo kwa adhabu mbadala kulingana na ukubwa wa kosa.

Alisema hadi sasa Tanzania ipo kwenye hatua isiyo rasmi ya kupinga na kutotekeleza adhabu hiyo, lakini kituo hicho kitaendelea kuungana na wadau mbalimbali duniani kupinga adhabu ya kifo inayotolewa kwa wafungwa kwa sababu ni ya kikatili.

“Tunaiomba Serikali kuiondoa adhabu ya kifo ili isiweze kutolewa kwa wafungwa waliohukumiwa kwenye mahakama mbalimbali nchini, kwa sababu adhabu hiyo ni ya kikatili,” aliongeza.

Alibainisha kutokana na hali hiyo, Serikali inapaswa kutekeleza mpango wa kujitathmini wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) iliyoingia mwaka 2016 kwa kuridhia mkataba wa nyongeza wa haki za kiraia na kisiasa na kutangaza rasmi kuwa haitatekeleza adhabu ya kifo.

Felista alisema pia Serikali inapaswa kuwafutia adhabu hiyo wafungwa waliokaa gerezani muda mrefu.

Alisema licha ya kutolewa kwa adhabu nyingine mbalimbali, lakini Serikali inapaswa kuboresha mazingira ya magereza wanakoishi wafungwa waliohukumiwa kifo kwa kuimarisha ulinzi wa haki zao wanapokua magerezani.

Felista alisema wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda haki ya kuishi na kuelimisha umma kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba ili kufuta adhabu hiyo.

Alisema kituo chao kimekuwa kikifanya utetezi wa kuhamasisha kufutwa kwa adhabu hiyo ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono mpango wa dunia wa kufuta adhabu ya kifo ambao mpaka sasa baadhi ya nchi zimeshaanza kutekeleza ikiwamo Malawi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here