24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

UCHOMAJI VIFARANGA WAIBUA MJADALA

 

ASHA BANI na ELIA MBONEA

BAADA ya vifaranga 6,400 vilivyokamatwa katika mpaka wa  Namanga wilayani Longido  mkoani Arusha, kuteketezwa kwa moto, kumeibuka mjadala mzito kutoka kwa watetezi wa wanyama kuwa kitendo hicho hakikubaliki.

Mjadala huo, umelenga hasa vifungu vya sheria ambavyo vimekuwa na mvutano, wakati Serikali ikisema hakuna sheria iliyokiukwa.

Vifaranga hivyo vyenye thamani ya Sh milioni 12.5 mali ya mfanyabiashara, Mary Matia (23) mkazi wa Mianzini jijini Arusha, viliteketezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na vyombo vya ulinzi.

Baada ya kuteketezwa malalamiko yameibuka mengi ambako watu wamekuwa wakidai ni ukatili na kinyume na haki za wanyama na ndege.

Akizungumza na MTANZANIA  jana, kuhusu madai hayo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega  alisema hakuna sheria iliyovunjwa.

Alisema Sheria ya Magonjwa ya Wanyama na Mifugo namba 17 ya mwaka 2003 iko wazi kwa sababu inafafanua uhalali wa hicho kilichofanyika.

“Sheria inasema ‘destroy and diseased’… kwa hiyo kilichofanyika hapo ni usahihi kabisa ila tu watu wanajadili na kuhusisha vitabu vya dini, wanaweka huruma bila kujua yanayoendelea.

“Wanashindwa kufahamu namna  vifaranga hivi vilivyoingizwa nchini, vingeleta madhara,kuua soko na hata kuleta maradhi zaidi,’’alisema Ulega.

Alisema wasiwasi mkubwa, ni pale mfanyabiashara huyo alipoulizwa kama ana vibali kutoka nchini kwake, ikiwamo cha madaktari wa mifugo kuthibitisha kama mifugo hiyo haina maradhi au laa, hakuonyesha aina kibali chochote.

Alisema Watanzania ni wepesi kusahau kwa sababu kumbukumbu zinaonyesha ugonjwa wa mafua ya ndege uliwahi kuzikumba nchi za jirani na kuleta madhara .

“Endapo ugonjwa huu ukiingia nchini mwetu,Serikali inabidi ianze kuteketeza mifugo yote aina ya ndege ili kuogopa kuendelea kuua watu.

‘’Wapo wafanyabiashara wanalalamika kukosa soko la vifaranga, huku mayai yanadoda wakati wakenya wanaingia na kuuza bila vibali…hili hawalioni?’’alihoji Ulega.

Alisema kama watu wanaona sheria hiyo, ina makosa inapaswa kufanyiwa marekebisho, basi kuna taratibu  kufuata ili ifanyiwe marekebisho

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Dk. Abdul Hayghaimo alisema uteketezaji huo, umezingatia Sheria ya Magonjwa ya Mifugo Sheria  namba 17 ya mwaka 2003 kifungu 8 (1) kinampa uwezo wa kukamata mifugo ama bidhaa za mifugo iliyoingizwa  nchini kinyume na sheria cha  namba 31 (1) 43 (a na b) na 61 (1) hivi vinasapoti kuharibu.

Chadema yalaani

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje , Mawasiliano Itifaki  na Uenezi,  John Mrema alilani kitendo alichokiita cha kikatili.

“Tunalaani kitendo cha kikatili  ambacho Watanzania hatujawahi wala kuzoea kukiona kuvichoma vifaranga vizima hadi vinateketea, ni ajabu hata sheria ya mifugo na ustawi wa wanyama kifungu namba 19 ya mwaka 2008 kinakataza kuwateketeza ,’’alisema Mrema.

Watetezi

Katika hatua nyingine, watetezi wa haki za wanyama na ndege, wamelaani uamuzi wa kuchomwa moto vifaranga hivyo.

Akizungumza na MTANZANI ofisini wake mjini hapa jana, Mkurugenzi Mtendani ya Shirika lisilo la kiseriali la ‘The Arusha Society Protection of Animals’ (ASPA), Livingstone Masija alisema kitendo hicho ni cha kikatali.

Alisema licha ya sheria kuwapo za kusimamia mazingira ya viumbe kama  hao, bado ubinadamu ulihitajika zaidi.

“Uamuzi  uliochukuliwa ni wa kikatili zaidi tunajua sheria zipo, lazima zizingatiwe… kuwe na ubinadamu katika kutekeleza majukumu ya kisheria,” alisema Masija

Alisema kila mnyama au ndege wa kufugwa anayo haki ya kuishi na panapohitajika kumuua ipo njia bora ya kumteketeza, badala ya kutumia njia za kumchoma akiwa hai

“Yale ni mauaji ambayo kwa ujumla hayastahili wala hayawezi kuvumilika kitaifa wala kimataifa. Ustaarabu wa taifa lolote pia huonekana kwa namna ya watu wanavyoishi na wanyama na ndege wanavyofugwa.

“Walipaswa kupuliziwa dawa itakayowalewesha kisha wakafa wenyewe usingizini, baada ya hapo ndipo zingefuata hatua za kuwafukia,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles