25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Uzimaji laini za simu sasa kwa mafungu

Nora damian – Dar es salaam

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema uzimaji laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole, utafanywa kwa awamu kuepuka mifumo kuelemewa.

Juzi usiku, TCRA ilianza kuzima laini ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole baada ya muda ulioongezwa kumalizika.

Awali uzimaji huo ulipangwa kufanyika Desemba 31 mwaka jana, lakini Rais Dk. John Magufuli aliongeza muda hadi Januari 20, mwaka huu, kuwezesha watu wengi zaidi kujisajili.

Akizungumza jana, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, alisema walianza kuzima laini 975,041 juzi saa 4 usiku.

“Wenye laini ambao hawajajisajili kwa alama za vidole ni kundi kubwa, tuliposema tunazima tarehe 31, kwa upendo mkubwa wa rais wetu na huruma yake akasema nawaongeza siku 20, Desemba 28 vituo vilikosa watu na kila tulipokuwa tunapokea takwimu usajili ulikuwa unakwenda chini.

“Lakini ilipofikia tarehe 17, 18, jana (Jumapili) na leo (Jumatatu) mmeshuhudia wenyewe mafuriko yalivyo.

“Hali hiyo haipendezi kabisa, hasa kwenye masuala makubwa ya kitaifa na ya msingi. Tabia hiyo inarudisha nyuma maendeleo, hasa katika masuala ambayo yanahusisha usalama wetu wenyewe,” alisema Kilaba.

WALIOANZA KUZIMIWA

Mkurugenzi huyo alisema laini zimeanza kuzimwa kwa awamu kwa kuanza na waliopata namba au vitambulisho vya taifa, lakini hawajasajili laini zao.

Alisema kundi lingine ni la wale waliosajili laini zao kwa vitambulisho vya taifa kabla mfumo wa kusajili kwa alama za vidole haujaanza.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, ambao wana namba, lakini hawajajisajili kwa alama za vidole ni 656,091 na waliojisajili mwanzoni kabla mfumo wa alama za vidole haujaanza ni 318,950.

“Wako watu ambao tayari wanazo namba za utambulisho wa taifa, wako 656,091 wako tayari kwa kuzimiwa leo (juzi).

“Kundi la pili ni wale waliosajili mwanzoni kwa kutumia vitambulisho vya taifa, lakini si kwa alama za vidole, wako 318,950.

“Hawa wote hawana sababu ya msingi ya kutozimiwa laini zao, hatutaki kumnyang’anya mtu laini yake ambayo ameizoea, ila tutaisitisha kupokea huduma ili aihuishe,” alisema Kilaba.

Alisema baada ya laini kuzimwa, simu ya mtumiaji husika itakachoweza kupokea ni ujumbe mfupi wa kumweleza hatua ya usajili wake.

“Haitaweza kufanya vitu vingi ikiwemo data, kutuma na kupokea fedha na nyingine, usajili wa laini haukuwekewa ukomo, bali uhuhishaji wa laini zilizokuwa zinatumika ukomo wake ndiyo ulipaswa kuwa juzi.

“Usajili unaendelea kama ambavyo watu watakuwa wanahama kutoka kwenye kundi moja kwenda lingine, hivyo si kwamba unakoma leo (juzi), utaendelea,” alisema Kilaba.

WANAZIMA KIDOGO KIDOGO

Mkurugenzi huyo alisema uzimaji laini ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole utafanywa taratibu kuepuka mifumo ya mawasiliano kuelemewa.

“Tunazima kidogo kidogo kwa sababu ya mambo ya kitaalamu, hauwezi ukazima laini milioni 5, 10 kwa mara moja.

“Tukienda wengi zaidi hawatapata huduma kwa wakati kama ambavyo leo (juzi) mzigo wa Nida ulivyoelemewa, sasa tukiongeza mzigo mwingine maana yake utakuwa mzito zaidi,” alisema Kilaba.

DAKIKA ZA LALA SALAMA

Alisema pia Watanzania wanatakiwa kubadilika na kuacha kupuuzia mambo ya kitaifa.

Kwa mujibu wa Kilaba, kabla ya muda wa nyongeza uliotolewa na Rais Magufuli, ofisi za Nida zilikuwa zikifurika watu, lakini siku zilivyoongezwa walianza kupungua.

Takwimu za TCRA zinaonyesha hadi kufikia Januari 15, jumla ya laini 27,287,091 zilikuwa zimesajiliwa sawa na asilimia 56 ya laini 48,717,967 zinazotumika.

Laini 21,430,876 ambazo ni sawa na asilimia 44 zilikuwa hazijasajiliwa kwa alama za vidole.

Juzi wataalamu wa uchumi waliozungumza na MTANZANIA walitahadharisha kuwa licha ya nia njema ya Serikali, lakini kuzimwa kwa laini kutasababisha athari kwa watumiaji, kampuni za simu na Serikali yenyewe kutokana na huduma za kifedha zinazotumika kupitia simu za mkononi.

Sheria ya Fedha iliyopitishwa wakati wa Bunge la Bajeti 2016/17 inaelekeza kutozwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika huduma za mitandao ya simu, benki na taasisi za fedha.

Ripoti ya takwimu za mawasiliano (Telecom Statistics) inayotolewa na TCRA kila baada ya miezi mitatu, inaonyesha miamala ya fedha iliyofanywa kuanzia Januari hadi Septemba mwaka jana ilikuwa milioni 756.3 yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 16. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kipindi cha robo ya tatu (Julai – Septemba 2019), watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi walikuwa milioni 23.6.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles