29.5 C
Dar es Salaam
Monday, May 13, 2024

Contact us: [email protected]

Quinine yasababisha mtoto kuzaliwa kiziwi

Young African American Woman Pregnant isolated on a black backgr

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

MATUMIZI yasiyo sahihi ya dawa zenye sumu kali ikiwamo Quinine inayotibu malaria imetajwa kuwa hatari kwa sababu huchangia kwa asilimia kubwa mtoto kuzaliwa akiwa na tatizo la usikivu (kiziwi).

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Masikio, Pua na Koo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Edwin Liyombo, alipozungumza na MTANZANIA Jumapili hospitalini hapo juzi kuhusu madhara yanayosababishwa na dawa.

Alisema hatari zaidi hujitokeza pale mjamzito anapotumia dawa hizo bila kufuata ushauri wa daktari hasa anapozidisha kipimo cha dozi anayopaswa kuitumia.

Dk. Liyombo alisema pamoja na Quinine dawa nyingine inayochangia mtoto kupatwa na tatizo hilo ni Gentamicin ambayo hutumika kutibu maradhi ya UTI.

“Wataalamu wa afya huwa tunawashauri akina mama kuhudhuria kliniki kila wakati na kufuata ule ushauri tunaowapa kwa sababu matumizi holela ya dawa zenye sumu ni hatari, anapozidisha dozi, sumu zile huenda moja kwa moja kuua seli zilizoko ndani ya sikio katika eneo la cochlea.

“Seli hizo zinapokufa, sikio hushindwa kupokea mawimbi ya sauti na kwa kuwa mawimbi ya sauti hayafiki kwenye cochlea ili yasafirishwe kwenda kwenye ubongo kupitia mshipa wa fahamu ulioko kichwani, mtu huyo anakuwa kiziwi,” alisema.

Dk. Liyombo alisema kwa kuwa sikio la mtoto mwenye tatizo hushindwa kupokea mawimbi ya sauti hivyo moja kwa moja hupatwa na tatizo la kuwa bubu.

“Kuwa bubu ni matokeo ya kutokusikia kile kinachozungumzwa. Katika hatua za ukuaji wa mtoto tunatarajia anapofikisha miezi minane au tisa anakuwa ameanza kusikia na kutamka baadhi ya maneno, mfano baba, mama, dada au kaka.

“Sasa wazazi wengi hawana elimu ya kutosha au wanapoona mtoto anachelewa kuongea wanadhani ni jambo la kawaida kumbe unakuta tayari kuna tatizo ndio maana wengi wanafikishwa hospitalini wakiwa wamechelewa,” alisema.

Pia alisema katika kliniki hiyo, idadi ya watoto wanaosumbuliwa na tatizo la usikivu imekuwa ikiongezeka kadiri miaka inavyozidi kusonga mbele.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles