23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Utata ubunge wa Mwambe

 MWANDISHI WETU– DAR ES SALAAM

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ameacha maswali baada ya kusema barua ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika iliyoarifu Bunge kuhusu Cecil Mwambe kujivua uanachama wa chama hicho, haina maana wala mantiki.

Mwambaye ambaye alikuwa Mbunge wa Ndanda, Februari 15, alitangaza kujivua uanachama wa Chadema akiwa ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Lumumba na kupokewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole.

Hata hivyo juzi, Ndugai alisema barua ya Chadema ya kutomtambua na kutaka Bunge lisimpe stahiki kama mbunge, haina mantiki suala ambalo limeacha maswali huku Mwambe mwenyewe akisema bado anasubiri maelekezo ya Spka ili ayafanyie kazi.

Kwa pande wake, Mnyika amesema ni vyema kwanza Spika aseme Mwambe atarejea bungeni kama mbunge wa chama gani ilihali mwenyewe ametangaza kujiengua Chadema.

KAULI YA NDUGAI

Akizungumza bungeni juzi, Spika Ndugai alisema; “nimepokea barua ya Bwana John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema akimwandikia katibu wa Bunge. Kwenye barua hii anasema kwamba tusimtambue mheshimiwa Cecil Mwambe kama mbunge na asipate stahiki zozote.

“Lakini barua yenyewe jinsi alivyoiandika ni fupi, niwasomee tu. Anasema; “Bwana Cecil Mwambe alikuwa mbunge wa jimbo la Ndanda aliyekuwa amedhaminiwa na Chadema hata hivyo Februari mwaka huu alitangaza kupitia vyombo vya habari kwamba amehama chama hicho.

“Hivyo basi kwa mujibu ibara ya 7 (1 F ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekoma kuwa mbunge na ameacha kiti chake katika Bunge, kwa hiyo Bunge lisiendelee kumpatia sitahiki zozote.” 

Ndugai alisema; “sasa namshangaa Mnyika kwa sababu hayo maneno anayosema alipaswa aambatanishe na barua ya Mwambe inayothibitisha haya anayosema, hakuambatanisha.

“Pili, mimi sina barua ya Mwambe ya kusema kwamba kaacha ubunge kwa hiyari yake mwenyewe, na kama ni chama hiki (Chadema) kimechukua hatua, sina viambatanisho vinavyoonyesha vikao halali vilivyofanya maamuzi hayo, kwahiyo hii barua haina maana, haina mantiki.

“Nichukue nafasi hii kuwaambia wabunge wote ‘including’ wabunge wa Chadema na wengine wanaotishwatishwa huko msibabaike, msiwe na wasiwasi, mnaye Spika imara atawalinda mwanzo mwisho, habari ya ukandamizaji na ubabaishaji hauna nafasi, fanyeni kazi zenu kwa kujiamini, mmeaminiwa na wananchi, fanyeni kazi zenu wala msiwe na wasiwasi.” 

 KAULI YA MWAMBE

Jana akizungumza na MTANZANIA, Mwambe alisema hakusikia moja kwa moja wakati Spika akieleza kuhusu kutoitambua barua kutoka kwa Mnyika na kwamba hata hivyo alipata taarifa baadaye.

Alisema kwa sasa anaendelea kufuatilia na kuwasiliana na Ofisi ya Spika Ndugai kupata taarifa kwa usahihi na kwamba maelekezo na uamuzi wa Spika ndio utakaompa nafasi ya kuamua nini cha kufanya kwa sasa.

Mwambe alisema kwa kuwa Spika ndiye mkuu wa mhimili wa Bunge, anaendelea kusubiri maelekezo yake kuhusu nini anachohitaji kwake.

Alipoulizwa iwapo atatakiwa kurejea bungeni kwa kuwa inaonekana Ofisi ya Spika bado inatambua ubunge wake baada ya kukataa barua hiyo ya Mnyika, atarejea bungeni kwa chama gani, alijibu kwa ufupi: “Katika hilo ninasubiri maelekezo ya Spika.”

Alisema kuhusu suala la yeye kuandika barua kwa Spika baada ya kutangaza kujivua uanachama Chadema, au kuandika barua rasmi kwa chama chake cha awali, alisema hilo ni suala binafsi sana, lakini tayari alishatekeleza wajibu wake kikatiba na mengine hawezi kuyazungumia kwa undani kwa sasa. 

“Kwa kweli katika hili ni suala binafsi sana, kwa upande wangu nilishatekeleza wajibu wangu wa kikatiba. Kwa sasa ninaendelea na shughuli zangu. Kwamba kama nitarudi bungeni nitarudi vipi, katika hilo nasubiri maelekezo ya Spika,” alisema Mwambe.

MNYIKA

Kwa upande wa Mnyika, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa hadi pale Spika Ndugai atakapoeleza kama bado anamtambua kama mbunge, anamtambua kama mbunge wa chama gani.

Alisema ni wazi kwamba barua yake inaeleza kuwa ubunge wa Mwambe unatokana na udhamini wa Chadema na kwamba tayari alishatangaza kujivua uanachama na kujiunga na chama kingine.

“Kwa hili, Spika atakapoeleza kama bado anamtambua kuwa mbunge na anamtambua kama mbunge wa chama gani, ndipo ninapoweza kuzungumza. Lakini kwa sasa siwezi kuzungumzia hilo kabla ya kupata ufafanuzi huo kwa Spika,” alisema Mnyika.

Mwambe alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya ubunge na nafasi za uongozi ndani ya Chadema Februari 15, mwaka huu kisha kuomba kujiunga CCM.

Alitangaza kufikia uamuzi huo katika ofisi ndogo za Makao Makuu ya CCM Lumumba, Dar es Salaam akidai sababu ya kufanya hivyo ni kutokana na kuwepo kwa makundi ndani ya Chadema. 

“Kuanzia leo Februari 15, 2020 ninajivua ubunge wangu na nafasi zote za uongozi ndani ya Chadema, na nimeamua kujiunga na CCM,” alisema Mwambe ambaye alipokewa na Katibu wa Itiakadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole.

 Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 2015, Mwambe akiiwakilisha Chadema alipata kiti cha ubunge katika Jimbo la Ndanda mkoani Mtwara kwa kuwa na kura 26,247, huku Mariam Kasembe wa CCM akikikosa kiti hicho kwa kupata kura 26,215.

Akiwa Mtwara Oktoba 7, mwaka jana Mwambe alitangaza kuwania uenyekiti wa Chadema Taifa na kisha baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo wa ndani wa chama Desemba 19, mwaka huo alipata kura 59 sawa na asilimia 6.2, huku mshindani wake, Freeman Mbowe akipata kura 886, sawa na asilimia 93.5.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles