Imechapishwa: Tue, Oct 3rd, 2017

OLE NASHA: SERIKALI HAIJAGAWA SALFA FEKI

Na Mwandishi Wetu


KUNA dalili zote kuwa migogoro kwenye uagizaji wa pembejeo za mazao mbalimbali nchini ni za kutungwa na wengi wanaoshindwa kupata zabuni, kwani hununa na kusema ovyo na hiyo imekuwa wazi zaidi kwenye zao la korosho lililopanda chati na umaarufu lakini lililokuwa linaonewa kwa mengi.

Baada ya kufanikiwa kupata bei nzuri ya korosho mwaka jana kutokana na ubora wa  zao hilo na mipango mizuri ya ununuzi kutoka kwa Serikali na wakulima, kumezuka sintofahamu nyingi mwaka huu ikiwamo ya dawa ya salfa  ambayo ni muhimu sana kwa zao hilo na ni mhimili.

Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ikishirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), imeagiza tani 17,100 za dawa aina ya salfa kwa ajili ya kupulizia mikorosho.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, alipoelezea utekelezaji wa wizara yake wakati wa kilele cha maonyesho ya Siku ya Wakulima ‘Nane Nane’ yaliyofanyika kitaifa mjini Lindi.

Dk. Tizeba alisema tayari tani 12,700 zimeshawasili hapa nchini na kuanza kuzigawa kwa vyama mbalimbali vya msingi na ushirika chini ya usimamizi wa wakuu wa wilaya husika tayari kusambazwa maeneo mbalimbali kwa ajili ya kilimo.

Alisema tani 2,100 zimesambazwa kwenye mikoa inayolima korosho huku tani nyingine 2,300 zikitarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kuanzia Agosti 20, na aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya zinazolima zao hilo kusambaza dawa hizo kwa wakulima wanaounda ushirika.

Waziri huyo alisema hali hiyo imetokana na uongozi wa Bodi ya Korosho (CBT) kuishauri Serikali kugawa dawa hiyo kwa wakulima wa korosho ili kuongeza uzalishaji kwa kuwa wengi wanashindwa kupulizia dawa hiyo ipasavyo kwa kukosa uwezo wa kulipia nusu ya gharama kupitia Mfuko wa Wakfu wa Korosho.

 

Malipyoto wazua jambo

Kutokana na Serikali ya mkoa kuwa karibu na wakulima na kushughulikia masuala ya matatizo yao kwa karibu zaidi walanguzi mkoani Mtwara na Lindi, wamepata pigo kubwa na hivyo kubuni maovu na kwa njama zao wamezusha mengi kuhusu dawa ya salfa inayogawiwa wakulima kwa kudai kuwa haifai (feki) na au imepitwa na wakati.

 

Hakuna salfa feki iliyosambazwa

Akiwa Bungeni, Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, William Ole Nasha, alisema hakuna salfa feki wala iliyopitwa na wakati iliyosambazwa kwa wakulima wa korosho hapa nchini msimu huu.

Nasha aliitoa kauli hiyo Bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Lathifa Hassan Chande (CCM).

Lathifa alitaka kujua Serikali inadhibiti vipi salfa feki ambayo ilipenya na kuingia nchini na kuwafikia wakulima wa zao hilo. Ole Nasha alisema, hakuna salfa feki au iliyopitwa na wakati iliyosambazwa kwa wakulima, kilichotokea ni kuwepo kwa salfa iliyopitwa  muda wake kwenye ghala lakini haikuwa kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima ila kuharibiwa au kupelekwa Kituo cha Utafiti Naliendele kwa ajili ya kutolea mafunzo na si vinginevyo.

Na alipotakiwa na gazeti hili kutoa uthabiti wa kauli yake, Ole Nasha alikuwa imara na kutoa angalizo kwa mtu yeyote aliye na ushahidi vinginevyo aulete hadharani ili kuthibitisha ubovu wa dawa hiyo na jaribio la kutaka kuingizwa kwenye soko kwa kugawia wakulima.

Awali kwenye Bunge akijibu swali la msingi la Lathifa, Ole Nasha alisema ushirikishaji wa wakulima na wadau wa korosho katika upangaji wa bei ya korosho na mjengeko wa bei, ni kwa mujibu wa sheria ya korosho ya mwaka 2009 na kurudia kuwa hakuna salfa feki wala iliyopitwa na wakati iliyosambazwa kwa wakulima wa korosho hapa nchini.

MTANZANIA lilipotaka kujua zaidi, alisema kwenye ghala moja kulikuwa na mabaki ya salfa (stoku) ya zamani ya dawa ya salfa na kwa vile alikuwa nje ya ofisi hakumbuki sawasawa kiasi chake, lakini thamani yake ilikuwa haizidi shilingi milioni 9 kwani salfa iko ya aina mbili ya maji na ya unga.

Kwa mara ya kwanza mwaka jana zao la korosho lilipata bei nzuri sana kwenye soko la ndani na la nje kwa wastani wa bei ya kutoka shilingi 3,000 hadi 3500 kwa kilo ikiwa ni mara tatu ya bei yake ya kawaida ya shilingi 1,000 kwa kilo.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

OLE NASHA: SERIKALI HAIJAGAWA SALFA FEKI