25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mwalimu shule ya msingi akutwa na bunduki ya AK47

Na JANETH MUSHI

-ARUSHA

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limemkamata Mwalimu wa Shule ya Msingi Naan, Solomon Kipuker (30), kwa tuhuma za kukutwa na bunduki ya kivita aina ya AK47 iliyokuwa na risasi tano zilizokuwa katika magazine.

Jeshi hilo pia  linawashikilia watuhumiwa wengine 12 wakiwemo watatu wanaodaiwa kuwa majangili sugu, ambao wamekutwa na vipande vinne vya meno ya tembo ambavyo thamani yake haikuwekwa wazi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, ACP Jonathan Shanna, alisema mwalimu huyo anayefundisha katika shule hiyo iliyopo Kata ya Enguserosambu, Tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro, alikamatwa Juni 2, mwaka huu.

Shanna alisema jeshi hilo limefanikiwa kumkamata mwalimu huyo kwa kushirikiana na kikosi kazi kabambe dhidi ya ujangili na uhalifu wa silaha za moto Kanda ya Ziwa chini ya uwezeshwaji wa TANAPA.

Alisema  mtuhumiwa huyo ni miongoni mwa wafanyabiashara haramu wa uingizaji wa silaha za moto nchini pamoja na biashara ya nyara za Serikali ikiwemo pembe za ndovu na faru na shughuli nyingine za ujangili.

“Mara baada ya kumhoji alikiri kumiliki silaha hiyo ya kivita kwa kushirikiana na watuhumiwa wengine ambao bado wanatafutwa, na silaha hizo zimekuwa zikitumika katika mapigano ya kikabila baina ya jamii za wasonjo/watemi na wamasai na zimekuwa zikikodishwa katika matukio mbalimbali ya ujambazi na utekaji wa watalii,wananchi na mali zao.

“Hii ni mara yangu ya kwanza tangu nijiunge na Jeshi la Polisi kumkamata mtuhumiwa ambaye ni mtumishi wa umma yuko kwenye orodha ya malipo, anapewa mshahara halali na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akijihusisha na matukio ya ujambazi.

“Mimi nilipoambiwa na kile kikosi kabambe kwamba kimemkamata mwalimu akiwa na silaha hii, nilidhani ni mwalimu wa ujambazi, lakini nimemhoji kwa kina ni mwalimu halali wa shule ya msingi lakini anajihusisha na ujambazi.

“Silaha hizi zimekuwa zikitafutwa kwa muda mrefu, kama nilivyoahidi tutafanya msako wa nyumba kwa nyumba, barabara kwa barabara, uvungu kwa uvungu, pori kwa pori ni bandika bandua mpaka kieleweke,” alisema Kamanda Shanna.

Mbali na tukio hilo, katika Kijiji cha Mbukeni, Kata ya Arash, Tarafa ya Loliondo ilikamatwa silaha nyingine aina ya AK47 ikiwa na risasi moja imetelekezwa katika ofisi ya kijiji hicho.

Wanaodaiwa kutelekeza silaha hiyo wanaendelea kutafutwa na jeshi hilo.

Kuhusu watuhumiwa wa ujangili, Kamanda Shanna alisema Mei 30 mwaka huu, walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao watatu (majina yamehifadhiwa), waliokutwa katika Kitongoji cha Maji ya chai, Tarafa ya King’ori, Wilaya ya Arumeru, ambao wanadaiwa kujihusisha na ujangili wakiwa na vipande vinne vya meno ya tembo.

“Watuhumiwa hao watatu ambao tumewahoji na wamekiri kujihusisha na biashara na ya ujangili wakiwa na vipande hivyo walivyokuwa wamehifadhi kwenye mfuko wa sarandusi na upelelezi ili kuwabaini washirika wenzao unaendelea,” alidai Kamanda Shanna.

 Katika tukio la tatu, alidai wanawashikilia watuhumiwa watatu ambao ni Hamis Juma (37), Isiaka Islamu (22) na Hassan Mush i(54), wakiwa na pikipiki nne ambazo hutumika katika matukio ya wizi ambazo ni MC 978 CAH aina ya Haojue, MC 559 BHT aina ya Toyo, MC 427 BKP na MC 789 aina ya Boxer.

Alisema wanaendelea kuwahoji watuhumiwa wote na watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles