23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi wa dini waja na ‘uchumi chotara’

LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

VIONGOZI wa dini wametoa kitabu kinachoshauri kufanyika kwa mabadiliko ya mfumo wa uchumi nchini kwenda ule wa soko jamii au kwa lugha nyingine ‘mfumo chotara’ ambao wanasema utaharakisha maendeleo ya taifa bila kumwacha mtu yeyote nyuma.

Kitabu hicho kimeandikwa na wataalamu wa uchumi wa ndani chini ya Shirikisho la Viongozi wa Dini nchini linaloundwa na Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa lengo la kusaidia kupata mfumo mzuri kwa kuwa ule wa sasa haueleweki kama ni wa kibepari au ujamaa.

Akizungumza katika uzinduzi wa kitabu hicho, Mwenyekiti wa shirikisho hilo, Askofu Stephen Munga, alisema mfumo huo umetumika katika baadhi ya nchi za Scandinavia ikiwamo Denmark, Norway, Iceland na Ujerumani na kuonesha mafanikio makubwa na kupunguza umaskini.

Wataalamu waliofanya utafiti ndani na nje ya Tanzania na kisha  kuandika kitabu hicho ni pamoja na Mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi na Makamu Mkuu Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) Padri Dk. Charles Kitima.

Wengine ni Mtaalamu wa Ugavi na Usafirishaji na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Winnie Nguni, mwezeshaji wa mafunzo ya biashara katika masuala ya uhasibu, utoaji taarifa za fedha, usimamiszi wa fedha na mbinu za utafiti (SAUT), Ntui Ponsian.

Wapo pia Mhadhiri Msaidizi na mtaalamu wa masuala ya fedha na uhasibu kutoka SAUT, Chrispina Kiemi na Dk. Stefanie Brinkel ambaye ni  Ofisa miradi na mhasibu wa Shirika la Konrad-Advenauer-Stiftunge.

Akifafanua kuhusu mfumo huo, Askofu Munga  alisema umezingatia mazingira na mahitaji Tanzania.

 “Hatujauchukua kama ulivyo, tumeutengeneza kulingana na mazingira yetu kwa sababu tumeona nchi zote zilizotumia mfumo huu zimefanikiwa.

“Misingi ambayo inashikilia mfumo huu wa uchumi ni pembe nne, kwanza jamii na makundi yake mbalimbali wote lazima wawemo, hatuwezi kuwa na fikra kwamba yeyote anaachwa nje kama hivi tulivyoifikia.

“Jambo la pili ambalo ni muhimu ni Serikali au utawala mzuri ni muhimu katika kuleta maendeleo katika nchi yoyote, ya tatu ni elimu, unapotaka kuendelea ni lazima uwe umetengeneza watu wazuri ukizungumzia viwanda ni lazima utengeneze watu wazuri hata muundo huu unahitaji watu wazuri katika kuhakikisha unasimamiwa.

“Kwa hiyo elimu kwa ujumla wake ni nyenzo muhimu katika kutekeleza ‘model’ (mfumo) hii” alisema Askofu Munga.

Alisema mfumo huo pia umechanganya mfumo wa uchumi wa kijamaa na mfumo wa uchumi wa kibepari na kutengeneza mfumo chotara ambao umeleta mafanikio katika maeneo ulikotumika.

Alisema mfumo huo pia unaifanya nchi kuwa na matajiri sana lakini kutokuwa na maskini sana hali ambayo inaleta unafuu kwa watu wote.

Akiwasilisha kitabu hicho, mmoja wa waandishi wake kutoka SAUT, Ponsian alisema lengo la kuja na mfumo huo wa uchumi ni kushawishi jamii na Serikali kuwa na mtazamo mpya wa uchumi kwa ajili ya kizazi kijacho na zaidi kuondokana na umaskini.

Alisema mfumo huo ni mzuri kwa sababu ripoti mbalimbali za Umoja wa Mataifa za maendeleo ya watu zinaonesha kuwa nchi zinazofanya vizuri ni zile zinazotumia mfumo huo.

“Nasi kama Watanzania tukaona tuchangie katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, tukaja na mfumo huu. Katika mkutano wa Rais na wafanyabiasharana alisema anataka akitoka madarakani aache mabilionea 100, watapatikanaje, anasema anataka kuona sekta binafsi inachangia kukuza uchumi. Itachangiaje?

“Kwamba makusanyo ya kodi ni madogo kwa nchi kubwa kama hii sasa majibu yote hayo yanapatikana ukiwa na mfumo huu,” alisema Ponsian.

Pia alisema kuwa katika mfumo huo Serikali inapaswa kutoa huduma ambazo sekta binafsi haziwezi kutoa pamoja na kuhakikisha ulinzi wa mazingira jambo ambalo halifanyiki katika uchumi wa kibepari.

Kuhusu utekelezaji wa mfumo huo alisema ni lazima kuangalia masuala muhimu kama vile elimu aliyodai kuwa bado imekuwa na kasoro kadhaa hasa katika mitaala yake, afya ambayo licha ya kupiga hatua bado kuna changamoto za hapa na pale.

Pia alishauri kuangaliwa masuala ya bima na hifadhi ya jamii hasa kwa kuwafanya wananchi kuona suala la kuweka fedha katika mifuko hiyo si la  waajiriwa tu.

Askofu Mkuu Jimbo Katoliki Mtwara, Titus Mdoe alisema kwa muda mrefu jamii imekuwa haishirikishwi vizuri katika masuala ya uchumi badala yake Serikali ndiyo inayoamua iwapelekee nini wananchi badala ya kuwauliza wao wanataka nini.

“Jamii hailetewi maendeleo na mtu mmoja ni lazima watu wote washirikishwe, Serikali ianzie chini watu waulizwe wanataka nini, kuliko kufanya mambo kutoka juu wanaamua wapeleke shule au maji kumbe siyo kipaumbele cha wananchi.

“Pia ni lazima kuwe na matumizi mazuri ya wataalamu, hatujaweka mpango mzuri wa kuwatumia,” alisema

Askofu Mdoe pia aligusia tabia ya wataalamu kutanguliza fedha mbele akitolewa mfano  Daktari ambaye badala ya kufurahia mgonjwa wake kupona anafurahia fedha.

Zaidi Askofu huyo alisema ukuaji wa uchumi kwa asilimia saba hauakisi kwenye maisha ya watu.

“Asilimia saba ni kubwa lakini huenda inanufaisha watu wachache, huenda ufisadi umesababisha hivi” alisema Askofu Mdoe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles