25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

SAKATA ESCROW: UHENGA WA KAFULILA KUWAUMBUA WENGI

                              David Kafulila

 

 

Na EVANS MAGEGE,

KATIKA maisha nimejifunza kitu kimoja kiitwacho ukweli. Nimeamini kwamba ukisimamia ukweli, hata kama utazibwa kwa kiwango gani, bado utabaki kuwa ukweli.

Kwa lugha ya picha, ukweli naweza kuufananisha na mpira wa miguu au kikapu uliojazwa hewa, kwamba hata kama una nguvu kiasi gani, hautaweza kuuzamisha kwenye pipa la maji, zaidi utakuponyoka na kuendelea kuelea.

Sakata la ukwapuaji wa Sh bilioni 309 kwenye Akaunti maalumu ya Tegeta Escrow, iliyokuwapo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati linaibuliwa liliikanganya jamii na hata lilipotulizwa liliacha maswali mengi yaliyokosa majibu kwa wakati ule.

Sakata hilo, ambalo chanzo chake kilitokana na wanahisa wawili wa Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), kwa sasa limeibuka kivingine, huku likigusa hisia za wengi kuhusu hatima ya wanufaika wanaofahamika na wasiofahamika.

Ikumbukwe ndani ya sakata hili kuna wanufaikaji wa fedha hizo, ambao baadhi wanafahamika kwa sababu walipata fedha zao kupitia Benki ya Mkombozi.

Hata hivyo, kundi jingine la walionufaika ambalo halifahamiki lilipata mgawo huo kupitia Benki ya Stanbic na hatima yao bado haijajulikana.

Tayari sakata hilo limewaingiza mahabusu vinara wake, James Rugemalira na Harbinder Seth, ambao wanakabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi.

Kukabiliwa na mashitaka kwa vinara hao kunatoa mwelekeo wa alama nyekundu kwamba  huenda hata wanufaika wa mgawo wa fedha hizo nao wanaweza kujikuta matatani iwapo vinara wa sakata hilo watatiwa hatiani.

David Kafulila si mhenga, kwa maana ya umri (mtu wa kale) au mzee wa baraza, bali unaweza kumjengea mtazamo wa uhenga kutokana na maarifa au uthubutu alioutumia kuibua sakata la ukwapuaji wa fedha hizo.

Maarifa aliyoyatumia kuliweka wazi sakata hilo ilitosha kabisa kumtafsiri kuwa alifahamu alitendalo wakati akitibua ukwapuaji wa fedha hizo.

Pamoja na kwamba Kafulia alielekeza hoja zake kuwa Serikali iliibiwa kupitia sakata hilo, lakini Serikali kwa upande wake ililazimisha kuzikana fedha hizo kwa kusema si zake, bali ni mali ya wanahisa wawili waliokuwa wanamiliki Kampuni ya kufua umeme ya IPTL.

Kimantiki, Kafulila alikumbana na vihunzi vingi kwenye uwasilishaji wa sakata hilo, alipuuzwa na ilifika mahali akatazamwa kama kibaraka au kiherehere anayetaka sifa za kisiasa.

Nakumbuka wakati fulani alipochochea zaidi moto wa sakata hilo ndani ya Bunge la 10 kwa hoja za kichokonozi, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alidiriki kumwita ‘tumbili’.

Haijulikani kama Werema alimwita Kafulila jina hilo kwa hasira au utani, lakini mtazamo wa jumla unaonyesha wazi kuwa Kafulia aliwakera wakubwa kutokana na ufuatiliaji na udadisi wa sakata hilo.

Pamoja na jitihada zake za kuliweka wazi sakata hilo kusongwa na vihunzi vingi,  hata hivyo hakukata tamaa kupigania kile alichokiamini kuwa ni sahihi kwake na kwa masilahi ya Taifa.

Mapambano yake kuhusu sakata la Escrow yaliacha alama kubwa ndani ya Serikali ya Awamu ya Nne.

Ni mapambano hayo hayo ndiyo yanatazamwa na wafuatiliaji wa siasa za nchi hii kuwa yalichochea kuangusha utetezi wa ubunge wake katika Jimbo la Kigoma Kusini.

Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, miongoni mwa wanufaika wa fedha za Escrow, Jumatatu ya wiki hii aliamua kurejesha serikalini fedha hizo kwa kigezo cha kulinda heshima na masilahi mapana ya nchi na chama chake.

Uamuzi huo wa Ngeleja unatoa tafsiri ya kuwa, kwa sasa wanufaika wa fedha hizo kila mmoja atabeba msalaba wake.

Uamuzi wa Ngeleja kurejesha fedha hizo umeibua maswali mengi miongoni mwa jamii na sehemu ya maswali hayo inahoji, kwanini sasa? Pia kurejesha fedha hizo kunafuta ujinai wa kosa husika?

Ifahamike kuwa, wakati anahojiwa na Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi Machi 4, mwaka 2015, Ngeleja alikiri kupokea Sh milioni 40.4 kutoka katika Kampuni ya VIPTZS Trustee na si Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited.

Hata hivyo, alifafanua kuwa, fedha hizo alizipata baada ya kuomba msaada kwa James Rugemalira, ambapo kama mwanasiasa, amekuwa akiomba msaada kwa wafadhili mbalimbali ili kushughulikia maendeleo ya jimbo lake.

Kwa utambuzi msaada huo, Ngeleja alisema alilipa asilimia 30, ambayo ni sawa na Sh milioni 13 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika utetezi wake wa msaada huo, Ngeleja alieleza bayana kuwa, wanasiasa wanaishi kwa kuombaomba kama ilivyo nchi, kwa sababu bajeti yake haijitoshelezi.

Ngeleja alitoa utetezi wake pasipo kuonyesha au kuahidi kuwa endapo fedha hizo zitaonekana kuwa na kasoro atazirejesha.

Swali la kujiuliza, nini kilichonyuma ya pazia ambacho kimemsukuma mwanasiasa huyo kurejesha fedha hizo sasa. Je, kuna shinikizo au amepima na kuona msaada huo unatoa ishara mbaya kwa mustakabali wa siasa zake?

Pia, kama fedha hizo zilikuwa za msaada na akajiridhisha kuwa anastahili kupewa, kwa nini arudishe sasa? Inamaana kwa muda wote tangu sakata la Escrow halijatibuliwa na Kafulila fedha hizo zilikuwa bado hazijakwenda kusaidia jimbo?

Hata hivyo, katika majibu yake wakati anatangaza kurejesha fedha hizo, Ngeleja alisema amechukua uamuzi wa kurudisha fedha hizo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya kujiridhisha kuwa aliyempa msaada huo anatuhumiwa na ana kesi mahakamani.

Katika maelezo yake, alisema  amejipima na kutafakari na hatimaye ameamua kwa hiari yake mwenyewe kuzirudisha fedha hizo serikalini, bila kujali alishazilipia kodi ya mapato TRA Januari, mwaka juzi.

Uamuzi huo wa Ngeleja ni hatua ya kwanza kuwa amekubali jinai na amerudisha na hivyo wenzake pia warudishe (asset recovery) ili wabaki na jinai ya kwanini walijipatia fedha hizo isivyo halali?

Kimantiki kurudisha fedha hizo hakumwondolei jinai yeyote aliyenufaika.

Uamuzi wa Ngeleja wa kuzirudisha fedha hizo ni sawa na kujitakasa na hauna tofauti na kilichofanywa wakati wa sakata la EPA, ambapo watu waliorejesha fedha hizo walisamehewa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria kwa sababu jinai haifutwi kwa kurejesha kilichokwapuliwa.

Hata hivyo, Ngeleja kajitakasa kwa kurejesha mgawo wa Escrow sxerikalini, hatujui kwa wanufaika wengine wa mgawo huo kama wataridhia kurejesha mgawo huo serikalini.

Maazimio ya Bunge la 10 kuhusu sakata la Escrow yaliyowasilishwa Novemba 28, mwaka 2014, yalitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, watu wote waliotajwa na Taarifa Maalumu ya Kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea.

Pia Bunge liliazimia kumtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Hata hivyo, majaji hao wameshaacha kazi, huku wakiacha maswali mengi.

Azimio jingine la Bunge ni kuitaka Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo.

Kimsingi hadi sasa leseni ya IPTL imemalizika jana na  mkataba wake unakwisha mwaka 2022.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles