25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI MAALUMU: MAMA LISHE KIMBILIO LA WATUMISHI, WANAFUNZI DRC

Wanawake wakiandaa chakula mtaani mjini Kinshasa

NA JOSEPH HIZA,

MIGOGORO na machafuko iliyopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), inaendelea kusababisha hali mbaya ya uchumi.

Kutokana na hali hiyo, si watu wengi wenye uwezo wa kumudu mahitaji mbalimbali, kitu kinachosababisha watafute njia mbadala.

Mojawapo ya njia hizo ambazo hata hivyo zimezoeleka katika mataifa mengine ikiwamo Tanzania ni ulaji vyakula mitaani badala ya kwenye migahawa.

Vyakula vinavyouzwa mitaani maarufu kama mama lishe au baba lishe vimegeuka kuwa kimbilio la wengi nchini humo, ingawa suala la usafi ni wasiwasi mno.

Kuanzia watumishi wa umma na wanafunzi hadi wafanyakazi wa sekta ya ujenzi na wazazi na watoto wao, wakazi wenye njaa wa Kinshasa huishi kwa kutegemea mama ntilie ambao nchini humo hujulikana kama ‘malewa.’

Na idadi ya wafanyabiashara hawa imeongezeka sambamba na wateja kwa kadiri uchumi unavyozidi kudhoofu.

Joseph Magamba, mwendesha taxi mwenye umri wa miaka 29, anasema anaweza kula chakula kwa malewa akitumia chini ya faranga  2000 ambazo ni sawa na Sh 2370 za Tanzania.

Joseph anaeleza hayo huku akiwa na sahani yenye mchuzi mzito wa kuku, ambayo aliilipia faranga 1,500, na pembeni kuongezea fufu, chakula kinachofanana na ugali kwa faranga 400.

Kijana huyo anasema katika hoteli ya kawaida angelazimika kuingia gharama mara 10 zaidi ili kupata mlo kama huo kitu, ambacho anasema hawezi kukimudu.

DRC imekuwa ikikabiliwa na migogoro ya kiuchumi na kisiasa kwa miaka mingi.

Mwenendo huo umesababisha kushuka kwa kiwango cha uzalishaji na kupanda kwa gharama ya maisha baada ya thamani ya sarafu ya nchi hiyo kuporomoka.

Lakini pia kitendo cha Rais Joseph Kabila kukataa kukabidhi madaraka Desemba mwaka jana, kimezidisha mgogoro wa kisiasa na hali kuzidi kuwa mbaya zaidi.

Kisingizio kilichotumiwa na Rais Kabila kukataa kuachia ngazi ni madai ya kutokamilika kwa zoezi la kuandikisha wapiga kura.

Novemba mwaka jana, Tume ya Uchaguzi nchini humo ilitangaza kuhitaji muda zaidi hadi Julai 2017 kusajili zaidi ya wapigaji kura milioni 30.

Hiyo ikawa sababu ya kutaka kuusogeza uchaguzi angalau kwa miaka miwili, kitu kilichogomewa na wapinzani kabla ya kuafikiana kufanyika kabla ya mwaka huu kuisha.

Makubaliano hayo hata hivyo, yalitokea kwa gharama ya damu za mamia ya waandamanaji waliokuwa wakipinga kubaki madarakani kwa Rais Kabila.

Mwishoni mwa 2016, serikali ilisema vyama vya upinzani vilikubaliana kuwa uchaguzi mkuu ungefanyika mwishoni mwa mwaka huu, mpango ambao ulipunguza hofu kati ya serikali na upinzani.

Lakini pia ni wiki iliyopita, serikali ilitangaza haina fedha za kutosha kuendeshea uchaguzi huo.

Waziri wa Bajeti Pierre Kangundia alidai gharama ya kuendesha uchaguzi huo ni dola bilioni 1.8, kiwango ambacho ni kikubwa mno kwayo.

Iwapo kweli uchaguzi hautafanyika mwaka huu baada ya kuahirishwa mwaka jana, maafa zaidi yatarajiwe hasa iwapo Kabila ataendelea kubaki madarakani.

Taifa hilo lina kati ya barabara mbovu zaidi duniani pamoja na mfumo duni wa mawasiliano.

Ijapokuwa taifa hili kubwa kieneo la katikati mwa Afrika ni tajiri kwa maliasili kama vile madini, maji na misitu, kwa muda mrefu limekuwa moja ya mataifa masikini zaidi duniani.

Ukosefu wa amani na utulivu wa kisiasa na kijamii umezidisha majanga ya kiuchumi nchini humo.

Magenge ya wauza chakula au mama lishe yamezidi kupata umaarufu mwaka mmoja na nusu uliopita mjini Kinshasa, jiji lenye wakazi milioni 10.

Si tu kwa watu hutafuta vyakula vya bei nafuu bali pia kwa wanawake wa nyumbani kama vile Marie Aloko Hioma, wamejitosa katika biashara ya kuuza vyakula mbele ya vyumba au mitaa yao mjini humo.

Kwa vile mjini Kinshasa kuna watu wengi wanaozidi kuongezeka wakiachana na utamaduni wa kula migahawani, ndivyo akina mama wanavyojitokeza kutumia fursa hiyo kujiunga na biashara hii.

Mama Marie mwenye watoto  wanane, anasema  ameanzisha sehemu hii ya kuuza chakula miaka sita iliyopita ili kuweza kulipia ada za shule ya watoto wake.

 Asubuhi saa 11 kila siku, watu huanza kujitokeza hapo kwake ili kupata samaki, kuku na pondu, chakula cha kienyeji kilichotengezezwa kwa mchanganyiko wa kisamvu na mboga mboga nyingine.

Kwa uhakika mama Marie hajui watu wangapi wanafika katika sehemu yake hiyo kwa siku.

“Nakisia ni kama watu 100 na kitu,” anasema. Kwa miaka saba pia Mama Annie amekuwa akifanya biashara kama hiyo, karibu na hapo.  Mapato yake anasema hutumia kwa ajili ya kununulia nguo za watoto wake.

Mmoja wa wateja wake wa kila siku, Papi Bula Mbemba (49), naye anasema:

“Hapa unapata chakula cha bei za kuridhisha. Sehemu hizi za vyakula zinawapatia watu wa Kinshasa suluhu ya tatizo hili la hali ngumu ya maisha,” anasema.

Suala la usafi katika sehemu za kula, hata hivyo halioneshi kutiliwa mkazo.

Dereva teksi, Bangamba anasema kuna baadhi ya wamiliki wa sehemu zinazouza chakula, wanatumia sahani na glasi zisizooshwa.

Wateja pia huwa hatarini kupata magojwa kama vile homa ya matumbo, kuharisha na hata kipindipindu kwa vile sehemu hizi nyingi zi katika mazingira machafu.

Miongoni mwa mazingira hayo machafu ni kuzingirwa na takataka pamoja na maji machafu yaliyotuama au kutiririka.

“Ugumu wa maisha unawafanya watu kula kile wanachoweza kumudu,” anasema Benjamin Kewngani Mavard, Mkuu wa Usafi wa Umma. Akionya kuwa kutakuwa na ongezeko la tatizo la afya kwa umma.

“Ni vigumu kuwafungia wauzaji chakula biashara zao. Hivyo wanapaswa kuzingatia usafi.”

Mama Marie anasema ijapokuwa wengine hawazingatii suala la usafi, sehemu yake yeye ni safi.

“Familia yangu na mimi mwenyewe tunakula kile ninachopika hapa,” anasema huku akiosha vyombo vyake

“Sitaki watu waugue. Nataka waje kwa siku ijayo kula kwangu na hivyo usafi ni moja ya vipaumbele vyangu,” anamalizia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles