23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

MWANAFUNZI AFARIKI, WALIMU WAOMBA KUZUIA MAPEPO

Na RAPHAEL OKELLO – BUNDA


MWANAFUNZI wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Bunda mkoani Mara, Jane Wilbert, amefariki dunia usiku wa kuamkia Jumatano katika bweni la shule hiyo.

Kwa mujibu wa wanafunzi wenzake, Jumatano asubuhi walipoamka kwa ajili ya maandalizi ya kuingia darasani, Jane, alichelewa kuamka na walipojaribu kumwamsha hakuamka ndipo walipogundua kuwa amefariki na kutoa taarifa kwa uongozi wa shule.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bunda, Machotta Kora, alisema mwanafunzi huyo alifariki wakati akiwa njiani kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda kupatiwa matibabu.

“Taarifa ya Jane kujisikia mgonjwa tuliipata usiku huo, mimi na patroni tulifika bwenini usiku huo na alichotuambia ni kwamba anajihisi mchovu, tulimpa huduma zinazostahili na kwa hali aliyokuwa nayo tulikubaliana tumpeleke hospitali asubuhi yake, ingawa pia tulikuwa na shida ya usafiri.

“Asubuhi tulipofika pale alizidi kuwa mchovu na tukiwa njiani kwenda hospitalini, Jane aliaga dunia, bado uchunguzi unafanyika na madaktari ili kujua alikuwa anasumbuliwa na tatizo gani,” alisema.

Machota alisema mwili wa marehemu ulitarajiwa kusafirishwa jana (Ijumaa) kwenda Moshi, Kilimanjaro kwa mazishi.

Kifo cha mwanafunzi huyo kinatokea ikiwa ni siku chache baada ya Kora kuiomba Serikali kuisaidia shule yake gari kwa ajili ya usafiri wa kwenda hospitali.

Katika hatua nyingine, walimu na wanafunzi katika Shule ya Sekondari  Makongoro iliyopo Kata ya Nyamswa wilayani Bunda, wameendesha ibada ya maombi kuzuia wanafunzi wa kike 70  kupagawa, kuanguka na kupoteza fahamu.

Maombi hayo yalifanyika juzi shuleni hapo kutokana na mfululizo wa wanafunzi wa kike kuanguka na kuzimia.

Akizungumza na gazeti hili kuhusu maombezi hayo, Diwani wa Kata ya Nyamswa, Fyeka Sumera (CCM), alisema kumekuwa na mwendelezo wa matukio ya wanafunzi wa kike kuanguka na kupoteza fahamu katika kata yake na kata jirani ya Nyamang’uta.

Alisema baadhi yao huzinduka wakiwa hospitalini na wanapofanyiwa uchunguzi  wanakuwa hawana tatizo, hivyo kuwafanya wanajamii kuhusisha jambo hilo na nguvu za giza.

“Mimi binafsi siamini katika jambo hili lakini tunawatahadharisha watu wanaojihusisha na usanii huu waache, pamoja na maombi haya ambayo kwa kiasi fulani yameleta ufanisi lakini tunaendelea kufuatilia zaidi kubaini nini chanzo cha tatizo hili,” alisema.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyamswa, Marwa Ghati, alisema walikutana na wazazi na baadhi ya wanafunzi 70 ambao hukumbwa na tatizo hilo na wamekuwa wakishutumiana wenyewe kwa wenyewe kujihusisha na ushirikina.

Alisema aliamua kutoa taarifa kwa wazazi na uongozi na walikubaliana njia ya kwanza kukabiliana na tatizo hilo ni kufanya maombi na njia nyingine zinafuata kubaini tatizo na kulikomesha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles