23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Paul Biya kushinda urais wa Cameroon leo?

YAOUNDE, CAMEROON

Wananchi wa Cameroon wanatarajia kupiga kura kumchagua rais wao mpya leo katika uchaguzi mkuu nchini humo, huku hali ya wasiwasi inaendelea kutanda katika maeneo yanayozungumza lugha ya Kiingereza, Kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za habari kutoka nchini humo, zinasema hadi sasa haijafahamika ikiwa wakazi wa maeneo hayo watashiriki uchaguzi au la.

Wakati huo huo Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi wa urais katika mazingira ya amani, uwazi, haki na umoja.

Katika taarifa yake iliyotumwa nchini humo, Guterres amesema kuwa raia wa Cameroon wanatakiwa kutekeleza haki yao ya kidemokrasia na kuwataka wadau wote husika na mchakato wa uchaguzi kujizuia na vurugu, kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Amewashauri Pia wagombea wote kutatua tatizo lolote lililohusiana na mchakato wa uchaguzi kupitia njia za kisheria na za kikatiba.

Hivi karibuni Naibu msemaji wake Farhan Haq alithibitisha kwamba Umoja wa Mataifa umekumbwa na wasiwasi kutokana na hali inayoendelea katika majimbo yanayozungumza lugha ya Kingereza nchini Cameroon na madhara ya matukio hayo katika kipindi hiki kuelekea katika uchaguzi mkuu.

Uchaguzi mkuu unaofanyika leo utahusisha wagombea tisa akiwemo rais anayemaliza muda wake Paul Biya watachuana kuwania nafasi ya urais katika mazingira ya kuendelea kudhoofika kwa usalama kaskazini mwa nchi hiyo kufuatia mashambulizi ya kundi la kigaidi  la Boko Haram pamoja na mzozo wa kijeshi unaoendelea katika maeneo yanayozungumza lugha ya kingereza wanaodai mjitengo.

Wakati huo, wagombea wawili wa upinzani nchini humo wamekubaliana kuungana siku moja tu kabla ya nchi hiyo kufanya uchaguzi mkuu wa urais.

Taarifa hiyo imethibitisha uvumi uliokuwepo wa vyama vya upinzani kuungana kujaribu kumuangusha rais Paul Biya, lakini muungano huu hautamjumuisha kinara wa upinzani kutoka chama cha Social Democratic Front, Joshua Osih.

Akere Muna kiongozi wa chama cha People’s Development Front FDP ametangaza kukubali kumuunga mkono mgombea mwenzake Maurice Kamto wa chama cha Movement for the Rebirth of Cameroon (MRC).

Juzi, chama cha MRC kilitoa madai kuwa tayari mpango mkubwa wa udanganyifu wa kura unafanyika kuhakikisha rais aliyeko madarakani anashinda, madai ambayo hata hivyo yamekanushwa na tume ya uchaguzi.

Mwenyekiti wa timu ya kampeni ya mgombea Maurice Kamto, Paul-Eric Kingue amesema tayari udanganyifu uliopangwa kufanyika leo umepewa baraka na maofisa wa tume ya uchaguzi.

“Hatutakubali matokeo yoyote ikiwa udanganyifu huu utaendelea,” amesema Kamto wakati wa mkutano wake na wanahabari mjini Yaounde.

Mamlaka nchini Cameroon mara zote zimekuwa zikishutumiwa kwa kumpendelea Biya ili asalie madarakani. Rais Biya alishinda kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2011 kwa asilimia 78 ya kura, uchaguzi ambao ulikashifiwa vikali na upinzani pamoja na waangalizi wa kimataifa.

Uchaguzi huo unafanyika katika hali ya machafuko kwenye majimbo yanayozungumza kiingereza nchini humo huku watu kadhaa wakiripotiwa kufariki dunia huku kukiwa na vuguvu la kutaka maeneo hayo kutaka kujitenga.

Kwa mujibu wa maofisa usalama nchini humo wamesema watu kadhaa wameuawa kwenye mji wa Kumba kati ya siku ya Jumatano na Ijumaa wakati wa makabiliano na vyombo vya usalama.

Kwa mujibu wa tangazo la ikulu ya nchi hiyo mipaka ya taifa hilo lenye watu takribani milioni 24 itafungwa kuanzia leo ili kuweka usalama katika zoezi la uchaguzi mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles