24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 7, 2024

Contact us: [email protected]

ODINGA: TUNAUNDA BUNGE LA WATU KUIONGOZA KENYA

NAIROBI, KENYA

KIONGOZI wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), Raila Odinga, amesema wako mbioni kuunda ‘Bunge la Watu’ kuiongoza Kenya hadi mhimili halali wa utendaji utakapochaguliwa na kuundwa.

Alisema hayo jana wakati akizungumza kwa mara ya kwanza tangu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), imtangaze Rais Uhuru Kenyatta kushinda uchaguzi wa marudio wa urais  Oktoba 26, mwaka huu.

Odinga aliususa uchaguzi huo, akipinga kutofuatwa kwa masharti, ikiwamo mageuzi ndani ya IEBC.

Akizungumza jana katika Makao Makuu ya Okoa Kenya jijini Nairobi, alisema uchaguzi huo wa marudio ulikuwa wa udanganyifu na kwamba kamwe hawatamtambua Kenyatta wala Serikali yake.

“Badala yake leo tunaanzisha Bunge la Watu kurejesha demokrasia ya nchi hii.

“Bunge la Watu litakuwa na vijana, viongozi wa dini, makundi yenye masilahi ya kiuchumi na taasisi za kiraia,” alisema Odinga.

Alisema kuwa Nasa itawasilisha hoja za kuundwa kwa chombo kipya cha kuiongoza Kenya kwa mabunge ya kaunti kwa majadiliano na kupitishwa.

“Ratiba ya baraza hilo itatolewa muda si mrefu,” alisema.

Awali Odinga alisema Vuguvugu la Taifa la Ukombozi la Nasa (NRM) litaendesha kampeni kali za kuunga mkono demokrasia kupitia ususiaji wa kiuchumi, migomo na vikwazo vya hapa na pale.

Odinga aliponda maandalizi na uendeshaji wa uchaguzi wa marudio, ambao ulitokana na kufutwa kwa ule wa kwanza wa Agosti 8, mwaka huu, ambao pia Kenyatta alitangazwa mshindi baada ya Mahakama ya Juu kubaini madudu yaliyofanywa na IEBC.

Alisema uchaguzi huo haukuwa na vigezo vilivyowekwa na sheria za uchaguzi, Katiba na Mahakama ya Juu.

Kwanza, alisema uchaguzi huo ulipaswa kuendeshwa na  Tume ya Uchaguzi kama ilivyoamriwa na Mahakama ya Juu, lakini badala yake ni Serikali kupitia makamanda wa Jeshi la Polisi na wanasiasa wa Jubilee waliouendesha.

Alidai idadi ya waliojitokeza kupiga kura ilikuzwa katika ngome kadhaa za Jubilee ili kumpatia Kenyatta ushindi na kujenga picha kuwa Wakenya walishiriki katika uchaguzi huo wa marudio.

KAULI YA KENYATTA

Kwa upande wake, wakati akitoa hotuba muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi, Rais Kenyatta, alimtaka Odinga kwenda mahakamani kwa mara nyingine kupinga uchaguzi wake.

“Wawacheni kwanza watumie njia zote za kisheria zilizosalia, wawacheni wafanye wanachotaka. Hakuna mtu yeyote atakayewadhulumu haki yao ya kikatiba.

“’Kuhusu ajenda yangu ya kusonga mbele, nitazungumza baada ya makabiliano ya mahakamani kwisha,” alisema Kenyatta katika makao makuu ya IEBC katika eneo la Bomas jijini Nairobi juzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles