24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

‘Upepo wa kisulisuli’ ulivyozaa mjadala wa wasichana na ndoa

SWAGGAZ RIPOTA

MAPEMA wiki hii mchungaji kiongozi wa kanisa la Mlima wa Moto, Dk. Gertrude Rwakatare, ameibua mjadala mzito katika mitandao ya kijamiii baada ya kusambaa kwa video fupi inayomwonyesha akiwafanyia maombi wasichana ambao hawajaolewa.

Katika video hiyo iliyorekodia kanisani kwake Mikocheni B Assemblies Of God jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita, Mama Rwakatare aliongoza jopo la wachungaji kuwaombea wasichana hao wenye uhitaji wa kuolewa.

Miongoni mwa maneno yaliyosikika na kupata umaarufu mkubwa miongoni mwetu ni ‘upepo wa kisulisuli’ alioutaka kuwaleta wanaume kutoka pande za Mashariki, Magharibi, Kaskazini na Kusini ili kuwaoa wasichana waliojitokeza katika madhabahu ya kanisa hilo wakiwa na uhitaji wa ndoa.

Video hiyo imezalisha utani mwigi katika mitandao ya kijamii kiasi cha watu kuitumia kama mzaha na burudani huku watu wengine wakiibua mjadala wenye mitazamo tofauti kuhusu wasichana na suala zima la ndoa.

Mastaa na watu wa kawaida wametumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kutoa mitazamo mbalimbali kuhusu wasichana na ndoa wakitumia video hiyo ya mchungaji Dk. Gertrude Rwakatare kama ifuatavyo.

Zamaradi Mketema: Hii video imekuwa kama komedi kwa wengi na ‘kutrend’ lakini niamini mimi ukiangalia kwa umakini utajisikia vibaya kwa jinsi wanawake wanavyokimbizana pale mbele kupata upako wa kisulisuli kitu ambacho ni ngumu kukiona kwa wanaume.

Hiyo inaonyesha kitu kimoja tu, wanawake wengi tuna upweke. Huwa tunahisi hatujakamilika peke yetu na tunahitaji mwanaume wa kutukamilisha kitu ambacho ni nadra kukuta hisia hizo kwa mwanaume ndiyo maana tunakimbizana tukisikia kuna ndoa, mara nyingi tunahisi matatizo ni fedha tu lakini hii inaonyesha upweke ni tatizo kuliko matatizo mengi yanayoonekana makubwa.

Lakini cha kujiuliza, kutokuwa na mume kunafanya mwanamke asiwe kamili kweli? Pia jinsi gani tunaweza kuepuka dhana hii isituletee upweke huu unaotuumiza wanawake maana sijawahi kuona wachungaji au masheikh wanaombea wanaume wapate wake wa kuoa.

Nikk wa Pili: Kijamii msichana akifunga ndoa ana heshimika kuliko akipata ‘degree’, ndoa imekuwa kama kilele cha mafanikio ya msichana, huu ni ukuta unahitajika kubomolewa, ni gereza la kuyafunga maono ya msichana, ni maono ya kiwango cha chini kabisa, msichana unaweza kuwa chochote ‘dream big’ (ndoto kubwa).

Andrea Muhozya: Hakuna ndoto ya maana kwa binti zaidi ya kuwa mke bora kwa mumewe na mama bora kwa watoto lakini pamoja na kuolewa binti anaweza kujiwekea malengo mengine.

Albert Msando: Hii nchi ina matatizo mengi sana ila tatizo la fikra ni tatizo kubwa pia. Matatizo kama upepo wa kisulisuli siyo makubwa. Kuelimisha umma siyo jambo dogo, huu upepo wa kisulisuli hauchagui wa kubeba, tukumbuke tu siku hizi wanaoingia kwenye ndoa idadi yao haitofautiani sana na wanaotoka. Kuna upepo wa Kaskazi pia unaotoa waume na wake kama ambavyo wa upepo wa kisulisuli unawaleta.

Akitoa maana ya neno ‘upepo wa kisulisuli’ kama alivyomaanisha katika video ile mchungaji Dk. Gertrude Rwakatale hivi karibuni alipozungumza na mtangazaji Lilian Mwasha wa SnS, alisema: “ Napenda nimshukuru Mungu kwasababu mada hii ya upepo wa kisulisuli imeweza kugusa jamii, imegusa wanaume na wanawake ni jambo zuri kwa wakati fulani.

“Kwa mfano, upepo wa kisulisuli maana yake ni nguvu za Mungu, sasa mtu ambaye hajaelewa yeye ameshika tu upepo wa kisulisuli, kitu ambacho ni kizuri kwa mtazamo wake,” anasema Dk Rwakatale.

Aliongeza kuwa: “ Ukisoma katika kitabu cha Hesabu 11:4, Musa alipokuwa jagwani na wana wa Israel, walichoka kula mana, wakalalamika wakasema Bwana tumechoka kula mana sisi tunataka nyama, kwanini umetuleta hapa kila siku tunakula mikate.

“Mungu akasikia akamwambia Musa, waambie wana wa Israel kama kitu kinachofanya wakonde na kuwaumiza mioyo yao ni nyama basi tutaleta kware kwa upepo wa kisulisuli, fikiria jangwani kware wanatoka wapi, sasa Mungu akaleta nguvu zake kwa njia ya upepo, kwanjia ya Roho Mtakatifu kama upepo wa kisulisuli,

“Kware ni kuku wa kienyeji wa porini ni mtamu zaidi kuliko kuku wa kawaida, Mungu alitaka kuwapa kitu bora ili kuwaridhisha hamu yao, kwahiyo kware waliswaga popote walipo wakaletwa na upepo wa kisulisuli kwa wana wa Israel.”

Aidha mchungaji mama Rwakatare alisema: “Huo ulikuwa ni muujiza, mimi nilikuwa naombea wasichana waolewe, siyo wasichana tu hata wanaume lakini maana yake ni kwamba upepo wa kisulisuli ulete kitu ambacho unakihitaji kuliko vyote, mfano gari, mume, mke, cheo na mengine.”

Akizungumzia suala la ndoa, Dk. Rwakatale alisema: “ Nikiwa kama mchungaji nikiona mabinti wazuri wamekaa muda mrefu wengine wananiambia mchungaji niombee nataka mume, sitaki kutenda dhambi, sitaki kumuudhi Mungu sababu wenzangu wanakwenda kwa mafundi, rafiki zangu wanakwenda kwa waganga, hapo lazima niombe kwasababu binti ameamini Mungu.

“Mpango wa Mungu kwa mwanadamu ni kila mwanamke awe na mume wake. Mungu kabla hajaanzisha taasisi yoyote alianzisha taasisi ya ndoa na akasema ndoa iheshimiwe na watu wote. ”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles