24.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

SHILINGI ‘MILIONI 80’ KUMZIKA AKWILINA

VERONICA ROMWALD NA PATRICIA KIMELEMETA- DAR ES SALAAM


FAMILIA ya marehemu, Akwilina Akwilini, imeipa Serikali mapendekezo ya bajeti ya Sh milioni 80,  zinazotarajiwa kutumika kwenye mazishi ya mwanafunzi  huyo.

Marehemu Akwilini aliyeuawa Februari 16, mwaka huu baada ya kupigwa kichwani na kitu kinachodhaniwa kuwa ni rasasi iliyofyatuliwa na askari polisi waliokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chadema wakati wakiandamana, anatarajiwa kuzikwa siku ya Ijumaa, Februari 23.

Mapema jana, Msemaji wa familia ya marehemu, Festo Kavishe aliwakabidhi Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwipalo na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisali Makori karatasi iliyoandikwa makadirio ya bajeti hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa dada wa marehemu Mbezi Luis jijini hapa, Kavishe alisema hayo ni mapendekezo ya awali ya familia na kwamba yanaweza kubadilika wakati wowote.

“Hayo ndiyo makubaliano ya familia, tumewakabidhi wajadiliane kisha tutakutana nao saa 10 jioni leo (jana), watatueleza ya kwao pia.

“Nisingependa kuizungumzia sana hii bajeti ya awali kwa sababu yenyewe ni ‘rough budget’ na inaweza kupungua au kuongezeka, tunachohitaji ndugu yetu apumzike kwa amani,” alisema Kavishe.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. alisema wamepokea makadirio hayo, watayajadili na kuipa taarifa familia hiyo.

 

Mchanganuo wa bajeti

Mchangunuo wa bajeti hiyo unaonyesha jeneza litagharimu Sh. 1,500,000, gharama za hospitali ni Sh. 200,000, gari la kubeba mwili wa marehemu Sh. 3,000,000, magari makubwa matano kwa ajili ya kubeba waombolezaji Sh. 20,000,000 na chakula njiani Sh. 3,000,000.

Pia bajeti hiyo inaonyesha chakula kinachotumika nyumbani Mbezi, mahali ulipo msiba tangu siku ya kwanza ni Sh. 10,000,000, viti 200 Sh. 400,000, turubai tatu Sh. 600,000, muziki na MC Sh. 400,000, video Sh, 1,000,000 na maji ya kutumia nyumbani Sh. 50,000.

 

Mahitaji ya msiba Rombo.

Bajeti inaonyesha chakula kitachotukimika Rombo kwa siku tano ni Sh, 30,000,000, muzika na MC ni Sh. 2,000,000, turubai Sh. 1,000,000, viti Sh. 400,000 maboza ya maji Sh. 100,000, kujenga kaburi Sh. 3,000,000, maua na mataji Sh. 1,000,000, mapambo Sh. 500,000 na dharura Sh. 2,000,000.

 

Matapeli waibuka

Kwenye jambo kuna mambo, ndivyo unavyoweza kusema kwani tayari watu wanaodaiwa kuwa ni matapeli wa mtandao wameanza kusambaza taarifa zinazohamasisha watu kutuma rambirambi.

Jambo hilo limewashangaza wengi kwani tayari Serikali imesema itagharamia shunguli zote za mazishi ya Akwilini.

Moja ya ujumbe uliosambazwa mitandaoni ukihamasisha watu kuchangia msiba unasomeka ‘namna ya kuchangia rambirambi kwa msiba wa Aquilina Aquiline, kama unatumia Vodacom na unataka kuchangia rambirambi ya Akwilina Akwilini piga 15000# chagua 4, lipa kwa M-pesa chagua 4 ‘week namba ya kampuni’ ingiza namba ya kampuni 150150 ingiza namba ya kumbukumbu 160160 ingiza kiasi TZS ingiza neno siri kukanilisha muamala.

‘Mchango huu unararibiwa na Bi Segolena Richard Wisso (0767 171 191) ambaye ni mama wa marehemu Akwilina Akwilini

 

Upumzike kwa amani Akwilina Akwilini.

 

‘Zimechangwa 147,000 TZS lengo 5,000,000, zimebaki siku 40, wawezeshaji 20.’

Akizungumza na MTANZANIA, Kavishe alisema ujumbe huo hawautambui na kwamba namba hiyo si ya mama wa marehemu.

“Hata sisi wametupigia, hao ni matapeli, hatuwatambui, naomba jamii iwapuuze, sisi hatuchangishi mchango kwenye simu, mtu aliye tayari kutuchangia afike nyumbani Mbezi Luis au pale Moshi hoteli ambako tunafanya vikao vya familia,” alisisitiza.

 

Jeshi laanza msako

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa jana aliliambia MTANZANIA kuwa wananchi wapuuze ujumbe huo.

Kamanda Mambosasa alisema ujumbe huo unatumwa na matapeli kwa sababu msiba wa Akwilina unasimamiwa na Serikali na tayari vikao vya mazishi vimeanza kufanyika kati ya viongozi wa Serikali na wanafamilia.

“Nimeshangazwa kuona meseji zinapita kwenye mitandao ya kijamii za kuwataka kutoa michango wakati msiba wa Akwilina unasimamiwa na Serikali na vikao vimeanza kufanyika,” alisema Mambosasa.

Alisema matapeli hao wanataka kutumia msiba huo kwa ajili ya kujinusha jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Kamanda Mambosasa alisema polisi wanawasaka wananchi wanaotuma meseji hizo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

 

Wanafunzi wataka ripoti

Serikali imeombwa kulifanyia kazi sakata la kifo cha Akwilina na kueleza ukweli wa mambo.

Waziri wa Fedha wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha St. Joseph, Nuru Zephania jana alikaririwa na waandishi wa habari akiwa nyumbani kwa dada wa marehemu pamoja na viongozi wenzake kuhani msiba.

“Tuna imani na Serikali kwamba  italifanyia kazi sakata la kifo cha Akwilina, tunalaani tukio hili ndiyo maana tuliungana nchi nzima tukatoa salamu za pole na Serikali tuliitaka ijitathmini katika hili, hili lipo mikononi mwao na walifanyie kazi na juhudi za dhati zifanyike kujua uhalisia wa mambo haya,” alisema.

 

Mwili kuagwa mara mbili

Akizungumza ratiba ya kuagwa mwili wa Akwilina, mmoja wa wanafamilia aliyejitambulisha kwa jina la Valentino Akwilin alisema utaagwa nyumbani na chuoni alipokuwa akisoma, NIT.

“Saa tatu wataenda kuchukua mwili Muhimbili utaletwa nyumbani, saa saba utapelekwa NIT na saa nane tunatarajia msafara utaanza kwenda Rombo kwa maziko,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles