27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

TATIZO LA MENO YA KAHAWIA LINATIBIKA – DAKTARI

Na MWANDISHI WETU,

FLUOROSIS ni mvurugiko maalumu katika mchakato wa utengenezwaji wa sehemu ngumu za meno (enamel). Mvurugiko huu husababisha mabadiliko katika muonekano, uimara na ubora wa meno yaliyoathirika. Fluorosis hutokea pale ambapo madini ya floraidi mengi kupita kiasi yanapojumuishwa kwenye meno wakati yanapokuwa yanatengenezwa mwilini. Kiwango cha floraidi kinachokubalika mwilini kwa afya kwa siku ni 0.05mg mpaka 0.07 mg F/Kg/day. Madhara na ukubwa wa tatizo la fluorosis una uhusiano wa moja kwa moja na jumla ya kiwango cha madini ya floraidi yaliyokuwa mwilini wakati wa kipindi cha utengenezwaji wa meno.

Vyanzo vikuu vya floraidi

Madini ya florini hupatikana kwenye sehemu mbalimbali, kama vile hewani, ardhini na kwenye maji. Floraidi iliyopo kwenye maji ndiyo chanzo kikubwa cha florini mwilini mwetu. Floraidi ambayo inaweza kusababisha fluorosis nchini mwetu hupatikana katika vitu vikuu vifuatavyo:

Maji

Kuna baadhi ya maeneo maji yanakuwa na kiwango kikubwa cha madini ya floraidi zaidi ya 1.5mg-F/l inayokubalika na Shirika la Afya Duniani (WHO). Nchini Tanzania sehemu za mikoa ya Arusha, Shinyanga, Mwanza, Mara na Singida ina maji yenye kiwango kikubwa cha floraidi (3.3 mg-F/l -24.9 mg-F/l). Mikoa hii inapatikana kwenye mkondo wa bonde la ufa.

Magadi (trona)

Baadhi ya magadi yanakuwa na kiwango kikubwa cha madini ya floraidi (29-9000 mg-F/l). Mfano magadi kutoka baadhi ya maeneo ya Kilimanjaro kama Rundugai na Sanya juu yana kiwango kikubwa cha floraidi, wakati maeneo mengine yanakuwa na kiwango kidogo cha floraidi kama Kahe. Baadhi ya maeneo ya Kilimanjaro wanapata ugonjwa wa meno kahawia kutokana na matumizi ya magadi na si maji yenye floraidi, maana utafiti umeonyesha maji ya maeneo hayo yana kiwango cha chini cha floraidi

Chakula

Vyakula vingi vina kiwango kidogo cha floraidi. Vyakula hivyo ni mboga za majani, samaki na nyama. Kiwango hiki ni cha chini kisicho na madhara kwa afya ya mtumiaji. Hata hivyo, iwapo chakula hichi kitatengenzwa na maji yenye kiwango kikubwa cha floraidi, basi huwa chanzo cha floraidi nyingi mwilini.

Uhifadhi wa floraidi mwilini

Floraidi kwa njia ya maji ya kunywa au chakula, hunyonywa haraka kutoka tumboni na kusafirishwa kwenye damu kuhifadhiwa kwenye mifupa na meno tu. Wingi wa floraidi mwilini, hupungua au kuongezeka, kulingana na eneo mtu analoishi kwa muda huo. Hupungua na kutolewa kwa njia ya mkojo, haja kubwa na jasho pale mtu anapoondoka eneo lenye madini hayo kwa wingi kwenye maji na vyakula na kuhamia sehemu yenye madini kidogo ya floraidi. Floraidi kwa njia ya hewa pia huingia mwilini ila ni kwa kiwango kidogo mno.

Kutokea kwa fluorosis (Pathogenesis)

Ugonjwa wa meno kahawia (dental fluorosis), unaweza kuonekana kwenye meno ya utoto au ya ukubwani. Hata hivyo, tafiti zinaonyesha kuwa meno ya ukubwa hupata tatizo hili zaidi kuliko meno ya utotoni. Hii ni kwa sababu wakati watoto wanazaliwa, utengenezwaji (mineralization) ya meno ya utotoni huwa umekamilika kwa kiasi kikubwa. Hivyo basi, floraidi inakuwa haina madhara makubwa kwenye meno haya. Lakini kwenye meno yale ya ukubwani ambayo mchakato wake wa utengenezwaji unakuwa ndiyo unaanza na unaendelea katika meno mengine huathirika iwapo kiwango cha floraidi kilichopo wakati huo ni kikubwa kulikoni kile kinachohitajika.

Umri muhimu ambao humfanya mtoto kuweza kupata tatizo hili ni miaka 0-6. Mtoto anapofikisha miaka 7-8, anakuwa hawezi kupata tatizo hili kwenye meno yake ya ukubwani kwa kuwa meno yake yote yanakuwa tayari yameshakamilika kujengeka na madini husika (ikiwamo floraidi), hata kama bado hayajaota/kutokelezea kinywani. Vile vile, tafiti zinaonyesha kwamba maziwa ya mama huwa na kiasi cha kawaida cha floraidi hata kama mama ana kiwango kikubwa cha floraidi mwilini mwake. Hivyo basi, maziwa ya mama si moja ya vyanzo vya fluorosis. Muonekano wa meno kahawia unategemeana na muda ambao muhusika amekuwa akitumia vitu vyenye madini ya floraidi kwa wingi.

Muonekano unaweza kuwa michirizi meupe mingi kwenye meno (mild dental fluorosis), rangi ya kahawia kwenye baadhi ya meno na vitundu vidogo vidogo (moderate dental fluorosis).

Rangi ya kahawia iliyokolea na kuharibika kwa sehemu ngumu ya nje ya jino na kubomoka pamoja na kuwa na vitundu vidogo vidogo (confluent enamel porosity).

Madini ya floraidi na dawa za meno

Hapo awali tumeona namna ambavyo madini ya floraidi yanavyoweza kusababisha fluorosis kipindi meno yanapotengenezwa (mineralization). Hata hivyo, kwenye meno ambayo tayari yameshatengenezwa na kukomaa, madini ya floraidi yana faida kubwa mno. Katika dawa hizi floraidi inakuwa ikifanya kazi pale pale kinywani; haijumuishwi kwenye utengenezaji wa jino kwa sababu jino linakuwa limeshatengenezwa.

Madini ya floraidi yanawekwa kwa makusudi katika dawa za meno. Madini haya huwekwa kwa kiwango kinachokubalika (1000-1500 ppm) kulingana na tafiti na miongozo ya WHO. Kiwango hiki cha madini ya floraidi ni nyenzo muhimu katika kuzuia ugonjwa wa kuoza kwa meno. Madini haya hufanya kazi zifuatazo:

1. Huongeza uimara wa meno na hivyo kuzuia yasitoboke (prevents demineralization).

2. Husaidia kujengeka kwa meno (encourages remineralization) katika hatua za mwanzo za ugonjwa wa kutoboka meno, hivyo kuzuia tatizo hilo lisiendelee.

3. Huzuia ufanyaji wa kazi wa kawaida(inhibits metabolism) wa seli za bakteria wanaosababisha kuoza kwa meno (S. Mutans, Lactobacillus spps).

Kinga

Kimsingi matumizi ya kiwango kinachokubalika kwa afya cha madini ya florini ndiyo kinga sahihi.

Maji

Kutumia maji yenye kiwango kinachotakiwa cha madini ya floraidi. Ifahamike kwamba maji haya hatuyatumii kwa ajili ya kunywa tu, bali pia pamoja na kupikia. Katika maeneo yenye madini mengi ya floraidi kwenye maji kuna jitihada mbalimbali zinazofanyika kupunguza kiwango cha madini haya ili maji yasilete madhara kwa watumiaji.

Hata hivyo, jitihada hizi zinapata changamoto za gharama za kitaalamu pamoja na kwamba maeneo mengi yanatumia vyanzo mbalimbali vya maji. Hata hivyo, kwenye familia zenye watoto wadogo wanaoishi kwenye maeneo yenye floraidi nyingi (endemic areas), matumizi ya maji ya kununua (bottled water) kwa ajili ya kunywa na kupikia chakula cha mtoto huweza kusaidia kupunguza madhara ya floraidi kwenye meno ya mtoto huyu.

Dawa ya meno

Watoto wasaidiwe kupiga mswaki na kiwango kidogo cha dawa yenye floraidi. Kiasi hichi kisizidi ukubwa wa punje ya njegere (pea-sized). Pamoja na hayo, matumizi ya dawa za meno maalumu kwa ajili ya watoto (children toothpaste) yanahimizwa. Dawa hizi zinakuwa na kiwango pungufu cha floraidi ili kupunguza uwezekano wa mtoto kupata fluorosis. Dawa hizi hupatikana kwa urahisi kwenye maduka mbalimbali hapa nchini.

Watoto wafundishwe kutema mara baada ya kuswaki na waendelee kutumia dawa za meno za watoto huku wakisaidiwa mpaka wanapofikia miaka sita.

Baada ya hapo waendelee kupiga mswaki chini ya uangalizi kwa kutumia dawa za meno za kawaida mpaka watakapoweza kujitegemea bila msaada (angalau miaka 12).

Magadi

Kutumia magadi yenye kiwango kidogo cha floraidi.

Matibabu

Walio wengi wenye meno yaliyopata rangi hii ya kahawia hupenda kubadili rangi ya meno yao kuwa meupe, kwa kutumia njia zinazohatarisha afya ya meno na kinywa. Wanatumia mkaa au mawe maalumu kusugua meno ili kuondoa hiyo yangi. Hii husababisha kuharibu sehemu ngumu ya jino inayoitwa enamel, hufanya meno kulika, kufa ganzi, kuwa dhaifu na hata kuvunjika. Kuna matibabu ya aina mbalimbali kwa ajili ya kubadili mwonekano wa meno ya aina hii. Mtu yeyote aliyepata madhara yatokanayo na fluorosis awaone wataalamu wa afya husika. Hii ni kwa sababu matibabu hutegemeana na kubadilika kulingana na hali ambayo mgonjwa atakuwa nayo.

Makala hii imeandaliwa na Dk. Kasusu Nyamuryekung’e (DDS, MPhil) akishirikiana na Dk. Deogratias Kilasara (DDS, MDent).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles