25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Array

Uhuru Kenyatta akanyaga nyayo za Gaddafi

Na Markus Mpangala

Bara la Afrika limeibuka tena kuhoji suala muhimu na lenye tija katika mamlaka za kisiasa na utawala duniani.

Viongozi wa Afrika waliohudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York nchini Marekani, Septemba 18, mwaka huu wametoa wito wa kuongeza ushirikiano katika baraza hilo.

Rais Hage G. Geinob wa Namibia  amesema wana hofu wanapoona dunia ikiendelea kugawanyika.

Miongoni mwa marais waliozungumzia suala hilo ni Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ambaye ameonekana kulipa uzito mkubwa suala hilo kama alivyowahi kusema aliyekuwa Rais wa Libya, Muammar Gaddafi (marehemu) mwaka 2009.

Akihutubia mkutano huo Rais Kenyatta amesema miongo ya hivi karibuni, Afrika imepoteza mamilioni ya dola kwa njia haramu za kuhamishiwa nchi za nje huku akionya kuwa kinachofanywa barani humo kinapaswa kufanyiwa sehemu nyingine duniani. Hata hivyo amelaumu vikali ule alioutaja kuwa ufisadi katika mfumo wa kifedha na kisheria duniani.

Kenyatta amesema Afrika ipewe viti vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kusisitiza kuwa ni muhimu Bara la Afrika kuwa na nafasi za kudumu kwenye vyombo vikuu vya maamuzi vya UN.

Mbele ya viongozi wenzake wa Afrika na wengine kutoka nje ya Afrika, Kenyatta amesema; “Kenya inaungana na wengine kutaka Afrika ipewe viti viwili vya kudumu vyenye haki na majukumu sawa na wengine ikiwemo haki ya kura ya turufu, pamoja na viti vingine zaidi ambavyo si vya kudumu jinsi tunavyojua. Afrika haijawakilishwa vya kutosha katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hatujawakilishwa kabisa katika kiwango cha kudumu. Ukosefu huu wa haki wa kihistoria ni ishara wazi ya mfumo wenye upendeleo unaochangia upungufu wa kutoaminiana kati ya mataifa.”

Hoja ya Rais Kenyatta imenikumbusha miaka 6 iliyopita ambapo niliandika makala juu ya suala hili na kusisitiza kuwa kuna umuhimu mkubwa Bara la Afrika kuwa na kura ya turufu ndani ya baraza hilo kama chombo chenye kubeba maamuzi mengi ya UN.

Katika maelezo yangu nilisema kama ni mipango, basi hakuna uchawi wowote katika kuwania utekelezaji wa dhamira hai kwa nchi yoyote.

Na katika hilo, mwanazuoni wa masuala ya sayansi, Louis Pasteur(1822-1895), alipata kusema maneno haya; “Chance favors only the prepared mind”.

Wakati tunapokumbuka kauli hiyo tunatakiwa kufahamu namna ya kuishi kwa mipangilio inayoeleweka na kujengewa. Mipangilio hii ni pamoja na juhudi za mhusika ili kufanikisha.

Aghalabu kila mwenye juhudi juu ya jambo fulani lazima atafanikiwa. Pengine kufanikiwa huko si kule kwa kiwango cha juu lakini angalau kuna kuwa na jambo lenye kuonyesha ufanisi.

Naam, kuna juhudi kubwa kwa nchi mbalimbali kupata nafasi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Baraza hilo linao wanachama wa kudumu ambao ni pamoja na  China, Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Japan.

Afrika Kusini ni moja ya nchi iliyopigiwa kampeni ya kuwa mwanachama wa kudumu kwenye baraza hilo. Lakini si nchi hiyo pekee, bali pia Nigeria inaweza kufikia mafanikio na kuwa mwanachama wa kudumu katika Baraza hilo.

Rais wa Rwanda Paul Kagame, aliwahi kueleza kuwa ikiwa Nigeria itafanikiwa kujitosheleza masuala yake ya ndani, basi ina kila sababu ya kuwa mwanachama wa baraza la usalama na kiongozi wa nchi za kupigiwa mfano barani Afrika.

Ipo Morocco na Tanzania ambazo zinaweza kabisa kuwa mwanachama wa kudumu kwenye baraza hilo kutoka upande wa Afrika. Lakini nazo zinaweza kukabiliana na hoja ya kujitosheleza mahitaji yake ya ndani.

Sifa za nchi inayotakiwa kuingia au kuwa mwanachama wa baraza la usalama ni;

Mosi; Taifa au nchi inayoibuka kama yenye nguvu duniani pamoja na uchumi wake kutawala katika biashara duniani kwa kiasi fulani.

Pili; Taifa au nchi inatakiwa kuwa mfadhili mkubwa wa shughuli za uendeshaji wa umoja wa mataifa.

Tatu; Taifa au nchi inatakiwa kuwa na kiwango cha chini cha uvunjaji wa haki za binadamu kwa mujibu wa matakwa au kanuni za kuwa mwanachama wa baraza la usalama.

Nne; Nchi au taifa halitakiwi kuwa kwenye mgogoro ambao unaweza kusababisha vita wakati wowote.

Tano; Nchi inatakiwa kutoa mchango wake katika jeshi la kulinda amani kwa baraza la usalama.

Sita; Unachama wa nchi kwenye baraza la usalama unapitishwa au kuridhiwa na wanachama wote.

Ukiangalia nchi nyingi za Afrika, hatuna sababu ya kungojea kupewa nafasi ya uanachama wa Baraza la Usalama la UN. Tuna kila sababu ya kuchukua hoja ya Uhuru Kenyatta na kuanza ‘kutaka’ uanachama kwenye baraza la usalama na vyombo muhimu vya maamuzi pamoja na kubadili masharti ya uanachama wenyewe.

Asilimia 75 ya kazi za baraza la usalama zinafanyika barani Afrika lakini hakuna nchi yoyote ya bara hili ambayo ni mwanachama wa kudumu wa baraza hilo, na sababu inayotolewa ni nguvu ya kiuchumi na kujitosheleza kwa mataifa.

Swali kuu linalotakiwa kutazamwa hapa ni namna tunavyojipanga kujitosheleza kiuchumi ndani ya nchi zetu. Ikiwa viongozi wa Afrika watafanikiwa kujitosheleza; kwa maana kuwatosheleza wananchi wao, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni bila shaka tutakuwa na hatua muhimu kwa manufaa ya Afrika.

Kila mwenye mawazo mazuri kwa Bara la Afrika ni lazima atafakari kwa kina juu ya suala la Kura ya Turufu(Veto) kwa bara letu.

Pengine wapo wanaodhani kura ya turufu si muhimu. Lakini polepole wataelewa kuwa masilahi ya nchi yanalindwa pale fursa ya kimaamuzi ndani ya chombo cha uamuzi kinapotaka kufanya kazi dhidi ya nchi au mwanachama yoyote.

Mathalani, China na Urusi zilitumia kura ya turufu kuzuia kupelekwa Jeshi la UN nchini Zimbabwe. China na Urusi zikapiga kura za Turufu kukataa mpango wa kupeleka Majeshi ya UN nchini Sudan Kaskazini.

Nchi hizo zilitumia haki yake ndani ya baraza la usalama lililokuwa linataka kufanya maamuzi ya kuhatarisha masilahi yao.

Zote mbili zinafahamu umuhimu wa kura hiyo ndiyo maana  haikuwa na kificho kukataa mapendekezo yanayowaumiza wananchi wa kawaida barani Afrika.

Kuwa mwanachama wa baraza la usalama kunasaidia nchi kupeleka muswada wowote juu ya suala fulani. Mfano, nchi yetu inaweza kupinga mpango wowote au hatua za kijeshi dhidi ya wananchi wa nchi yeyote duniani.

Hii inasaidia uhusiano kati ya nchi yetu na nchi inayosaidiwa kupitia kura ya turufu au kambi ambayo inathamini na kulinda masilahi yetu.

Sasa inakuwa vigumu kwa nchi nyingi za Afrika kuamua kwenye eneo la usalama ikiwa itategemea azimio lolote la Baraza la Usalama UN.

Tunatambua kuwa Baraza la Usalama la UN linaundwa kwa azimio la umoja huo. Baraza hilo likiwa na lengo la kulinda amani na ulinzi duniani.

Chini ya kanuni ya Sura ya VII ya azimio hilo, Afrika inaweza kufanya vyema na kushiriki harakati za uamuzi dhidi ya masuala mbalimbali.

Barani Asia zipo Japan na China. Kule Ulaya zipo Ufaransa, Uingereza, Ujerumani na kadhalika. Lakini kwetu Afrika bado hatuna mwanachama wa kudumu mbali na uwepo wa Afrika Kusini, ambayo ilikuwa mjumbe maalumu wa baraza hilo la UN.

Enzi za uhai wake Gaddafi aliwahi kutoa hotuba mbele ya Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuhoji kwanini muundo wa uendeshaji kwenye vyombo vya maamuzi umezitenga baadhi ya nchi.

Hoja ya Gaddafi imebaki kuwa hai hadi leo na sasa Uhuru Kenyatta anaonekana kupeperusha bendera ya nchi yake na Afrika kwa ujumla kusisitiza mabadiliko ya vyombo vya uamuzi vya umoja wa mataifa ukiwemo baraza la usalama la umoja huo.

Miaka miwili kabla ya Gaddafi kuuawa alipendekeza kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kubadilishwa muundo wa uanachama wa baraza la usalama na pamoja na uendeshaji wa umoja wa mataifa.

Alisema inawezekana kabisa uanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ukatolewa kikanda. Kwa mfano, Afrika inatakiwa kuwa na mwanachama katika baraza hilo, sambamba na Asia,Ulaya, Amerika Kusini, Kaskazini na kwingineko.

Ndiyo kusema Afrika inatakiwa kukaribisha majadiliano kuhusu kura ya turufu miongoni mwa wanachama wa AU.

Vile vile inaweza kuanzia kuwa kwenye baraza hilo kati ya wanachama 15 kabla ya kuingia kwenye wanachama wa kudumu watano.

Kila mwaka wanachama wapya  huchaguliwa ili watumikie kipindi cha miaka miwili kulingana na mpangilio wa jiografia yenye uwiano kwa mujibu wa Baraza la Usalama UN.

Kwa namna yeyote Bara la Afrika linahitaji  kura ya turufu. Lakini kufanikisha jambo hilo lazima watawala wetu wathibitishe uwezo wao kwa kuzitosheleza nchi zao. Ni lazima tujenge uchumi wetu. Lazima tuhakikishe wawekezaji wa ndani wanakuwa msingi kuliko wawakezaji wa nchi ambao huhamisha faida zao.

Kwahiyo kujitosheleza mahitaji ya kiuchumi kunasaidia sana katika harakati za kuwania uanachama wa baraza la usalama ambapo baadaye huwa na uwezo wa kupiga kura ya turufu.

Faida nyingine ni kuweza kupambana kwa kila namna kwenye asasi za Baraza la Usalama UN, ambapo baadhi ya wanachama wa baraza hilo wanazitumia kama muhuri wa kutekeleza ajenda zao. Nguvu kubwa ya kiuchumi inajengwa kwenye baraza la usalama.

Pengine si nchi zote za Afrika zinaweza kupata nafasi ya kuwepo kwenye baraza la usalama, lakini ni vyema watawala wetu waelewe kujitosheleza ndani ya nchi zetu ni ngao kubwa ya kupata nafasi ya kura ya turufu.

Tunahitaji elimu, afya, huduma za jamii, miundombinu na kadhalika. Yote hayo yanakuja kutokana na mpangilio ambao nchi zetu zinajikita kwenye suala la kujitosheleza.

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles