25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

UTEUZI WA PROFESA KITILA GUMZO

Na WAANDISHI WETU-DAR/DODOMA


BAADA ya Rais, Dk. John Magufuli, kumteua Profesa Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, mjadala mkali umeibuka kuhusiana na uteuzi wake.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, ilisema Profesa Mkumbo anachukua nafasi ya Mhandisi, Mbogo Futakamba ambaye amestaafu.

Tayari Profesa Mkumbo ameandika barua ya kujiuzulu nafasi yake ya Mshauri wa Chama cha ACT Wazalendo na sasa atabaki kuwa mwanachama wa kawaida.

Pia Profesa Mkumbo amemshukuru Rais Dk. Magufuli kwa kumteua na kuahidi kutumikia nafasi hiyo kwa uadilifu.

“Namshukuru Rais Dk. Magufuli kwa heshima aliyonipa katika kutumikia nchi yetu katika nafasi ya Katibu Mkuu. Mungu anisaidie,” aliandika Profesa Mkumbo katika ukurasa wake wa Twitter.

Hata hivyo wasomi, wanasiasa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamekuwa na maoni tofauti juu ya uteuzi huo huku wengine wakiupongeza na wengine wakishangazwa nao.

Baadhi ya wanazuoni wameuelezea uteuzi huo kama hatua ya Serikali kutaka kupunguza makali ya wapinzani.

DK. LWAITAMA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Josiah Kibira (JoKUCo), Dk. Azaveli Lwaitama, alisema uteuzi huo utaleta ukakasi kwa sababu ni mara ya kwanza nchini mshauri wa chama cha upinzani kuteuliwa kuwa mtendaji wa serikali iliyoko madarakani.

“Ingawa kisheria haikatazwi lakini unaleta changamoto kifikra, ni uteuzi utakaomkwaza Profesa Mkumbo kwa sababu hataweza tena kuikosoa Serikali, kutoa sera mbadala ama ushauri kama alivyokuwa akifanya, anakwenda kutekeleza matakwa ya Serikali,” alisema Dk. Lwaitama.

PROFESA MPANGALA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema watawala huwa wana mbinu nyingi za kupunguza makali ya wapinzani na kwamba uteuzi huo unaweza kuwa ni mbinu mojawapo.

“Mimi nimeshangaa sana kwa sababu najua msimamo wa Rais Dk. Magufuli haendani na upinzani, kumteua Mkumbo labda anataka kupunguza wale wanaokosoa serikali kwa sababu sasa Profesa Mkumbo hatakuwa na uhuru wa kukosoa serikali.

“Alikuwa ni mchambuzi mzuri sasa sijui ataendelea kuwa mchambuzi…lakini nampongeza ni rafiki yangu,” alisema Profesa Mpangala.

PROFESA MOSHI

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi, alisema yeye haoni tatizo katika uteuzi huo kwa sababu anaamini maendeleo ya Tanzania yanahusisha pande zote za walioko madarakani na upinzani.

“Kila mtu ana mchango wake katika taifa hili, awe upande wa pili (mpinzani), mkulima ama mfanyabiashara. Mahusiano baina ya serikali na upinzani yataimarika,” alisema Profesa Moshi.

MTATIRO

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema uteuzi wa Profesa Mkumbo lazima ujadiliwe bila hofu.

“Tunahoji kwa nini watu wanaunga mkono au kupinga uteuzi wa Mwalimu Kitila? Ni jamii mfu tu ndiyo haijadili yanayotukia kila siku.

“Mjadala juu ya Kitila utakwisha, iko mijadala mingine mingi inakuja. Kinachonishangaza ni kuwa, wapo watu wanaponda mijadala kama hii, ni ajabu kwa dunia ya sasa ilivyo, wanadamu wanajadili kila linalotukia na linapopita linajadiliwa lingine lijalo.

“Mimi nasema acheni watu wajadili watoe maoni yao, wamuite msaliti, wamuite shujaa, wamuite kila jina huo ndo uhuru wa mawazo. Mwisho wa siku Kitila mwenyewe ataamua kipi afanye,” alisema Mtatiro.

ZITTO

Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe, alisema uteuzi huo unaonyesha Rais Dk. Magufuli ameamua kuunganisha nchi kwa kufanya kazi na watu wote bila kuwabagua kwa itikadi zao za vyama.

“Tumepokea kwa mikono miwili taarifa juu ya uteuzi wa mshauri wa chama chetu kwa sababu imeonyesha kuwa Rais ameona hata Watanzania walio kwenye vyama vya upinzani wana uwezo, weledi na uzalendo wa kutumikia nchi yetu.

“Nimepokea barua yake (Profesa Mkumbo) na kumkubalia kwa masilahi mapana ya nchi yetu. Msimamo wa chama chetu ni utumishi wa kizalendo kwa Taifa utokanao na kila mwananchi, ndio msingi wa kaulimbiu yetu ya 'Taifa Kwanza, Leo na Kesho,” alisema Zitto.

Chama hicho kimemsihi Profesa Mkumbo aanze na ajenda ya Mfuko wa Maji Vijijini na kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini utakaosimamia upatikanaji wa maji kwa wananchi.

“Wizara hii ni kubwa na muhimu sana kwa nchi yetu. Maji ni tatizo moja kubwa ambalo wananchi wetu wanakumbana nalo na kama Taifa hatujaweza kulimaliza,” alisema Kabwe.

PROF. MKUMBO NI NANI

Profesa Mkumbo ni Mhadhiri wa UDSM na mwanaharakati wa masuala ya kisiasa.

Alizaliwa Juni 21 1971, katika Kijiji cha Mgela wilayani Iramba mkoani Singida.

Alisoma katika Shule ya Msingi Mgela iliyoko Wilaya ya Iramba kati ya mwaka 1981-1987 kisha akajiunga Shule ya Sekondari Mwenge mkoani Singida na kusoma kidato cha kwanza hadi cha tano mwaka 1988-1991.

Elimu ya Juu ya Sekondari aliipata Shule ya Sekondari Pugu kati ya mwaka 1992-1994 akijikita katika mchepuo wa PCB (Fizikia, Kemia na Bailojia).

Alihitimu shahada yake ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)  mwaka 1999, akisomea Sayansi.

Aliaanzia kazi UDSM kama Ofisa Utawala, aliifanya kazi hiyo kwa miaka minne (1999 – 2003) na wakati huo aliendelea kusoma Shahada ya Uzamili/umahiri (M.A) akibobea katika Saikolojia, alihitimu mwaka 2002.

Baada ya kufundisha UDSM kwa miaka michache, alipewa udahili katika Chuo Kikuu cha Southampton kilichoko Uingereza ambako alitunukiwa Shahada ya Uzamivu mwaka 2008akibobea pia katika saikolojia.

Kati ya mwaka 2009 – 2012, Profesa Mkumbo alifanya kazi kama mratibu wa kamati ndogo ya ufundi ya masuala ya Ukimwi.

Mwaka 2010 hadi 2012 alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa) na kisha akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Oktoba 2014.

Mwaka 2009 alikuwa Ofisa anayesimamia mitihani katika Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE), amekuwa Mhariri Mkuu na Mhariri Msaidizi wa machapisho mbalimbali yanayohusu elimu ya saikolojia, sanaa na sayansi.

Aliwahi kuwa Mkuu wa Idara ya Elimu ya Saikolojia na masomo ya Mtaala UDSM kuanzia mwaka 2009 –2012.

Amekua Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho kuanzia mwaka 2011 – 2014, amekuwa Mkuu wa Kitivo cha Elimu DUCE na kufanikiwa kuwa Profesa Mshiriki kuanzia Julai 2014.

Alianza siasa kama mwanachama wa CCM, baadaye alijiunga Chadema akiwa mshauri muhimu wa chama hicho.

Mwaka 2014, alifukuzwa uanachama kwa tuhuma za kuandaa waraka wa mapinduzi na kukihujumu chama hicho.

Mwaka 2014, alijiunga na Chama cha ACT-Wazalendo akiwa na wanasiasa wengine maarufu.

WENGINE WALIOTEULIWA

Mbali na uteuzi huo wa Profesa Mkumbo, Rais Dk. Magufuli pia amemteua Dk. Leornard Akwilapo kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Kufuatia uteuzi huo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maimuna Tarishi, amehamishwa na kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge).

Rais Dk. Magufuli pia amemteua Dk. Ave Semakafu kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambako anajaza nafasi iliyoachwa na Dk. Leornard Akwilapo aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

Habari hii imeandaliwa na Patricia Kimelemeta, Nora Damian, Mauli Muyenjwa na ELIZABETH HOMBO

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles