25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ngoma ampagawisha pluijm

DONALD NGOMANA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, amekunwa na bao alilofunga mshambuliaji, Donald Ngoma, wakati timu hiyo ilipolazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) juzi.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ilishuhudiwa Ngoma akifunga bao hilo dakika ya 45 kwa mpira wa kubetua aliopiga baada ya kupokea krosi safi ya juu kutoka kwa beki wa kulia, Juma Abdul na kutuliza vyema kifuani kabla ya kufunga.

Azam waliocheza vizuri kipindi cha pili walisawazisha bao hilo dakika ya 82 kupitia kwa mshambuliaji wao, Kipre Tchetche, aliyeingia kuchukua nafasi ya Mkenya, Allan Wanga.

Yanga walishindwa kufunga penalti iliyoonekana kuwa na utata waliyopewa na mwamuzi, Abdallah Kambuzi kutoka Shinyanga baada ya kipa wa Azam, Aishi Manula kugongana na winga, Simon Msuva, lakini kiungo Thabani Kamusoko alikosa na kupanguliwa na kipa huyo.

Akizungumza na MTANZANIA mara baada ya mchezo huo, Pluijm alisema Ngoma alifunga bao zuri sana na ameonyesha thamani yake iliyomfanya apendekezwe Yanga na kusajiliwa.

“Bao zuri sana, ukiona namna alivyoipokea ile krosi, alivyotuliza mpira na kufunga, inatosha kudhihirisha ubora wa bao lile. Nilimpendekeza asajiliwe na ameonyesha thamani yake kwanini yupo Yanga,” alisema.

Kwa bao hilo Ngoma amefikisha mabao matano sawa na mshambuliaji wa Simba, Hamis Kiiza, wakiwa wamezidiwa bao moja na Elias Maguli wa Stand United ya Shinyanga mwenye mabao sita.

Akizungumzia mechi hiyo kwa ujumla, Mholanzi huyo alisema bao walilofungwa na Azam lilitokana na makosa ya mabeki wake walioshindwa kumkaba mfungaji huku akidai walitakiwa kuwa makini muda wote wa mchezo.

“Nilitarajia mechi ngumu na ndivyo ilivyokuwa, Azam walicheza kwa kutumia nguvu kuliko sisi na hilo ndilo tatizo lililotukabili. Kama unapata penalti dakika tano za mwisho na ukashindwa kufunga ni tatizo pia,” alisema.
Sare hiyo inaifanya Yanga kushindwa kuifunga Azam ndani ya dakika 450 sawa na mechi tano za ligi, mara ya mwisho Wanajangwani hao kuifunga ilikuwa ni Februari 23 mwaka juzi walipoichapa 1-0.

Yanga ambayo imeendelea kukaa kileleni kwa pointi 16 sawa na Azam FC kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, itashuka tena kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam keshokutwa ikiikaribisha Toto Africans ya Mwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles