Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
WACHEZAJI wapya wa Yanga wa kimataifa wanatarajia kuanza kuingia leo kwa maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga imethibitisha kufanya usajili mzuri wa wachezaji wa kigeni ambao ni Lamine Moro (Ghana), Mustapha Selemani (Burundi), , Sadney Ukhob (Namibia), Issa Bigirimana (Burundi), Patrick Sibomana (Rwanda), Juma Balinya (Uganda) Faruk Shikhalo (Kenya) na Maybin Kalengo (Zambia).
Wakati wanzawa wakiwa Ally Ally (KMC), Abdulazizi Makame (Zanzibar) na Balama Mapinduzi (Allience) Ally Mtoni ‘Sonso’ (Lipuli FC.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mratibu wa klabu hiyo, Hafidhi Salehe, alisema wachezaji hao baada ya kuwasili ndio wataanza kupanga programu ya mazoezi kujiandaa na msimu mpya ikiwa pamoja na michuano ya kimataifa.
“Maybin ataingia saa saba usiku wa kuamkia leo, lakini wale wengine ambao wanatoka Burundi nao wataingia leo mchana(jana), wazawa wao wataanza muda wowote kuanzia sasa kwa sababu wenyewe hawapo mbali,” alisema.
Klabu hiyo tayari imeshatangaza kufunga usajili kwa wachezaji ambao walikuwa wakiwahitaji katika msimu ujao kutokana na mapendekezo ya kocha Mwinyi Zahera.
Yanga imepania kurudisha makali yao katika Ligi na kuchukua ubingwa ambao unaoshikiliwa na Simba mara ya pili mfululizo.