24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TRA: KAKOBE ANAHIFADHI FEDHA KWENYE MAJABA, NDOO

 

Mwandishi Wetu- Dar es Salaam


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe hana akaunti katika taasisi yoyote ya fedha nchini.

Imesema Kakobe amebainika kuwa mmoja wa wasimamizi wakuu wa akaunti za kanisa lake ambalo limehifadhi benki Sh. Bilioni 8.13 huku pia likiwa linahifadhi kiasi kikubwa cha fedha kwenye ndoo za maji na majaba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA),

Charles Kichere, licha ya Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship kuwa na kiasi cha fedha benk, limebainika kukwepa kodi ya Sh. milioni 20.83.

Katika taarifa yake iliyokuwa ikirejea ripoti ya uchunguzi wa TRA kuhusu kauli ya Kakobe kuwa na fedha nyingi kuliko serikali, alisema watoto wa Kakobe ambao wanajishughulisha na biashara nao walibainika kukwepa kodi ya Sh. milioni 37.28.

“Kufuatia kauli iliyotolewa na Askofu Kakobe katika mahubiri ya ibada ambayo alisema ‘Yeye ana pesa kuliko Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,’ TRA ilifanya uchunguzi kubaini usahihi wa kauli hiyo.

“Askofu Kakobe hana akaunti wala fedha katika taasisi yoyote ya fedha hapa nchini. Aidha uchunguzi ulibaini kuwa Askofu Kakobe ni mmoja wa wasimamizi wakuu wa akaunti za kanisa (signatories) zilizopo katika Benki ya NBC, zenye jumla ya kiasi cha Sh 8,132,100,819.00.

“Kiasi hiki cha fedha kimetokana na sadaka, zaka na changizo ambazo zinatolewa na waumini wa kanisa tajwa hapo juu, hivyo kwa mujibu wa sheria hakitozwi kodi,” alisema Kichere katika taarifa yake hiyo na kuongeza kuwa.

“Kanisa lilikwepa kulipa kodi Sh. 20,834,843.00 zilizotokana na uwekezaji katika makampuni ya kukuza mitaji. Kodi hiyo imelipwa baada ya uchunguzi,” alisema Kichere.

Akizungumzia Kampuni inayomilikiwa na watoto wa Kakobe, alisema imebainika kukwepa kulipa kodi Sh. 37,280,030.00.

Kwamba fedha hizo zililipwa baada ya uchunguzi na kufanya pesa ya kodi waliyokuwa wakidaiwa watoto wa Kakobe na kanisa lake kuwa Sh. 58,114,873.00.

“Kanisa linatunza kiasi kikubwa cha fedha kwenye ndoo na ‘majaba’ kinyume na taratibu za utunzaji wa fedha, lakini pia uwekaji na utoaji wa fedha nyingi kutoka benki haushirikishi vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya usalama wa fedha zenyewe na wahusika,” ilisema taarifa hiyo.

Ilisema TRA ilibaini pia kanisa hilo kutotengeneza hesabu za mapato na matumizi ya fedha  kwa mwaka jambo ambalo ni kinyume na Katiba ya Kanisa pamoja na sheria za usimamizi wafedha.

Kichere alisema aina hiyo ya utunzaji wa fedha imesababisha kuwepo matumizi mabaya ya fedha za waumini huku akiitaja moja wapo kuwa safari za nje anazofanya na familia yake kwa udhamini wa kanisa.

“Vile vile fedha za Kanisa zinatumika kujenga nyumba ya mke wa Askofu, kwa jina lake na wala si kwa jina la Kanisa kitu ambacho ni kinyume na taratibu za Kanisa.

“Aidha, wakati uchunguzi huo ukiendelea, Januari 24  mwaka huu, Askofu Kakobe aliandika barua kwa Rais John Magufuli kuomba radhi kwa kauli yake ya kebehi pamoja na matamshi yake ya dharau kwamba ana pesa nyingi kuliko Serikali,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema pia kuwa, TRA inatoa wito kwa taasisi zote za dini zinazojihusisha na shughuli za kiuchumi kulipa kodi stahiki na kwa wakati kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kodi.

“Mamlaka ya Mapato Tanzania inazitaka taasisi zote za kidini kufuata katiba zao ikiwa ni pamoja na kutengeneza hesabu za mapato na matumizi,” ilisema taarifa hiyo ya Kichere.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles