25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

RC Iringa awaombe radhi waandishi wa habari

NA MWANDISHI WETU

KWA siku mbili sasa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ali Hapi  amezua mjadala mzito wa kuwataka waandishi wa habari  koani humo kuhakikisha wananua vitambulisho vya wafanyabiashara ambavyo vimetolewa na Rais Dk. John Magufuli.

Uamuzi huo  unatokana na orodha ndefu ambayo imetolewa na Hapi ikijumuisha waandishi wa habari kuhakikisha wananua vitambulisho hivyo  wavitumie wakati wa kazi zao za kila siku.

Jambo hilo limezua mshangao mkubwa hadi kufikia hatua ya watu kujiuliza tangu lini waandishi wa habari wamekuwa wafanyabiashara ndogo ndogo katika nchi hii? 

 Ieleweke uandishi wa habari ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine ambazo zina misingi yake inayoisimamia. Katika hilo tunasema Hapi na jopo lake lote ambalo lilikaa chini na kukubaliana jambo hilo, wote kwa pamoja wameteleza. 

Ndiyo sababu tunakubaliana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuwa kauli hiyo insikitisha, inashangaza na inazua   maswali mengi kuliko majibu.

Tunaamini  chombo pekee chenye mamlaka ya kutoza kodi ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) – kama sheria inavyoanisha –  na si  mkuu wa mkoa.  

  Ifahamike waandishi wa habari hawana bidhaa wanazouza, bali wanafanya kazi zao kwa mujibu wa taaluma,   iweje watembee mitaani kila siku wamening’iza vitambulisho kama kwamba wanauza karanga!

Kama kila mmoja wetu anavyojua, kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 (MSA 2016) na kanuni zake za mwaka 2017, kinatambua taaluma ya uandishi wa habari na waandishi wa habari. Kazi za waandishi wa habari ni kukusanya, kuchakata, kuhariri na kuchapisha habari na taarifa na si kugawiwa vitambulisho vya wafanyabiashara.

Miaka nenda rudi, waandishi wa habari wamekuwa na utaratibu  mzuri  kwa kushirikiana na Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO)  ambako hupewa  vitambulisho vya kazi  (press cards) kwa kulipia ada ya Sh 30,000 kila mwaka, ikizingatiwa   utaratibu huo ulikuwako tangu Sheria ya Magazeti Na 3 ya mwaka 1976 ilipotungwa.

Tunamkumbusha Hapi na wenzake mkoani Iringa  kuwa uandishi wa habari ni muhimili wa nne wa dola, hivyo siyo vema kuushusha hadhi kwa kuugeuza kuwa ni kazi isiyo rasmi.  Si haki au busara hata kidogo kuwataka waandishi wa habari wa nchi hii, bila kujali maeneo yao ya  jiografia, katika kutimiza wajibu wao, wanunue vitambulisho vya watu wanaojishughulisha na sekta isiyo rasmi. 

Agizo la kuwaingiza waandishi wa habari kwenye orodha hiyo linaonyesha   kiongozi huyo ama anatindikiwa uelewa wa sheria za nchi au hakuomba ushauri wa  sheria au amejielekeza vibaya. Kama amejielekeza vibaya alipaswa kuwa mwepesi wa kukiri kosa kuliko kuendelea kushikilia msimamo wake huo. Katika hilo   amejikwaa na anapaswa kukaa chini na kujitafakari. 

Tunamkumbusha Hapi  kuwa waandishi wa habari wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria, na si kupitia maagizo na matamko. Tunasema kama mzigo wa vitambulisho umemuelemea basi atafute njia nyingine na si kutaka kuponea kwa wana habari.

Kwa sababu hiyo, tunakubaliana uamuzi wa  na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC) wa kumtaka Hapi kuwaomba msamaha ndani ya wiki moja kwa sababu anafanya nao kazi kila siku. Baada ya kufanya hivyo awaombe radhi waandishi nchi nzima kwa sababu amedhalilisha  kazi yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles