24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

VIGODORO VINASAHAULISHA WATOTO MASOMO

Na FERDNANDA  MBAMILA -DAR ES SALAAM

KADIRI miaka inavyozidi kusonga mbele, na maadili ya Mtanzania yanazidi kupungua. Heshima kwa wazazi na jamii inayotuzunguka haipo tena.

Muziki hasa unaopigwa nyakati za usiku katika matukio mbalimbali, maarufu kwa jina la vigodolo umekuwa kinara wa kupotosha jamii na kuwafunza watoto mambo yasiyofaa.

Muziki huo ambao hukesha, huwafanya kinadada na wasichana wadogo wacheze huku wakiwa wamevalia madela (wenyewe wanaita vijora), ambayo huwa ni mepesi huku yakishonwa na kuwekwa mipasuo mirefu na kuwaacha  wakiwa watupu.

Mbaya zaidi huwa wanacheza wakijifunua nguo na kuonyesha nguo za ndani bila aibu. Wakati hayo yakiendelea, watoto huwa pembeni wakishuhudia kile kinachofanywa na mama, dada zao.

Jambo hili limekuwa ni la kawaida hasa kwa wakazi wa maeneo ya Pwani. Wakiwa na sherehe bila kucheza utupu hawaoni raha.

Sasa basi, kilichonisukuma kuandika wazo hili, ni namna ambavyo maadili ya Mtanzania yanavyozidi kudidimia. Jamii haiogopi tena kucheza utupu, watoto wanajifunza mambo ambayo yanawafanya wasahau masomo. Hii si sawa.

Ni vema Serikali ikaliangalia suala hili kwa jicho pana, ikiwezekana ipiege marufuku uchezaji wa aina hii, kwani hufikia hatua wengine huvua kabisa nguo zao mbele ya watoto ambao ni Taifa la leo.

Kuna wakati, Rais Dk. John Magufuli alitoa onyo kwa wanamuziki ambao hurekodi video zao wakiwa utupu, hali inayowafanya wazazi washindwe kuangalia nyimbo hizo wakiwa na watoto wao.

Wakati mwingine ni aibu kwa mzazi kukaa sebuleni kuangalia muziki huku ukiwa na watoto wako au watu unaowaheshimu.

Ifike wakati, wazazi au walezi tujisitiri ili kuwafunza maadili mema watoto. Siku zote mtoto hujifunza kupitia kile anachokiona au kufundishwa, kama jamii haitabadilika tutajenga kizazi ambacho hakitajali masomo na badala yake kutamani yale yanayofanywa na wazazi wao, au wanayoyaona kwenye luninga.

Serikali za mtaa, au watu wanaohusika na kutoa vibali kwa watu wanaotaka kukesha na muziki (vigodoro), wajaribu pia kuzungumza na waombaji kujaribu kujiheshimu pindi wanapocheza na kufurahi.

Pia wajaribu kufukuza watoto katika maeneo kama hayo ili kuepuka kuwakuza kifikra na kimatendo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles