24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 30, 2023

Contact us: [email protected]

Dk. Magufuli arusha kombora Ukawa

g6NA BAKARI KIMWANGA, GEITA

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema mabadiliko ya kweli hayawezi kuletwa kwa kuzungusha mikono, bali yatakuja kwa kufanya kazi.

Kutokana na hali hiyo, amesema yeye ndiye anayeweza kuleta mabadiliko ya kweli yanayokwenda na vitendo katika kujenga uchumi wa nchi na watu wake.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti, alipokuwa akizungumza wakati wa  mikutano ya kampeni iliyofanyika katika majimbo ya Buchosa, Geita na Busanda.

Katika mazungumzo yake, Mgufuli aliwataka Watanzania wasidanganywe na baadhi ya wanasiasa wanaowataka wasiipigie kura CCM.

Alisema kwamba, pamoja na baadhi ya wanasiasa kukesha wakihamasisha mabadiliko kwa kutoichagua CCM, jambo hilo halitawezekana kwa kuwa ni sawa na ndoto za mchana.

“Ninasema hapa, eti kuna watu wanahangaika kuzungusha mikono na kusema wanaleta mabadiliko, ni lazima wajue mabadiliko hayawezi kuja kwa mtindo huo.

“China hivi sasa inatisha kwa kuwa na uchumi wa daraja la kwanza duniani na kuna hatari hata ya kutaka kuizidi Marekani.

“Kwa mfumo wao huo, hawakukiondoa madarakani chama tawala ila walifanya mabadiliko ya ndani ya chama na Serikali.

“Ndiyo maana Magufuli ninakuja na mabadiliko ya kwenda ndani ya Serikali na ndani ya CCM. Katika hili, sina mchezo ndugu zangu Watanzania, naomba mniamini,” alisema Dk. Magufuli.

Kwa kuwa Watanzania wameshaamua kumpa urais Oktoba 25, mwaka huu, jambo atakalo anza nalo ni kuunda mahakama ya mafisadi.

Alisema, amezaliwa katika familia maskini na hatakuwa tayari kuona wajasiriamali wadogo wakinyanyaswa na hata kutozwa ushuru ambao umekuwa ukiwakandamiza katika biashara zao.

Alisema anajua eneo la Nkome ni maarufu kwa kilimo cha mananasi daraja la kwanza, lakini bado wakulima wamekuwa wakikosa soko la uhakika.

Kutokana na hali hiyo, atatimiza mkakati wa Serikali yake kwa kujenga kiwanda cha juisi katika  eneo hilo.

“Ni aibu kwa nchi yetu inayozalisha matunda kwa wingi, kukosa kiwanda cha kusindika matunda.

“Napenda kuahidi hapa, nitajenga kiwanda cha juisi kitakachosaidia wakulima wa mananasi kuwa na soko la uhakika badala ya kwenda Geita mjini au Mwanza.

“Tukijenga kiwanda hapa, tutatoa ajira kwa vijana na tutatengeneza juisi yetu badala ya kila siku kuagiza kutoka nje ya nchi, hii ni aibu,” alisema.

Vita ya Tizeba

Dk. Magufuli aligusia mgogoro wa kifamilia uliopo kati ya mgombea ubunge wa Jimbo la Buchosa, Dk. Charles Tizeba, anayepigwa vita na wapinzani wake wakishirikiana na kaka yake wa kuzaliwa.

Alisema anatambua kazi inayofanywa na Dk. Tizeba, hivyo aliwaomba wananchi wa jimbo hilo wamchague kwa kura nyingi.

“Jamani mti wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe maana hapa Buchosa eti Tizeba anapigwa vita na watu tena hata ndugu yake wa kuzaliwa naye,” alisema.

Azuru kaburi la babu yake

Akiwa njiani kuelekea katika mkutano wa kampeni katika Jimbo la Geita Vijijini, Dk. Magufuli alilazimika kwenda katika Kijiji cha Katoma na kuzuru kaburi la babu yake mzaa baba, Marco Nyahinga, aliyefariki akiwa na miaka 103.

Katika makaburi hayo, alitembelea pia kaburi la bibi yake mzaa baba, Anastazia Nuhi.

Akizungumza katika makaburi hayo, baba mdogo wa Dk. Magufuli, Simon Marco, alisema familia imefarijika kwa ujio wa mtoto wao huyo na kwamba Mungu atamsaidia ili ashinde.

“Tunafurahi sana mtoto wetu amekuwa na kazi kubwa ya kuomba kura kwa Watanzania, nasi tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu ili ashinde,” alisema.

Kwa upande wake Dk. Magufuli alisema anajua asili yake kwani babu yake mzee Marco aliwapenda watu wote wakiwemo majirani zake, jambo ambalo limemsaidia naye kufuata nyayo hizo.

“Hapa Katoma ndipo asili yangu na kitovu changu kilipo, ndipo babu na baba zangu walipolala, baba yangu maisha yake yote yalikuwa hapa Katoma kabla hajahamia Chato,” alisema Dk. Magufuli.

Wakati huo huo, Dk. Magufuli alipowasili katika uwanja wa Shule ya Msingi Ihumilo kwa ajili ya mkutano wa hadhara, alikataa kiti cha mapambo alichopangiwa na badala yake alikalia kiti cha plastiki.

Kutokana na hali hiyo iliwalazimu wasaidizi wake kupanga viti vya kawaida katika jukwaa na kuvitoa viti maalumu vya mapambo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,285FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles