23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Tunalaani mauaji haya, wahusika wasakwe

Mwandishi Wetu

MATUKIO ya watu kujichukulia sheria mkononi hayaruhusiwi kisheria kutokana na ukweli kuwa yanakatisha uhai watu.

Tabia hii imekuwa ikikemewa siku hadi siku na vyombo vya dola, lakini wananchi wamekuwa wakikaidi na kuendelea kuchukua sheria mkononi ambazo zinasababisha maafa makubwa.

Tumelazimika kusema haya kutokana na tukio la kusikitisha la wananchi kujichukulia sheria mkononi na kusababisha vifo vya watu wanne wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Hakuna mtu aliyepewa dhamana ya kukatisha uhai wa mwenzake, tukio hili  linasikitisha.

Katika mauaji hayo, watu wanne wa familia moja waliuawa kinyama kwa kukatwakatwa kwa mapanga na kundi la wananchi kwa kuwatuhumu ni washirikina.

Watu hawa akiwamo baba wa familia ya Petro Sagalika ambaye ni mganga wa kienyeji wameuawa, akiwemo mwanawe ambaye alikuwa mjamzito.

Lakini unyama huu haukuishia hapo, kwani baada ya mauaji haya, wananchi waliamua kuchoma vitu vya ndani na kubomoa nyumba, kitu ambacho hakikubaliki katika jamii iliyostaharabika.

Hatuamini kama marehemu wote hawa walikuwa wanatuhumiwa kwa imani za ushirikina hadi kufikia hatua ya kuuawa.

Mbali na Sagalika, wengine waliouawa ni mke wake, Suzana Mkuka na watoto wao, Fonsi Petro na Aniza Petro aliyekuwa mjamzito.

Inasikitisha kuona wananchi hawa bila huruma wanachukua uamuzi wa kutoa roho watu ambao inawezekana hawakuwa  na hatia yoyote.

Kwanini suala hili hawakulipeka sehemu husika ili hatua zichukuliwe, licha ya ukweli siku zote Serikali haiamini masuala ya ushirikiana?

Tunasema hivyo kwa sababu, tukio hili limeacha simanzi na huzuni kubwa kwa jamii nzima na watoto wengine wa marehemu waliobaki.

Ni wazi waliobaki katika familia hii wataendelea kuishi maisha ya wasiwasi na kushindwa kuendelea na majukumu yao ya kila siku katika uzalishaji mali, wakihofia usalama wao.

Huu ni ukatili ambao haupaswi kufumbiwa macho, mamlaka zote za Serikali zifanye kazi usiku na mchana kuhakikisha  wale wote waliohusika wanakamatwa.

Hali hii inasababisha wengi wa wanafamilia kukosa uhakika wa kuishi kijijini hapo kwa amani na utulivu.

Katika tukio hili, baadhi ya wanafamilia, hasa watoto wadogo walilazimika kujificha katika mashamba ya migomba ili kujiokoa na mauaji.

Tunamshauri Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange na kamati yake ya ulinzi na usalama kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wahusika wote wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Polisi wetu tunategemea hawatalala kuhakikisha kila anayedaiwa kuhusika anakamatwa kwa sababu hakuna aliyepewa haki ya kukatisha uhai wa mtu.

Lakini pia wakati kamatakamata hii inaendelea, ni vema kamanda wa polisi mkoa huo kwa kushirikiana na timu yake wakafanya mikutano na kuzungumza na wananchi kuhusu athari za kujichukulia sheria mkononi.

Tunaamini mikutano hii itasaidia maana, maelezo ya kina yatatolewa na wataalamu mbalimbali.

Lakini pia viongozi wa dini ambao tunaamini wako karibu zaidi na wananchi, wanapaswa kukemea hali hii kwa nguvu kubwa kwa sababu inaathiri jamii na ni aibu kwa taifa letu.

Viongozi wa dini kwa kutumia nafasi zao, tunaamini wana uwezo mkubwa wa kukemea matukio haya ambayo hakika yameshika kasi katika mikoa mbalimbali nchini.

Tunalaani vikali mauaji haya na kulitaka Jeshi la Polisi kuwasaka kwa udi na uvumba wahusika wote ili wafikishwe mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles