27.2 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

TRA YAONGEZA JUHUDI KUKAMATA WALA RUSHWA, WAVUNJA MAADAILI 

Na KOKU DAVID


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikiendeleza mikakati  mbalimbali iliyoiweka ili kufanikisha malengo yake katikaa suala la ukusanyaji wa kodi.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuwafukuza kazi watumishi watakaobainika kukiuka maadili ya kazi ikiwa ni pamoja na kupokea rushwa.

Sambamba na kuwafukuza kazi watumishi wasiokuwa na maadili kazini, pia huwahamisha baadhi ya watumishi ambao hukaa kwa muda mrefu katika kituo cha kazi ili kuepusha ukiukaji wa maadili unaoweza kufanyika kutokana na mazoea na kuzoeana.

Mamlaka hiyo ambayo imepewa jukumu la kukusanya kodi kwa mujibu wa sheria, kupitia Idara ya Maadili ya Watumishi hufanya upelelezi ili kubaini watumishi ambao hukiuka maadili ya kazi na kwamba wanaobainika huwaondoa kazini.

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Gerald Mwanilwa anasema TRA imekuwa ikiwachukulia hatua za kisheria watumishi wanaokiuka maadili ya kazi kama ambavyo sheria za kazi zinavyosema.

Anasema TRA kupitia idara ya Maadili ya Watumishi imekuwa ikifanya upelelezi kwa lengo la kuwabaini watumishi wanaokiuka maadili ya kazi au wala rushwa ili kuwachukulia hatua.

Anasema rushwa ni jambo linalofanyika kwa siri na kwamba ili kulibaini ni lazima ziwekwe mbinu zitakazowezesha kuwakamata  wahusika ikiwa ni pamoja na kusaidia kuidhibiti.

Anasema utendaji kazi wa TRA ya serikali ya awamu ya tano ni tofauti na ile ya miaka ya nyuma na kwamba utendaji wake wa kazi unafuata maadili.

Anasema msimamo wa TRA ya sasa ni kufanya kazi kwa kufuata maadili ambayo yatawezesha kufikia malengo katika ukusanyaji wa mapato.

Mwanilwa anasema kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikiwawafukuza kazi baadhi ya watumishi ambao hubainika kukiuka maadili ya utumishi.

Anaongeza kuwa sambamba na kuwafukuza pia huwahamisha vituo vya kazi watumishi ambao hukaa kwa muda mrefu katika kituo kimoja cha kazi ili kuepuka ukiukaji wa maadili.

Anasema katika ukusanyaji mapato suala la rushwa limedhibitiwa kwa kiwango kikubwa na kwamba katika serikali hii wameanza vita dhidi ya rushwa.

Anasema uadilifu kazini ndio msingi wa mafanikio ya kufikia malengo na kwamba kila mtumishi wa mamlaka ya mapato anatakiwa kuwa mwadilifu.

Anasema sambamba na uadilifu, ushirikiano kazini ni njia mojawapo inayoifanya TRA kufanikiwa kufikia malengo yake katika suala la ukusanyaji wa mapato.

Mwanilwa anasema pia elimu ya kuwajengea uwezo wa kazi inayotolewa mara kwa mara kwa watumishi wa mamlaka hiyo pia inachangia mafanikio.

Anasema TRA imeweka utaratibu wa kutoa elimu ya kuwajengea uwezo watumishi wake wapya ambao baada ya kazi ofisini hupelekwa darasani kwaajili ya kupata mafunzo zaidi na kwamba mafunzo hayo hutolewa na wataalamu wa kodi kutoka katika Chuo cha Kodi(ITA) kilichopo Mikocheni

jijini Dar es Salaam.

Anasema katika mafunzo hayo hufundishwa masuala mbalimbali ya kodi pamoja na uboreshaji wa utendaji kazi hasa katika mbinu za uchunguzi, kuboresha ujuzi wa namna ya kuchunguza ikiwa ni pamoja na kupigana vita dhidi ya wakwepa kodi.

Anasema wakwepa kodi wakipungua itasaidia nchi kupata maendeleo na kwamba kwa wananchi wanatakiwa kuwa wazalendo kwa nchi yao kuhakikisha kila mwenye kipato analipa kodi kwa hiyari kuepuka kuchukuliwa hatua.

Anaongeza kuwa pamoja na walipakodi, watumishi wa TRA  wanatakiwa kuwa waadilifu kazini ili kuiwezesha mamlaka hiyo kuweza kufanikisha malengo yake iliyojiwekea ambayo yataisaidia serikali kutekeleza majukumu yake ya kufanya maendeleo kwa wananchi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles