25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

NAPE: VYOMBO VYA HABARI VILIUNGANISHE TAIFA

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amesema ili kushinda mapambano ya dawa za kulevya, lazima kila mwananchi ashiriki na vyombo vya habari viliunganishe Taifa.

Nape alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani ambayo huadhimishwa Februari 13 ya kila mwaka.

Alisema Taifa linaweza kushinda vita hiyo iliyoanzishwa na Rais Dk. John Magufuli ikiwa kila mtu atamuunga mkono.

“Tuna vita kubwa ya dawa za kulevya, vyombo vyetu vyote vya habari ni lazima viunganishe wananchi wote, sisi tunao uwezo wa kuunganisha Taifa kushinda mapambano ya dawa za kulevya.

“Hii ni vita ya watu wote, si ya mtu mmoja, tumuunge mkono Rais katika mapambano haya na sisi wanahabari tusibaki nyuma kwa sababu tunayo nguvu kubwa ya kuwafanya watu wote kufahamu madhara ya dawa za kulevya katika jamii,” alisema.

Aidha Nape alisema umefika wakati kwa watendaji wa redio kuangalia nafasi ya vyombo hivyo katika wakati huu wa mapinduzi ya teknolojia ambao watu hurekodi matukio na kuyatuma mitandaoni jambo linalohatarisha utendaji wa vyombo hivyo.

Alisema katika kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi katika mazingira rafiki, wizara yake inaendelea kupitia sheria mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwawezesha maofisa habari kutoa habari kwa waandishi tofauti na ilivyo sasa.

“Maofisa habari wa halmashauri wanapofuatwa na waandishi wanakimbia, ni kwa sababu hawashiriki katika vikao vya maamuzi.

“Tumeanza mchakato kuanzia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari – Maelezo awe na uwezo wa kutoa habari yeye mwenyewe, lakini hata maofisa habari wataanza kushiriki katika vikao vya maamuzi, kama hawashiriki ni lazima wawakimbie waandishi,” alisema.

Aliwakata waandishi wa habari na wadau wengine wa tasnia hiyo kupeleka malalamiko yao wizarani kwake ikiwa watabaini kuwapo kwa sheria inayokwamisha utendaji na kukwamisha upatikanaji wa taarifa.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk. Ayub Rioba, alisema wana jukumu la kuhakikisha wanaendelea kuwaunganisha wananchi kuwaelimisha na si kuwatenganisha sambamba na kuwaburudisha na si kuwakarahisha.

“TBC inapaswa kuendelea kuwa kubwa kwa sababu ni kubwa tangu wakati wa ukoloni na ilisaidia kwa kiasi kikubwa kulifanya bara la Afrika kuwa huru, hivyo iendelee kuwaunganisha watu wote,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles