24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

SAMATTA NA SAFARI YAKE KIMATAIFA

Na HASSAN DAUDI-DAR ES SALAAM


HIVI karibuni, Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf), lilitaja orodha ya wanasoka watakaoiwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa mwaka huu, na mshindi wake atatangazwa kwenye hafla itakayofanyika Januari 4 mwakani mjini Accra, Ghana.

Katika listi hiyo iliyojaa mastaa wanaokipiga barani Ulaya, wakiwamo Sadio Mane na Mohamed Salah (Liverpool), Victor Moses (Chelsea), Naby Keita (Leipzig), Yacine Brahimi (Porto) na Piere-Emerick Aubameyang (Borussia Dortmund), lilikuwamo jina la Mtanzania Mbwana Samatta.

Kwa upande mwingine, kuingia kwenye listi hiyo ni mara yake ya kwanza. Lakini pia, anakuwa Mtanzania wa kwanza kuwa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Makala haya yamekuandalia safari ndefu ya mwanasoka huyo ambaye kwa sasa anakipiga barani Ulaya katika klabu ya Genk inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ubelgiji.

Atua TP Mazembe kisa mabeki wanne

Safari ya Samatta katika soka la kulipwa ilianza mwaka 2011 akiwa na kikosi cha Simba SC ambayo alijiunga nayo akitolea African Lyon.

Samatta, ambaye kwa kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 19, alisajiliwa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Licha ya kuwa hakuwa amecheza mechi nyingi katika kikosi cha Simba baada ya kuugomea uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi akidai baadhi ya stahiki zake, straika huyo aliwavutia mabosi wa TP Mazembe wakati timu yao ilipovaana na Simba katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ulikuwa ni mchezo wa marudiano uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo aliwapiga chenga mabeki wanne wa TP Mazembe, jambo ambalo lililivutia benchi la ufundi la timu hiyo ya mjini Lubumbashi.

Usajili wake Sh mil. 440

Kwa mujibu wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba kwa kipindi hicho, Ismail Aden Rage, TP Mazembe walikubali kuzama mfukoni na kutoa kitita cha Dola za Marekani 150,000, ambazo ni zaidi ya Sh mil 440 za Tanzania.

Rage alisema katika mgawo huo, klabu yake ya Simba ingevuna Dola 100,000 (zaidi ya Sh mil 290) na Samatta mwenyewe angepata kiasi kilichobaki, yaani Dola 50,000.

Atupia mechi ya kwanza Mazembe

Katika mchezo wake wa kwanza akiwa na ‘uzi’ wa Mazembe, Samatta aliwathibitishia mabosi wa timu hiyo kuwa hawakukosea kumfuata Bongo baada ya kufunga akitokea benchi.

Katika mtanange huo dhidi ya Republican Guard, alifunga bao pekee katika dakika ya 89.

Haikuishia hapo, akatoa ‘asisti’ mbili katika mchezo mwingine dhidi ya FC Saint Pierre, ambao timu yake iliibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-0.

Atajwa Mchezaji Bora Mazembe

Baada ya mchango wake wa mabao kikosini na hata kuiwezesha Mazembe kufanya vizuri Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa Afrika na hata Kombe la Shirikisho, Samatta alichaguliwa kuwa mchjezaji bora wa timu hiyo kwa mwaka 2013.

Samatta alipewa heshima hiyo baada ya kujizolea kura 248, akiwapiku Asante Solomon (219), Robert Kidiaba (200), Nathan Sinkala (97) na Rainford Kalaba (67).

Aipeleka Mazembe fainali, atwaa kiatu cha dhahabu

Mashabiki wa Mazembe hawatasahau kile alichokifanya Samatta katika mtanange wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015.

Straika huyo alitumia dakika mbili pekee kuzitikisa mara mbili nyavu za Al Merreikh ya Sudan na mabao yake hayo yaliwezesha Mazembe kuwamaliza Merreikh na kuipeleka timu hiyo fainali kwa ushindi wa mabao 3-0.

Katika mchezo wa fainali, alizipasia mara moja nyavu za MC Alger ya Algeria, ambapo Mazembe walishinda mabao 2-0 na kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Kwa kufunga siku hiyo, alifikisha jumla ya mabao saba na kutajwa kuwa mfungaji bora wa mashindano hayo. Si tu kwa Samatta, pia ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kutoa mchezaji aliyeichukua tuzo hiyo.

Atajwa Mchezaji Bora wa Ndani Afrika

Usiku wa Januari 7 ulikuwa mzuri kwa Samatta kwani aliandika historia nyingine kwa kuiweka mkononi tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani

Katika kinyang’anyiro hicho, alikuwa akifukuzana na mchezaji wa kimataifa wa Algeria, Baghdad Boundjah, na kipa wa TP Mazembe, Robert Kidiaba.

Baghdad ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho na Kidiaba aliiwezesha Mazembe kutwaa ubingwa wa Afrika kama alivyofanya Samatta.

Kwa kuichukua tuzo hiyo katika hafla iliyofanyika mjini Lagos, Nigeria, Samatta aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kuibeba.

Genk wamng’oa Congo kwa mbinde

Wiki chache baada ya kuinyakua tuzo hiyo, viongozi wa klabu ya Genk ya Ligi Kuu nchini Ugiriki walivutiwa na huduma yake ya mabao na kufunga safari hadi mjini Lubumbashi yaliko makazi ya Mazembe.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa mmiliki wa Mazembe, Moise Katumbi, kumruhusu Samatta kuondoka kwenye kikosi chake, hali iliyosababisha mvutano wa muda mrefu.

Taarifa zilidai kuwa Katumbi hakutaka Samatta aende Ubelgiji kwa sababu tayari alikuwa na mpango wa kumuuza Nantes ya Ligi Kuu Ufaransa ‘Ligue 1’.

Itakumbukwa kuwa hata Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, iliingilia kati ikiitaka Mazembe kumwachia nyota huyo.

Baada ya mvutano, huo hatimaye alifanikiwa kujiunga na Genk na kusaini mkataba wa miaka minne na nusu.

Tishio Genk, aipeleka Ligi ya Europa

Msimu uliopita, ambao ulikuwa wa kwanza kwake nchini Ubelgiji, Samatta alifunga mabao 10, timu yake ya Genk ilishika nafasi ya nane baada ya kufikisha pointi 48 katika mechi 30.

Mei 29, mwaka huu, Mbwana Samatta aliifungia Genk bao lililoiwezesha timu hiyo kushinda mchezo wake wa ‘play off’dhidi ya Sporting Charleroi na hatimaye kufuzu kucheza Ligi ya Europa.

Samatta alifunga bao la pili katika ushindi wa mabao 5-1, mchezo ambao walikuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Cristal Arena. Mchezo huo ulikuwa ni wa marudiano, mbali na ule wa kwanza ambao Genk walichapwa mabao 2-0 wakiwa ugenini.

Tangu kuanza kwa msimu huu wa 2017-18, tayari mchezaji huyo ameshaziona nyavu za timu pinzani mara nne, huku timu yake ikishuka dimbani mara 13, ikishinda mechi nne, sare sita na kushinda mara tatu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles