24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

NETIBOLI IMELALA, IAMSHWE

Na GRACE HOKA- DAR ES SALAAM

KUNA michezo ambayo ukiitazama mara mbili unajiuliza ni kwanini imefikia katika hatua hii. Unaweza kujiuliza maswali mengi juu ya michezo mbalimbali, lakini chozi linaweza kukutoka juu ya mpira wa pete, netiboli.

Unaweza kubaki kujifungia kujihoji wewe mwenyewe juu ya Anna Kibira amekosea wapi? Mbona mtu huyu ni jembe na anajua mengi juu ya mchezo huu? Kwanini netiboli imefika hapa ilipo?

Lakini lawama zinapaswa kutupwa kwa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) au wadau wote tunahusika? Kibira anapaswa kubeba lawama? Swali hili ndilo linalokufanya ukubali mchezo huu unahitaji kupepewa. Usharogwa!

Unaukumbuka Uwanja wa Relwe Gerezani pale Kariakoo? Mashabiki wengi kwa sasa wanaisikia Uhamiaji au Uchukuzi, lakini Bandari, Posta, Reli, Jeshi Stars, JKT Mbweni, Kurugenzi Dodoma, CDA, Akiba zipo wapi?

Siyo hizo hizo tu lazima ujue juu ya timu nyingine kali kama Bora, Bima, Tanesco, Mapinduzi Dodoma, Muhimbili, Bohari Kuu, Madawa, NBC na nyinginezo ambazo zilikufanya hata kwenda kuripoti michuano inayofanyika pale Relwe Gerezani, ‘uwe na amani moyoni’.

Ila zote hizo ukitazama utabaini ni timu zilizokuwa chini ya taasisi za Serikali au mashirika ya umma. Chaneta wao kwa kulewa sifa, wakawa wanagonga mvinyo na kujisifu kwamba mchezo upo juu.

Wengi wanadai mchezo huu ulianza kupoteza umaarufu kabisa mwanzoni mwa miaka ya 2000, lakini ukweli ulishaingia kaburini toka mwishoni mwa miaka ya ’90.

Unaweza ukaja na takwimu za miaka ya karibuni kufanikiwa kuwa moja kati ya nchi bora duniani katika mchezo huo, lakini hizo ‘data’ wala zisikufanye ‘ujisikie raha na amani’, ila kubali netiboli ilishapotea njia.

Kweli Tanzania ilifanikiwa kupanda toka nafasi ya 19 mpaka ya 17 ikiwa ya nne barani Afrika na kuziacha nchi maarufu kama Ireland, Singapore, Malaysia, Uswisi, Namibia, Zambia, Sri Lanka na Marekani, lakini kwangu hicho si kigezo.

Kutokana na Chaneta kutojipanga, huku ikijua mashirika ya umma na taasisi hizo za Serikali zipo tu, umaarufu wa netiboli ulishuka miaka ya ‘90 kutokana na mfumo wa uchumi huru, ambapo mashirika mengi yalibinafsishwa na hata yaliyobaki hayakutoa tena kipaumbele kwenye michezo.

Chaneta walipokumbuka mvinyo umechacha, wakaamua kuipigania timu ya taifa, Taifa Queens, ambayo kweli ikafanya vyema katika mashindano ya kimataifa yaliyofanyika mwaka 2010 nchini Singapore ambapo katika mchezo wa fainali walifanikiwa kushinda dhidi ya wenyeji kwa 52-36.

Mchezaji Mwanaidi Hassan, akaonekana kama anataka kumrithi Grace Daudi ‘Sister’, lakini ‘wenye akili’ walijua tu Chaneta bado haijajipanga.

Wala huwezi kupinga kile walichofanya pia mwaka 2011 kwa kushiriki kwa mafanikio katika mashindano ya All African Games yaliyofanyika Maputo Msumbiji, kwa kutwaa medali ya shaba nyuma ya Uganda ambao walitwaa medali ya dhahabu.

Ila lazima tukubali Chaneta ilijisahau kwa kiasi kikubwa na kuufanya mchezo huu ujikute ukiingia kaburini ukisubiri kufukiwa tu.

Hakuna hata kiongozi mmoja ndani ya Chaneta kuanzia waliopita mpaka wa sasa wanaoweza kukwepa lawama kwa kile ambacho kimeukuta mchezo huu. Kwanini akwepe lawama?

Siwezi kumsifu kiongozi wa Chaneta aliyekuwepo kipindi hicho enzi za Bandari, Posta au Jeshi Stars eti alifanikiwa kuuweka mchezo huu juu. Hapana, wao pia walikuwa chanzo cha kuudidimiza.

Siwezi kumsifu kiongozi aliyepita hapa kati au hata wa sasa kwamba amepambana kuisaidia netiboli kutoka pale ilipo, hapana, nao wanahusika katika kuufanya mchezo huu upoteze mwelekeo.

Viongozi waliopita kwa kukosa dira, wakabaki kutegemea timu za mashirika ya umma au taasisi za Serikali, wakashindwa kuupeleka mchezo huu kwa wananchi, ambao wakabaki wakifanywa kama mashabiki.

Wakabaki kuzitegemea shule zifanye zenyewe zinavyojua jinsi ya kuuendeleza mchezo huu, huku mashabiki wanaume waliokuwa wakijitokeza wakifurahi kwa sababu ya vivazi tu vya wachezaji.

Viongozi wa kati na hata wa sasa wakakosa maono na kubaki kulalamika, huku wakiwashutumu viongozi wa vyama vya mikoa au wilaya kwa kushindwa kuusongesha mbele mchezo huu.

Nafasi ipo, ipo sana na bado mchezo huu unaweza kutoka hapa ulipo, lakini badala ya kuanza kulalamika ni lazima zichukuliwe hatua stahiki kuanzia sasa.

Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alijaribu kuleta mpaka kocha, lakini akapigwa zengwe mwanzo mwisho mpaka akaamua kujiondokea zake, ila Serikali bado isichoke kuwashika mkono Chaneta.

Ila viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika leo nao wawe na maono badala ya kutaka kuongoza kwa mazoea.

 

Tutafika tu!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles