UDSM wajipanga kufanya utafiti hamahama ya wapinzani

0
780

NA GABRIEL MUSHI, DAR ES SALAAM

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kinajipanga kufanya utafiti ili kujua sababu halisi za wimbi la wanasiasa wa vyama vya upinzani kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa madai ya kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli.

Hadi sasa jumla ya wabunge nane na madiwani takribani 140 wa upinzani wamehamia CCM.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mhadhiri wa UDSM, Profesa Alexander Makulilo, wakati akijibu hoja za baadhi ya wanafunzi wa shule mbalimbali za Dar es Salaam, waliowabana wasomi watoe sababu halisi za wimbi la baadhi ya wanasiasa wa upinzani kuhamia CCM.

Hata hivyo, alisema suala la kuhama vyama halikuanza awamu hii kwa sababu tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi lipo kwa mujibu wa Katiba lakini kutokana na wimbi hilo kuwa kubwa kwa awamu hii wanakusudia kufanya utafiti.

“Kwa sababu vyama vingi havifanyi uchaguzi, vinamtegemea mtu mmoja zaidi ya miaka 30, unaweza kukuta mtu huyu hana mawazo mapya hivyo tunajipanga kufanya utafiti tupate majibu sahihi,” alisema Profesa Makulilo.

Awali, wanafunzi hao waliozungumza mbele ya maprofesa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, walikosoa dhana ya umuhimu wa demokrasia katika ukuaji wa uchumi kwa mataifa ya Afrika.

Wanafunzi hao kutoka shule za sekondari Kisutu, Makongo na Relini walitoa kauli hizo Dar es Salaam jana wakati wakichangia mjadala katika mdahalo wa kumbukizi ya miaka 19 ya Tanzania bila Mwalimu Julius Nyerere.

Mdahalo huo uliofanyika katika Ukumbi wa Nkuruma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kupewa jina la ‘Mienendo ya uchaguzi na mustakabali wa mataifa ya Afrika’, ulihusisha wanasiasa, wasomi na watu wa kada mbalimbali.

Mmoja wa wanafunzi hao anayesoma kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Relini aliyejitambulisha kwa jina moja la Latifa, pamoja na mambo mengine alitaka kujua sababu za wimbi la wanasiasa hao kuhamia CCM na iwapo kama Serikali inapata hasara katika kugharamia uchaguzi mdogo wa marudio.

Pia mwanafunzi mwingine wa kidato cha sita kutoka Shule ya Sekondari Kisutu, alikosoa hoja zilizowasilishwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ghana, Profesa Ransford Van Gyampo, kuwa maendeleo ya nchi za Afrika yamekwamishwa na udikteta.

“Nchi kama Ujerumani kipindi cha vita walikuwa wakiongozwa kidikteta na walipata maendeleo makubwa, hili huwezi kufananisha na nchi za Afrika ambazo licha ya kuwa na demokrasia zimeshindwa kupiga hatua kimaendeleo,” alisema mwanafunzi huyo.

Lowassa

Akichangia mjadala huo, Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema wananchi wamejengewa hofu na chuki ili wawachague watu wasiowataka licha ya kutokuwapo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani pindi uchaguzi unapofanyika.

Alitolea mfano uchaguzi mdogo wa ubunge wa Monduli kwamba kulikuwa na magari zaidi ya 45 ya polisi pamoja na magari manne yenye maji ya kuwasha.

“Jana (juzi) Mzee Butiku amezungumza juu ya amani na akasema kuna viashiria vya kukosekana kwa amani. Mimi neno hilo halinitoshi, msamiati huo nahitaji uwe mkali kidogo.

“Mimi naona nchini kuna hofu na chuki. Inajengwa hofu kubwa kwa wananchi inayowafanya wawachague watu wasiotaka kuwachagua.

“Kwa mfano kamji kale (Monduli) kalikuwa kamezungukwa na magari ya jeshi utafikiri kuna vita. Vitu hivyo vinafanywa kwa kutumia vyombo vya dola kusimamia uchaguzi, inakuwa ni tabu sana,” alisema.

 

Pia alisema licha ya baadhi ya wanasiasa kuuponda Uchaguzi Mkuu wa Kenya, kwa upande wake aliupenda kwa sababu waliwafuata watu waliofanya makosa katika tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kwa kuwapeleka mahakamani na kuadhibiwa.

Alisema wanaosimamia uchaguzi nchini ni watumishi wa Serikali na wanalipwa na Serikali, jambo ambalo si rahisi kuacha Serikali ianguke.

“Miongoni mwa watumishi hao, wapo waliosema waziwazi kuwa hawawezi kuiacha Serikali ianguke, zimewekwa mbinu ili wapinzani wasishinde uchaguzi wa marudio.

“Kuna chuki mbaya imefikia hatua mwanachama wa Chadema na CCM wanachukiana. Inatia hofu kwa wananchi,” alisema.

Alisema kuna ulazima sasa wa kuzungumza na wananchi ili waachane na chuki na kutokuwa na hofu kwa kuzingatia mapendekezo ya Katiba Mpya yaliyotolewa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.

“Haitoshi kuwaambia kuna viashiria (vya hofu na chuki), waambiwe wazi hili na hili si sawa. Bila demokrasia hakuna haki na bila haki hakuna demokrasia,” alisema.

Dk. Bashiru: Kuna hofu za kuchonga

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, alisema hakuna hofu nchini kama ilivyobainishwa na Lowassa bali hofu zilizopo ni za kuchongwa.

Dk. Bashiru alidai kusikitika kwa kuwa Lowassa baada ya kuwasilisha hoja zake katika mdahalo huo aliondoka, alimtaka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, amfikishie ujumbe.

Alisema Kigoda cha Mwalimu Nyerere hakijafa na suala la mijadala ni muhimu kama damu katika mwili.

Alisema kwa kuwa mijadala ya kisiasa ina faida za kubadilisha mazoea mabaya kwa jamii, kudumisha mazoea mazuri na kubuni mazoea mapya.

“Mimi kama Katibu Mkuu wa CCM nitapigia debe bajeti kwenye vyuo vikuu vya umma ili viweze kuzalisha wasomi watakaotukomboa kifikra na kimaendeleo, pia nipo tayari kujadiliana na wenzangu lakini si kwa kugombania mgawanyo wa madaraka ndani ya vyama ambayo baada ya kuyapata yanatumika kufanya matumizi ya anasa,” alisema.

Pia alisema habari za hofu alizozungumzia Lowassa zinahusu wezi wa mali za umma, wakwepa kodi, madalali wa mikataba ya Serikali na makuwadi wa soko huria ambao lazima wataishi kwa hofu.

Alisema wananchi wasikubali watu hao kuanza kusambaza hofu hiyo kwa jamii.

“Hofu ya wananchi ni upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii, hizo ni hofu za halali, ila zipo hofu za kuchonga, watu wana midomo mirefu na mipana, wanaelekea kwenye mitandao ya kijamii kutisha wananchi wakati wana hofu zao halisi, nchi hii hatukubali hofu za kuchonga.

“Tusisambaze habari kuwa kuna hofu, kuna hofu ambayo inagusa wala rushwa, hata kama wamekimbilia kwenye vyama tutawafuata, ilimradi haki imetendeka,” alisema.

Pia alisema suala la kulinda usalama katika kipindi cha uchaguzi ni wajibu wa Serikali kwa kuwa huwa kuna viashiria vya uvunjifu wa amani kwa kupitia kwa baadhi ya vijana ambao ni wafuasi wa vyama vinavyoshiriki chaguzi hizo.

“Eti majeshi yanapiga wapiga kura! Wakati vijana wanatembea na bisibisi, vijana wa Chadema na CCM, ni nadra katika ushindani kuwakuta wamekaa pamoja. Ni kweli kuna matatizo na kuna uwezo mdogo ila hatujafika kiwango cha kusema hakuna uhatarishi wa usalama,” alisema.

Alisema CCM inasimamia misingi ya Azimio la Arusha na kama kuna mwanachama asiyetaka ahamie chama kingine.

Alisema ndani ya CCM bado kuna matatizo ya kutoelewana kifikra na wezi wengi wamehodhi mali za chama hicho.

“Bado hatuelewani katika suala la itikadi ndiyo maana tumekubaliana kuanza kujenga vyuo vya itikadi,” alisema.

Pia alisema wanachama wengi CCM hawana nidhamu, wanatumia ovyo fedha za chama na wakikemewa wanakuwa wakali.

“Nimekuwa kwenye tume ya uhakiki wa mali za CCM, wengine waheshimiwa lakini wezi, nikiwataja hamtaelewa wameiba ardhi, magari, mwingine nilimkamata na gari nikamwambia ushuke hata kama yeye ni mbunge ashuke kama sivyo nitamwita polisi… leo ukimsikia anabwatuka, unaona kwamba mzalendo, mpenda maendeleo wakati ni mwizi,” alisema.

Alisisitiza vyama vya siasa kujenga misingi ya kujitegemea ili matajiri wasihodhi nafasi ndani ya vyama hivyo na kupanga safu za uongozi.

“Wafukuzeni matajiri ambao wanataka kuja kuleta fedha kupanga safu za chaguzi.

“Nimefanya chaguzi Buyungu matajiri wananipigia simu eti usikwame katibu mkuu, nikawaambia nina fedha za kutosha, nimeshinda uchaguzi wao wanasema tumeiba kura,” alisema.

Butiku: Mabadiliko ya Katiba hayaepukiki

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, alisema ni jambo jema kufanya mabadiliko ya Katiba kwa kuwa wananchi hawaridhishwi na mambo yanayoendelea katika chaguzi mbalimbali nchini.

Butiku alisema kila mara baada ya wananchi kupiga kura kunakuwapo na vurugu zinazosababishwa na viongozi ambao wanajulikana, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.

Zitto: Rais atuite wanasiasa na kuweka mezani kero zake

Naye Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema tangu alipoingia madarakani Rais Magufuli alionyesha kutokubaliana na baadhi ya mambo ya wapinzani lakini cha ajabu hadi sasa hajawaita na kueleza kero zake.

“Jambo ambalo naumia halifanyiki, ni kwamba Rais alipoingia madarakani alionesha demokrasia yetu inaturudisha nyuma, njia pekee naona ni kwamba kuna mambo ambayo ni kero kwake ayaweke mezani na ambayo tunaona ni kero tuyaweke mezani tukubaliane.

“Kwamba ndugu zangu mnatukana mno na sisi atuambie hayo matusi, akishayataja na sisi tutamwambia hili si tusi, ni kukosoa, tutakubaliana tutasonga mbele,” alisema.

Alisema wapinzani wanachodai ni angalau Katiba ya sasa iheshimiwe na mikutano ya kisiasa iendelee kufanyika.

Alisema licha ya Dk. Bashiru kusema hakuna hofu, kwa upande wake anaona kuna hofu kwa sababu waandishi wa habari wanatekwa, wafanyabiashara wana hofu mwenzao ametekwa, wanasiasa wanapigwa risasi.

“Hivyo kuitishwe mjadala tukubaliane kuwa wewe CCM una hili sisi hatukubali na wewe Chadema una hili sisi tukubali, kwa hiyo nakubaliana hofu itapungua na kujenga demokrasia ndani ya nchi yetu.

Alisema licha ya watu kufurahia vitendo vya utumbuaji kwa watendaji wa Serikali, huo si uwajibikaji kwani kuna ufisadi mwingi.

“Kwa mfano leo ukienda benki ukiomba noti mpya, huipati kwa sababu kuna ufisadi mkubwa kwenye uchapishaji wa noti zetu, kampuni zilizopewa kazi hadi leo hakuna hela, sasa hivi hela ikichafuka inarudishwa vile vile kwa sababu hakuna noti mpya, kuna kuchezewa kwa zabuni hiyo,” alisema.

Makinda: Hatujaacha misingi ya Nyerere

Kwa upande wake, Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda, alisema si kweli kwamba awamu hii imeacha kutekeleza misingi aliyoacha Mwalimu Nyerere.

Pia alisema Bunge linaloongozwa na Spika Job Ndugai, lina uhuru wa kumkosoa pale alipoishia.

“Kama nimekosea wenzangu lazima wasahihishe. Wasahihishe waende mbele zaidi,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here