24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

PLUIJM: TUTAKULA SAHANI MOJA NA YANGA

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

UONGOZI wa klabu ya Singida United na kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van der Pluijm, wametamba kushinda katika mchezo ujao dhidi ya Yanga utakaofanyika Uwanja wa Namfua, mjini Singida.

Mchezo huo utakuwa wa kwanza kupigwa kwenye uwanja huo tangu ligi msimu wa 2017/18 ilipoanza, ulikuwa ukifanyiwa ukarabati na utazinduliwa katika mchezo huo.

Akizungumza jana kocha huyo alisema mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa timu zote mbili, mbali na ubora wa timu hizo, Singida itakuwa ikiutumia uwanja huo kwa mara ya kwanza mbele ya mashabiki wake.

“Naifahamu Yanga, nimeifundisha, nimesajili nawafahamu wachezaji asilimia 80 uzuri na ubaya wao, sina wasiwasi kabisa na mchezo huo,” alisema Pluijm.

Alisema wachezaji wake na Yanga hawatofautiani kwa kila kitu, kuanzia uwezo na na mambo mengine ambayo hakutaka kuyaweka wazi.

Katika mchezo uliopita Singida dhidi ya Mtibwa Sugar ilitoka suluhu kwenye Uwanja wa Manungu mjini Morogoro, ambapo kwa sasa wanashika nafasi ya tano ikijikusanyia pointi 13, ambapo imeshinda mara tatu na kupata sare nne huku ikipoteza mchezo mmoja.

Singida United ilifanikiwa kupanda ligi kuu msimu huu ikiwa ni pamoja na Lipuli FC na Njombe Mji.

Mchezo huo utakuwa wa kukata na shoka kutokana na baadhi ya wachezaji wanaokipiga katika timu hiyo, Deus Kaseke pamoja na Nizar Khalifan, walishawahi kuichezea Yanga kwa misimu tofauti ikiwa ni pamoja na kocha wa zamani wa Wanajangwani hao ambaye kwa sasa anainoa timu hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, katibu mkuu wa klabu hiyo, Abdulrahman Sima, alisema wanahitaji kuanza na ushindi wa kishindo kwenye mchezo huo, ili kuwapa zawadi mashabiki wao kwa sababu hiyo itakuwa ni mechi ya kwanza kuutumia Uwanja wa Namfua.

“Baada ya kumaliza mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar kesho (leo), tunarejea nyumbani Singida kwa ajili ya maandalizi ya mchezo unaofuata dhidi ya Yanga, hivyo lazima tujipange vema,” alisema.

Alisema anafahamu watakutana na mabingwa watetezi, lakini watahakikisha wanapambana na kupata ushindi kwenye mchezo huo.

Upande wao mabingwa watetezi, Yanga, wanatarajiwa kuwafuata Singida United, Alhamisi ikiwa na kikosi kamili isipokuwa wachezaji; Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe na Donald Ngoma ambao ni majeruhi, ikiwa ni pamoja na Juma Abdul ambaye ana kadi tatu za njano.

Wanajangwani hao walianza jana mazoezi kwenye Uwanja wa Uhuru ikiwa ni miongoni mwa maandalizi ya mchezo huo, baada ya mechi iliyopita kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Yanga wanahitaji ushindi baada ya kuambulia sare ili kuendelea kujikita katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi na kuendeleza mbio za ubingwa msimu huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles