NA ZAINAB IDDY,
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema kuwa linautambua uongozi mpya wa klabu ya Stand United ambao umeingia madarakani hivi karibuni na kubariki utendaji wake wa kazi.
Ofisa Habari wa TFF, Alfredy Lucas, alisema Kamati ya Uchaguzi ya TFF imepitia vielelezo na vipengele vyote vilivyofuatwa katika uchaguzi huo na kubaini kuwa ulikuwa wa huru na haki.
“Kama TFF tumeukubali uchaguzi uliofanywa na Stand lakini pia tuwatakia majukumu mema ya kuongoza timu hiyo katika kipindi cha miaka minne ijayo na hiyo inatokana na uchaguzi wao kufuata taratibu zote.
“Katika usajili wa timu kuna Stand United FC na si Stand United kampuni, hivyo uchaguzi uliofanywa ni wa haki na huru ukizingatia waliopiga kura ni wanachama wanaotambuliwa na timu hiyo,” alisema Alfred.
Kabla ya TFF kutoa msimamo wake huo, Stand United ilijikuta ikiwa njiapanda baada ya kuibuka makundi mawili yanayohasimiana, huku kila moja likidai lina haki ya kuendesha na kusimamia mambo ya timu hiyo likiwemo suala la usajili.