26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

‘Siri ya mafanikio yetu

ELIZABETH HOMBO NA ANDREW MSECHU

WANAFUNZI walioongoza kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita, mwaka 2019, wameeleza siri ya kufanya vizuri katika masomo yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mtanzania jana, wanafunzi hao wameeleza pamoja na juhudi walizokuwa nazo shuleni, hawakuwahi kutarajia kuongoza kitaifa, kwa kuwa mchuano miongoni mwao ulikuwa mkali.

Faith Matee ambaye amekuwa mwanafunzi wa kwanza kitaifa katika masomo ya sayansi kutoka Shule ya St Marys Mazinde Juu iliyopo mkoani Tanga, alisema siri ya kufanya vizuri ni kusoma kwa bidii.

“Nilikuwa nasoma kwa bidii huku nikimtangaliza Mungu, pia nilikuwa nikishirikiana na wanafunzi wenzangu na walimu,”alisema Faith.

Kwa upande wa Moreen Lyimo, ambaye ni wa kwanza kati ya wanafunzi wote waliosoma masomo ya biashara, alisema japo alikuwa akifanya jitihada na kufanya vizuri katika matokeo ya shule, hakutarajia kuwa angeweza kuongoza kitaifa.

Alisema kwa juhudi alizokuwa akifanya, alikuwa akitekeleza wajibu wake kama mwanafunzi kwa kuwa alikuwa akisoma kwa mujibu wa maelekezo ya walimu, lakini hakutarajia miujiza.

“Inawezekana kweli nilikuwa naongoza na kuwacha wenzangu mbali, lakini hakuna mwanafunzi ambaye hakuwa anafanya juhudi katika masomo kwa nia ya kufanya vizuri. Labda tuseme tu kuwa huenda juhudi zinatofautiana,” alisema.

Naye Herman Kamugisha ambaye amekuwa wa pili kitaifa katika masomo ya Sayansi, alisema siri ya mafanikio yake ni kusoma kwa bidii kuwasikiliza walimu, kusoma vitabu vingi na usaidizi wa kutosha kutoka kwa wazazi na walimu.

Mwanafunzi huyo kutoka Shule ya Kisimiri, alisema amekuwa akipata msaada wa kutosha kutoka kwa mama yake ambaye ndiye anayemlea, akifanya shughuli zake za ujasiriamali.

Kamugisha alisema japokuwa alikuwa kifanya vizuri shuleni, hakuwahi kutarajia kuwa atakuwa miongoni mwa wanafunzi bora kitaifa katika matokeo haya ya mwisho.

“Kwa kweli sikuyatarajia matokeo haya kabisa, sikutarajia kushika nafasi za juu kitaifa, pamoja na juhudi zangu lakini hili kwangu jinaona kama muujiza,” alisema.

Alisema matarajio yake ya baadaye ni kuwa mhandisi wa ndege au mhandisi wa Teknolojia ya Mawasiliano.

Naye Beatrice Mwella kutoka Shule ya St Marys Mazinde Juu ambaye alikuwa wa nane kwenye wasichana bora 10 waliosoma sayansi, alisema alifanya vizuri kwa sababu alikuwa akijitambua katika masomo yake.

“Pia nilikuwa nikimshirikisha Mungu kila kitu, nilikuwa nasikiliza maelekezo ya walimu na juhudi zangu binafsi katika kusoma,”alisema Beatrice.

Latifa Mroso ambaye alipata daraja la kwanza pointi tano na kitaifa akawa wa tisa kati ya watahiniwa 10 bora waliofanya masomo ya lugha na alisema siri ya kufanya vizuri ni kumtanguliza Mungu.

Mroso ambaye alikuwa akisoma katika Shule ya Sekondari Ahmes iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani, alisema “kumtanguliza Mungu katika kila jambo ni muhimu sana nami nilikuwa nikifanya hivyo, lakini pia nilikuwa nasoma sana na tulikuwa tuna ushirikiano mzuri kati ya walimu na wanafunzi,”alisema Latifa.

Kwa upande wake Justin Muhangwa ambaye alipata daraja la kwanza pointi sita akitokea Shule ya Ahmes, alisema amefaulu kwa sababu alikuwa akijituma katika masomo yake.

“Pia kikubwa kwa kweli Mungu ameniinua nilianza kumshirikisha tangu nilipoanza kusoma na leo amenifikisha hapa ninamshukuru sana. Lakini pamoja na hilo nilikuwa nikisoma sana kwa bidii,”alisema.

Riziki Joseph aliyepata daraja la kwanza ponti saba akitokea Shule ya Sekondari ya Mwandet iliyopo mkoani Arusha, alisema siri ya kufanya vizuri katika matokeo yake ya kidato cha sita ni kutumia muda mwingi katika kusoma.

“Siri ya kufaulu ni juhudi zangu binafsi, za walimu na kushirikiana na wanafunzi wenzangu. Pia tulikuwa tukifanya discussion ya mara kwa mara vilevile tulikuwa tukitembelea shule mbalimbali na kushindana katika mitihani,”alisema Riziki.

Kwa upande wake Irene Anold ambaye alipata daraja la kwanza pointi saba, alisema siri ya kufanya vizuri ni ushirikiano uliopo baina ya wanafunzi na walimu.

“Tulikuwa tukielewana vizuri na wenzangu darasani kwa mfano kama fulani ana uwezo zaidi katika jambo fulani tunasaidiana na tunachukua ujuzi kwake lakini pia walimu wetu walikuwa wakitufundisha kwa upendo,”alisema Irene.

Naye Sara Mbaga ambaye alipata daraja la kwanza pointi saba akitokea Shule ya Sekondari ya Mwandet, alisema siri ya kufaulu ni kumtanguliza Mungu na kuishi vizuri na wenzake shuleni.

“Sisi tuna mwalimu mkuu mzuri sana alikuwa anashirikiana na vizuri na walimu wengine lakini pia walimu wetu walikuwa wakitufundisha kwa upendo,”alisema.

Mzazi wa Benius wa Mzumbe

Kwa upande wa Benius Eustace aliyekuwa wa nne kitaifa kati ya wanafunzi waliosoma masomo ya sayansi, baba yake alisema mwanaye kwa sasa yupo kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo mzazi huyo ambaye ni mkulima anayeishi Bukoba mkoani Kagera, akizungumzia matokeo ya mtoto wake huyo alisema  “huyu ni mtoto wangu wa pili kati ya saba.

“Familia yetu hatuna uwezo mkubwa, uwezo wetu ni mdogo sana. Ni wakulima wadogo tu ambao hatuna hata biashara, kwa hiyo hatua hii ni ukombozi kwetu, ametusaidia sana,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles