24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali yatoa msimamo mikopo yenye masharti magumu

Na RAMADHAN HASSAN

-DODOMA

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema hayuko tayari kusaini mikataba ya mikopo kutoka kwa wahisani yenye masharti magumu, ikiwamo kuchukua mali za jeshi na migodi endapo Serikali ikishindwa kulipa.

Dk. Mpango alitoa kauli hiyo juzi bungeni wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge walizotoa wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya wizara yake, hususan madai ya wizara hiyo kuchelewa kusaini mikataba mbalimbali.

Akiwasilisha hotuba ya wizara yake, Dk. Mpango alitaja changamoto za utekelezaji wa bajeti ya 2018/19 kuwa ni pamoja na masharti yasiyo rafiki ya mikopo katika masoko ya fedha duniani na kupungua ama kutopatikana kwa wakati kwa fedha za washirika wa maendeleo kugharamia miradi ya maendeleo.

Jioni ya siku hiyo akihitimisha hotuba yake hiyo, Dk. Mpango alisema inachokifanya Serikali ni kupitia  masharti ya mikataba ili kujiridhisha kama kinachoelezwa kinawiana na fedha ambazo Serikali itakopeshwa.

“Serikali tunapitia masharti ya mikataba ili kujiridhisha kama kilichoelezwa kinawiana na fedha ambazo Serikali itakopeshwa na kama tukiona kuna uhalisia tutaisaini, hakuna asiyetaka kutekeleza miradi hiyo muhimu.

“Siko tayari kuhukumiwa kwa kusaini mikataba inayotaka kushilikiliwa mali za jeshi na migodi yetu pale ambapo Serikali ikishindwa kulipa madeni,” alisema Dk. Mpango.

Mikataba iliyokuwa ikizungumziwa ni pamoja na ule wa ujenzi wa uwanja wa ndege Zanzibar, Bandari ya Mpinga Nduri na upanuzi wa Mto Msimbazi.

Pia, Dk. Mpango alisema wameziandikia barua wizara na taasisi kuzitaka kuzingatia sheria ya bajeti pale wanapotaka kutoza kodi na tozo mbalimbali.

Alisema wizara yake imekuwa ikiwataka wadau kuwasilisha kodi na tozo wanazopendekeza ili kuondoa mgongano kwa taasisi kutoza kodi zinazofanana.

Kuhusu ulipaji madeni, alisema Serikali inaendelea kutenga fedha kulipa yaliyohakikiwa.

“Madeni yakishahakikiwa yanawasilishwa kwa maofisa masuhuli, hivyo maofisa masuhuli wanatakiwa kuwajulisha wahusika ambao madai yao yamekataliwa ili wafahamu,” alisema.

Alisema uhakiki wa madeni ya mwaka 2017/18 hadi 2019 umeanza na utakamilika ikifika Agosti.

Pia alisema kuwa Serikali inajielekeza kukusanya mapato ya ndani lengo ikiwa bajeti kubwa ya Serikali itumie mapato ya ndani.

Alisema Serikali inaendelea kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa deni la taifa ambalo kila mwaka lazima wafanye uthamini wake.

“Tunafanya majadiliano na nchi ambazo si mwanachama wa Paris Club kuangalia uwezekano wa kutusamehe madeni yao, lakini pia tunahakikisha mikopo ya ndani inazingatia uwezo wa soko na kukopa bila kupunguza uwezo wa taasisi mbalimbali kukopesha sekta ya ndani.

“Kukopa si dhambi ili mradi mikopo ielekezwe kwenye kuzalisha mali na uwezo wa nchi katika kulipa,” alisisitiza Dk. Mpango.

AMJIBU ZITTO

Akijibu madai yaliyotolewa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), kwamba kumbukumbu za madeni ya Serikali zinatunzwa kwenye madaftari, waziri huyo alisema madai hayo yamelenga kupotosha.

“Naomba niseme tuhuma alizozitoa Zitto ni ‘very serious’, haiwezekani tukatunza takwimu za deni la Serikali kwa “counter book”. Si kweli ni udhalilishaji wa Serikali. Alipaswa kufuta kauli hiyo,” alisema.

Alisema katika kutunza madeni hayo, Serikali inatumia mfumo wa utunzaji madeni unaotumika kwa nchi za Jumuiya ya Madola tangu mwaka 1996.

“Usipoteshe umma hata kidogo. Takwimu za deni ni sahihi. CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) hazuiliwi kufanya ukaguzi wa deni la taifa na hata akitaka kuhakiki atafanya hivyo.

“Tofauti zinaweza zikaja kwa tofauti ya “exchange rate” (viwango vya kubadilishia fedha) au “human era” (makosa ya kibinaadamu). Hata kukiwepo kwa makosa hayo majadiliano yanafanyika,” alisema.

Kuhusu ukusanyaji mapato kudaiwa kushuka, Dk. Mpango alisema Zitto hafahamu suala hilo vizuri kwa sababu masuala ya kisiasa yanamchanganya.

“Nadhani siasa inakuchanganya. Uwiano wa pato la taifa ni kweli unachukua makusanyo ya kodi unagawanya na pato la taifa. GDP imeongezeka kwa kasi kuliko makusanyo ya kodi.

“Ni muhimu pato la taifa liendane na ukuaji uchumi. Wakati ule tulikuwa tukitumia kizio cha mwaka 2007, kuna mabadiliko makubwa tangu wakati ule hadi sasa.

“Muhimu kuzingatia baadhi ya nchi za Afrika Mashariki bado hazijabadilisha vigezo vya ulinganifu kama tulivyokubaliana,” alisema.

VITAMBULISHO VYA WAJASIRIAMALI

Pia Dk. Mpango alizungumzia madai yaliyotolewa na baadhi ya wabunge kuhusu utaratibu uliotumika kugawa vitambulisho vya wajasiriamali.

“Malipo ya vitambulisho yapo kisheria na yanaratibiwa kupitia Sheria ya Usimamizi wa Kodi sura 438 ambayo ilimpa mamlaka Kamishna Mkuu wa TRA kuwatambua wafanyabiashara wadogo na watoa huduma na wengine ambao mauzo ghafi hayazidi Sh milioni 4.

“Vitambulisho viko kisheria ni suala la mgawanyo wa majukumu na kama Serikali lazima itumie mtandao mpana kwa wale wanaoweza kuwafikia Watanzania kwa urahisi,” alisema.

NAIBU WAZIRI ALIA NA MAKUSANYO

Akihitimisha mjadala wa wizara hiyo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashantu Kijaji, alisema si kweli kwamba makusanyo ya kodi yameshuka.

“Watanzania wanaona yanayotendeka kupitia makusanyo ya kodi. Kama makusanyo yameshuka tungeweza wapi kutekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), kama makusanyo yangekuwa ya chini, tusingeweza kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme kwenye Mto Rufiji,” alisema.

Alisema kabla ya awamu ya tano kuingia madarakani, mwaka 2014/ 15 makadirio ya makusanyo yalikuwa Sh trilioni 11.9, kilichokusanywa ni Sh trilioni 10.66.

“Mwaka 2017/18 makadirio yalikuwa kukusanya Sh  trilioni 17.3, lakini tulikusanya Sh trilioni 15.25. Ukilinganisha mambo hayo mawili unaweza ukabaini kama mapato yamepungua au la. Takwimu za kodi hazijawahi kudanganya,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles