25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA: TUNAONEWA

Na JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM

UONGOZI wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, umedai kuwa umechoka kuonewa kutokana na maamuzi ya utata yanayotolewa na waamuzi katika mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema  kutokana na kuchoshwa na maamuzi hayo, wameiandikia barua Bodi ya Ligi Kuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT), wakizilalamikia kudhulumiwa ushindi katika mechi tatu za ligi hiyo msimu huu.

Manara alizitaja mechi hizo kuwa ni dhidi ya Mbao FC iliyochezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Stand United  katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na nyingine dhidi ya watani wao wa jadi Yanga iliyochezwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita.

Alisema wamechoka kuonewa hivyo wameamua kuandika barua na kuambatanisha na video za mechi hizo ili viongozi husika watambue na kuona waamuzi wa Tanzania wanaovyoonesha uonevu wa wazi kwa klabu hiyo.

“Waamuzi wote waliochezea mechi hizo tatu hawajafanya haki, sisi tunahitaji kama ni ushindi uwe wa haki, lakini tunashangaa kuona wanatudhulumu haki zetu.

“Kila mara tumekuwa tukililalamikia suala la waamuzi, lakini  hakuna kinachofanyika, sasa tumeamua kuandika tena na kuambatanisha na video ili wahusika waziangalie,” alisema Manara.

Alisema kila wanapokutana na Yanga, lazima watabebwa sababu mwamuzi anakuwa ametoka nyumbani na matokeo yake binafsi.

Alisema waamuzi wanachangia soka la Tanzania kutopiga hatua yoyote kutokana na maamuzi ya ovyo ambayo wamekuwa wakiyatoa viwanjani.

Wakati huo huo, Manara alisema usalama mdogo wa Uwanja wa Uhuru umechangia kwa asilimia kubwa idadi ndogo ya mashabiki kujitokeza katika mchezo dhidi ya Yanga, uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Alisema mashabiki na wadau wengi waliogopa kujitokeza kwa wingi katika uwanja huo kutokana na kuhofia usalama wao.

“Tulisisitiza Serikali yetu ituruhusu kutumia Uwanja wa Taifa ila ilikuwa ngumu kukubaliwa, lakini tuliheshimu maamuzi ya Bodi ya Ligi Kuu (TPBL), matokeo yake mashabiki waliojitokeza ni aibu, haijawahi kutokea mechi kati ya Simba na Yanga ikawa na idadi ndogo ya mashabiki kama hii.

“Simba na Yanga ni klabu kubwa nchini, hata kama zimekuwa na mapungufu mbalimbali zinatakiwa kupewa heshima kubwa  maana ndio waanzilishi wa mechi za ushindani,” alisema Manara.

Alisema kikosi hicho kinatarajia kuelekea Mbeya Ijumaa kujiandaa na mechi  dhidi ya Mbeya City, mchezo utakaochezwa Novemba 5, mwaka huu katika Uwanja wa Sokoine.

Alisema maandalizi kwa ajili ya mechi hiyo yameanza na timu ilitarajiwa kuanza mazoezi leo (jana) jioni katika Uwanja wa Polisi Kurasini.

Alisema baada ya mechi dhidi ya Mbeya City, timu itakuwa na mapumziko ya wiki mbili kabla ya kuikabili Tanzania Prisons Novemba 18, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles