23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara nyanya, vitunguu, viazi kutumia mizani

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAKALA wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Kinondoni imetoa miezi miwili kwa wafanyabiashara wa nyanya, vitunguu na viazi mbatata kutumia vipimo vya mizani kama inavyofanyika kwenye mazao mengine badala ya kutumia sado, ndoo na makopo.

Hatua hiyo inafuatia baada ya wakala huo kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika Soko la Tandale na Manzese na kubaini baadhi ya wafanyabiashara wanatumia vipimo ambavyo haviruhusiwi kisheria.

Akizungumza juzi wakati wa ukaguzi huo, Kaimu Meneja wa WMA Mkoa wa Kinondoni, Charles Mavunde, alisema vipimo hivyo ni batili na ni kosa la jinai kuendelea kuvitumia.

“Sado, ndoo, bakuli, kopo na vikombe katika kupimia viazi, nyanya, vitunguu na mazao mengine ya shambani ni kosa kisheria. 

“Tunatoa miezi miwili kila mfanyabiashara awe anatumia mizani, soko la Magomeni tumehamasisha matumizi ya vipimo sahihi wafanyabiashara wote wanatumia mizani.

“Nanyi Soko la Tandale, Mabibo na Mwananyamala tutawafikia mmoja baada ya mwingine, pia masoko madogo madogo katika Wilaya za Ubungo na Kinondoni itumike mizani,” alisema Mavunde.

Alisema wafanyabiashara watakaokaidi watachukuliwa hatua za kisheria zikiwemo kukamatwa, kutozwa faini na kufikishwa mahakamani.

“Ni kosa kutumia vipimo batili, mizani isiyohakikiwa au kuchezewa kwa lengo la kumpunja mteja. Kwa atakayebainika kukiuka Sheria ya Vipimo Sura ya 340, atachukuliwa hatua za kisheria, akikutwa na hatia atastahili kifungo, faini au vyote kwa pamoja…tuko wakali sana katika eneo hili na wafanyabiashara wanatambua,” alisema Mavunde.

Alisema wakala huo una jukumu la kumlinda mlaji katika matumizi ya vipimo vinavyotumika kwenye biashara na huduma nyingine na kwamba katika

Mkoa wa Kinondoni kuna kata 34 zilizopo katika wilaya za Ubungo na Kinondoni na hadi kufikia Mei mwaka huu tayari wamezifikia kata 31.

Mavunde alisema pia kwa mwaka 2019/20 walikadiria kuhakiki vipimo 61,626 na hadi kufikia robo ya tatu (Machi) wamehakiki vipimo 51,393 sawa na asilimia 83.4 ya lengo.

Alisema kila mwaka huwa wanahakiki mizani kisha kugonga muhuri wa Serikali na stika ya uhakiki hivyo mlaji anapokwenda kununua bidhaa anaweza kujiridhisha kwa kuangalia alama hizo za uhakiki.

Mmoja wa wafanyabiashara wa kufungasha unga katika eneo la Manzese Darajani, Tabrani Kinoji, alisema yeye anatekeleza sera ya viwanda kwa vitendo kwani anafungasha bidhaa zake kwa kufuata taratibu, sheria na kanuni.

“Wananchi wanatakiwa wapimiwe kwa usahihi wasipate hasara, kama wafanyabiashara tufanye vitu kwa kufuata Sheria ya Vipimo kwa sababu kupata faida kwa ujanja ujanja hata Mungu hapendi,” alisema Kinoji.

Naye Katibu wa Soko la Tandale, Said Kisailo, alisema hamasa ya kufuata sheria ya vipimo ni kubwa kwani kila mwaka wamekuwa wakihakiki mizani yao kuepuka kuwapunja wateja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles