30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 19, 2021

Mishahara, mafao wabunge Chadema shakani

 RAMADHANI HASSAN– DODOMA

SIKU moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwataka wabunge wa Chadema waliojiweka karantini ya wiki mbili warudi bungeni ama warejeshe fedha walizochukua, kiongozi huyo amewaongezea mtihani mwingine akisema huenda wakapoteza mshahara wa Mei na mafao mengine.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangazia wabunge wa Chadema kutoingia bungeni wala kusogea katika mazingira ya Bunge Dar es Salaam na Dodoma.

Badala yake aliwataka wote wakae ndani kwa wiki mbili mjini Dodoma ili kujiangalia na virusi vya corona huku akiwataka pia wasiende majimboni mwao.

Juzi Ndugai alisema tangazo la Mbowe ni batili na kuwataka wabunge hao kurudi bungeni ama kurejesha fedha za wiki mbili, zaidi ya Sh milioni 110 ambazo walikuwa wamelipwa kama posho ya kujikimu.

Pia alisema wakikaidi agizo lake hilo, wiki mbili walizojipa zikiisha watalazimika kwanza kupimwa corona kisha ndiyo waingie bungeni wakishalipa fedha walizochukua.

Akizungumza kabla ya kuhitimisha Bunge jana, Ndugai alisema wabunge kuna mambo matano wanatakiwa kuyazingatia badala ya kudhani chama pekee ndicho chenye hatma ya ubunge wao. 

“Wabunge wengi ni wa mara ya kwanza, hasa wa upinzani, hivyo viongozi wao wamekuwa wakiwateka nyara kwa u-mara wa kwanza wao, wamewajaza imani ya kufikiri kwamba chama chao peke yake ndicho chenye ‘Alfa na Omega’ katika kazi zao za ubunge kitu ambacho si kweli kiasi hicho.

“Mbunge anapofanya shughuli zozote zile za kibunge, ana mambo kama matano ya ‘ku-balance’ (kuweka kwenye uwiano), kwanza lazima aangalie taratibu za kibunge, kwa maana ya sheria na kanuni, lakini pili lazima aangalie je jambo linaloendelea ambalo inatakiwa yeye afanyie kazi lina masilahi gani kitaifa.

“’Balance’ ya tatu lazina aangalie jimbo lake, wananchi waliomtuma. Je, hili lina masilahi kwa wananchi wangu? Suala la nne ni chama kilichomtuma. Je, katika jambo hili kina mtizamo gani? Suala la tano ni mbunge mwenyewe, wewe mwenyewe, hiyo barua ya Mbowe wewe unaona ina mantiki?

“Na wananchi wa jimbo langu wanakubali wewe ukae ndani usifanye shughuli za Bunge? Je, hilo jambo lina masilahi kitaifa? Je, hilo jambo limetokana na vikao vya chama chako au ni amri ya mtu tu? Maana mtu si chama, sasa wabunge ni watu wazima, lakini kwa sababu ni mara ya kwanza wanajazwa vichwani mwao kwamba bwana Mbowe akitaka unakuwa mbunge au auwi mbunge.

“Katika hayo ‘usipoya-balance’ vizuri, wewe ukabeba moja tu itakula kwako, wamekuwa (Chadema) wakitaka nchi iwekwe kwenye ‘lockdown’, sasa wananchi wengi kule Kongwa na kwingineko hawaelewi ‘lockdown’ ndo nini, labda ni jambo jema hilo kwanini wanakataa hawa? 

“’Lockdown’ maana yake wananchi wote muwekwe rumande ya hiyari, kila mtu akae kwakwe, atakayekuwa Morogoro ubanishwe hapohapo, Tabora ubanishwe hapohapo, hakuna kutoka, kuzunguka, kufanya biashara wala kwenda mashambani, inabidi mkae ndani, sasa kukaa rumande nani anataka? 

“Na pia hata hizo rumande mabunge ya nchi nyingi ndiyo yameishauri Serikali, kama Bunge kama taasisi, sisi hatujashauri Serikali jambo hilo na hatudhani kama wananchi wetu wanataka jambo hilo, kama wanataka wasema tuishauri Serikali ishauri ‘lockdown’ hata ya siku saba Watanzania hawa waelewe, hiyo rumande ni hatari kubwa. Kwa hiyo tunadhani mwongozo wa Serikali ni suala la maana,” alisema Ndugai.

Alisema kwa saa 24 mbunge anakuwa bungeni kwa saa nne tu (saa nane hadi saa 12 jioni) za kikao, na kuhoji saa nyingine 20 wabunge watakuwa wapi.

“Sasa nilielezea jana (juzi) kuhusu kuchukua fedha, maana wamelipwa tangu Mei 1 – hadi 17, alafu wakaamua kuwa watoro na kutokufanya kazi, naendelea kusisitiza ambao hawatarudisha fedha hizo tutawachukulia hatua manake tutahesabu ni wizi wa kuaminiwa.

“Ulipewa fedha kwamba umeaminiwa zitakusaidia kufanya kazi, wewe unaamua kutoroka, nilisema jana ni utoro na warudishe, wakirudisha hatuna maneno, habari ya kusema tutakata baadaye haipo hiyo. 

“Wanaobanisha wakiamini hawatarudisha haiwezekani, lazima zirudi hizi fedha na bado natafakari kwa mtu ambaye amekuwa mtoro kwa wiki mbili kazini kwake, kule serikalini siku tano unafukuzwa kazi, bado sifikiri kwenda huko, lakini kwa kawaida ya mtu ambaye hajaenda kazini wiki mbili hivi huwa analipwa mshahara?

“Kwa hiyo wajue mshahara wa Mei wakiendelea kufuata hilo (kutoingia bungeni), nimesema ‘una-balance’ mambo matano, wewe ukibeba moja katika mzani ukaacha manne, sasa huu mshahara wa mwezi wa tano labda wanieleze ni kwanini walipwe mshahara wa mwezi wa tano.

“Na nikiongea hata wabunge hawa wananielewa, mwezi huu una mazingira haya, hayaruhusu mtu kuwaingiza kwenye mchezo wa namna hii, ‘opportunity lost’ ni kubwa sana, lakini kazi kwenu.

“Pia natoa tangazo tumeshapokea kutoka taasisi mbalimbali za fedha nchini taarifa za bakaa ya mikopo ya wabunge wote, mikopo mbalimbali ambayo itatumika katika kukokotoa na kulipa mafao ya kazi ya ubunge. 

“Kesho nitaelekeza watu wangu wa uhasibu watoe barua kwa wabunge waliopo kwa kumkabidhi kwa ‘dispatch’ siyo kwa e-mail wala kupeleka kwenye ‘tablet’ kwa sababu hii hatutaki liwe tangazo, atapewa mbunge mmoja mmoja kwa waliopo, hawa wasiokuwepo waendelee kukaa hukohuko wakose hizi ‘information’.

“Na mwisho wa mwezi huu kuna shughuli inaendelea ambayo wao wanaifahamu vizuri kuliko mwananchi mwingine, watashangaa kwa yatakayoendelea, nawahasa wabunge hawa warudi, wapo kwenye mtihani mkubwa kwelikweli wa kuendelea kumtii huyo jamaa yao ama warudi tuendelee kwa taratibu zinazotakiwa,” alisema Ndugai.

Hata hivyo, agizo la Mbowe la kutoingia bungeni halikuitikiwa na wabunge wote wa Chadema kwani baadhi wameendelea kuhudhuria vikao vya Bunge ambao Ndugai amesema hawatahusika kwenye kurejesha fedha.

Wabunge hao ni pamoja na Peter Lijualikali wa Kilombero, David Silinde (Momba), Jafary Michael (Moshi Mjini) na Wilfred Lwakatare (Bukoba mjini).

 Wengine ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini na Antony Komu (Moshi vijijini) ambao wametangaza kuhamia NCCR Mageuzi baada ya Bunge kwisha.

Wengine ni wabunge wa viti maalumu; Ratifa Chande, Sabrina Sungura, Suzan Masele na Mariam Msabaha.

POLISI YAWAVAA WABUNGE

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewataka wabunge wote wa Chadema waliopo katika Jiji la Dar es Salaam kuripoti kwa hiyari yao kwenye Ofisi za Upelelezi Kanda Maalumu kwa mahojiano zaidi.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na jeshi hilo na kutiwa saini na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ronarld Makona kwa niaba ya Kamanda wa Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa, ilieleza kuwa agizo hilo 

 linafuatia agizo la Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Paul Makonda alilolitoa juzi.

Ilieleza kuwa mkuu huyo wa mkoa aliwataka wabunge waliopo katika Mkoa wa Dar es Salaam badala ya bungeni ambako vikao vya Bunge vinaendeela warejee bungeni haraka.

ACP Makona alisema mkuu huyo wa mkoa alitoa saa 24 wawe wamerejea bungeni, muda ambao ulimalizika jana mchana.

Juzi, Makonda aliagiza kukamatwa na kuwapa mashtaka ya uzururaji wabunge wote wa Chadema ambao wapo katika mkoa wake badala ya kuwepo katika kituo chao cha kazi, bungeni Dodoma iwapo hawatohudhuria vikao vya Bunge vinavyoendelea.

Makonda alitoa muda wa saa 24 kwa wabunge wote walioko katika jiji hilo kuondoka vinginevyo atawatia mbaroni.

Kauli yake hiyo mbali ya kuzua gumzo kubwa, pia imekuwa ikijadiliwa kwa kulinganisha na kauli zake zinazofanana na hizo alizowahi kuzitoa siku za nyuma.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,848FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles